Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Kibaya awafuata Samatta, Ngassa

Wed, 28 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabao matatu ‘hat trick’ ya mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Jaffary Kibaya aliyofunga jana dhidi ya Northern Dynamo, yamemfanya atembee katika nyayo za Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa.

Mtibwa ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya timu hiyo ya Shelisheli katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.

Ngassa na Samatta ndiyo walikuwa Watanzania pekee kufunga mabao matatu na zaidi kwenye mchezo mmoja wa mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu na hakuna mwingine aliyewahi kufanya hivyo.

Ngassa alifunga ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 7-0 ambao Yanga ilipata dhidi ya Komorozine ya Comoro mwaka 2014 katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini.

Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji alimlipa Ngassa mwaka uliofuata baada ya kuifungia TP Mazembe ya DRC idadi hiyo ya mabao katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Moghreb Tetouan ya Morocco jijini Lubumbashi.

Kibaya naye amewajibu kwa kufunga idadi kama hiyo ya mabao dhidi ya Dynamo.

Mabao hayo aliyafunga dakika ya 13, 35 na 57 katika mechi hiyo ambayo ilitawaliwa na Mtibwa.

Dalili za Mtibwa kupata ushindi mnono kwenye mchezo wa jana zilijionyesha dakika ya mwanzo kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Dynamo.

Hata hivyo, safu yake ya ushambuliaji ilionekana kuwa na papara na tamaa ya kila mchezaji kutaka kufunga bao jambo lililosababisha wapoteze nafasi nyingi ambazo walitengeneza.

Kibaya ambaye alionyesha utulivu, aliipatia Mtibwa bao la kuongoza dakika ya 13 akimalizia vyema pasi ya winga Salum Kihimbwa aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Dynamo.

Mtibwa ilipata bao la pili dakika 10 kabla ya mapumziko baada ya Kibaya kufunga kwa shuti kali la mguu wa kulia akimalizia pasi ya Juma Liuzio.

Kipindi cha pili Mtibwa iliendelea kutawala na dakika ya 57 Kibaya alifunga bao la tatu kwa mkwaju wa penalti.

Riphat Khamis aliyetokea benchi alifunga bao la nne dakika za lala salama. Mtibwa imeendeleza rekodi ya kutopoteza mechi ya hatua ya kwanza inapocheza nyumbani kwa mara ya tano baada ya kufanya hivyo mwaka 2000, 2001, 2002 na 2004.

Mtibwa inatakiwa kufanya maandalizi kabambe kujiandaa na KCCA ya Uganda kati ya Desemba 14 na 16 kabla ya kurudiana Desemba 21 na 23.

Mtibwa: Shabani Kado, Ally Shomari, Cassian Ponera, Dickson Daudi, Issa Rashid, Ismail Aidan, Ally Makarani, Shabani Nditi, Salum Kihimbwa, Jaffary Kibaya na Juma Liuzio/Riphat Khamis.



Chanzo: mwananchi.co.tz