Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS), Ligi Kuu Tanzania Bara inashika namba sita kwa ubora barani Afrika nyuma ya vinara Misri, Morocco, Algeria, Tunisia na Afrika Kusini. Takwimu hizo zilitolewa Januari 2024.
Ukiangalia orodha hiyo katika nne bora unazikuta nchi za Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika ambazo zimekuwa zikitawala soka kwa ujumla. Wanaofuatia ni Afrika Kusini, wote tunafahamu ukuaji wa soka lao unavyokuja kwa kasi kwenda kuwatibulia Kaskazini.
Ubora huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara umewafanya viongozi wetu kufikiria kuitambulisha teknolojia inayomsaidia mwamuzi kufanya marejeo ya picha (Video Assistance Referee-VAR) katika kufanya uamuzi sahihi wa matukio mbalimbali.
Matumizi ya VAR katika Ligi Kuu Bara ni wazo zuri lakini muda sahihi wa kuitambulisha teknolojia hiyo bado haujafika, pengine tudili la vitu vingine tofauti na mzigo huo mkubwa tunaotaka kujitwisha.
Katika ligi yetu kuna changamoto nyingi ambazo zinaweza kufanyiwa kazi kupitia gharama tunazotaka kuzitumia kwenye utumiaji wa VAR.
Ukweli uliowazi ni kwamba, matumizi ya VAR yanahitaji gharama kubwa, achana na gharama za kununua vifaa vyenyewe, pia kuna wataalamu wa kusimamia na utoaji wa elimu kwa waamuzi kwani si kitu ambacho kinaweza kutumika kwa mazoea, lazima iwepo elimu mahususi.
Licha ya kwamba Serikali imeondoa kodi ya uingizaji wa vifaa vya teknolojia hiyo, lakini bado tunakuja kubanwa katika kuwapata wataalamu wa kuvifunga na kuviendesha, lakini pia tusisahau hali ya miundombinu ya viwanja vyetu.
Tumeona wakati Afrika inatambulishwa teknolojia hiyo ambayo imekuwa ikitumika zaidi katika michuano iliyopo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuna kozi mbalimbali zimekuwa zikiendeshwa kwa waamuzi kuhusu matumizi ya VAR.
Ikumbukwe kwamba, mpango wa matumizi ya VAR kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara umeshaanza kufanyiwa kazi ambapo Caf kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivi karibuni waliendesha mafunzo ya awali ya kufunga vifaa hivyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam yakiongozwa na Meneja wa Teknolojia ya Soka kutoka CAF, Wael Elsebaie.
Mafunzo hayo ya kuvifunga sambamba na kuviendesha vifaa hivyo yalishirikisha jumla ya watu sita wakiwemo Watanzania wanne na Wakenya wawili. Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, inafahamika kuwa yataanza mafunzo kwa waamuzi waweze kutumia VAR katika michezo mbalimbali.
Baada ya Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba Juni 13, 2024 wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2024/2025 kusema Serikali imekusudia kuwasilisha pendekezo la kuondoa kodi kwenye vifaa vya teknolojia ya VAR kuanzia mwaka mpya wa fedha, jambo hilo limefanyiwa kazi.
Amesema uamuzi huo utawezesha viwanja vyote hapa nchini vinavyotumika kuchezwa ligi hiyo kufungwa VAR lengo likiwa ni kuhakikisha matokeo yanayopatikana yanakuwa ya haki. Lakini kiuhalisia Uwanja wa Benjamin Mkapa pekee ndiyo umekuwa ukitumiwa kwa majaribio na ndiyo utafungwa teknolojia hiyo kwa sasa.
Pia Serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya vya mpira wa miguu na kukarabati baadhi ya vilivyopo, kuhusu ubora wa eneo la kuchezea (pitch) tayari Serikali ilitunga sheria inayotoa msamaha kwenye uingizaji wa nyasi bandia na vifaa vyake.
VAR imekuwa ikitumika kwenye ligi na mashindano mbalimbali duniani kwa sasa yakiwemo ya Euro yanayoendelea nchini Ujerumani.
Kwa Tanzania hii itakuwa mara ya kwanza kufanyika kwenye ligi lakini ikiwa imeshatumika kwenye michuano ya kimataifa, ukiwemo mchezo wa Yanga na Mamelodi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Al Ahly msimu uliopita, lakini pia Simba ilikumbana nayo tena kwenye mchezo wa African Football League ilipovaana na Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa.
Ukiachana na kuwepo kwa malalamiko ya baadhi ya timu kunyimwa haki yao kutokana na matukio ya utata uwanjani, lakini kilio kikubwa cha makocha, wachezaji na hata mashabiki ni ubora wa viwanja vyetu hasa sehemu ya kuchezea (pitch).
Mamlaka zinapaswa kuanza kuboresha 'pitch' kabla ya kufikiria VAR kwani ukiangalia hata walipokuja na wazo la kufunga taa viwanjani ili kutoa mwanya wa mechi zingine zichezwe usiku, bado mpango huo umekuwa na changamoto kubwa.
Septemba 16, 2023 wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji Kagera Sugar na Geita Gold uliochezwa usiku kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, taa zilizimika na kuufanya mchezo huo kuahirishwa dakika ya 39, ukaendelea kesho yake kwa kuchezwa kuanzia saa 10 jioni.
Hiyo ni changamoto mojawapo ya matumizi ya taa viwanjani. Ukiondoa Uwanja wa Mkapa na Azam Complex, viwanja vingine vilivyofungwa taa vina changamoto ya taa hizo kutokuwa na ubora ambapo ukiangalia mechi kupitia runinga, hufurahii mchezo kwani kuna vivuli vingi vya wachezaji.
Tunataka kuona boli likitembea na siyo hivi sasa hali ilivyo katika viwanja vingi ambavyo tunashuhudia kipindi cha mvua matope yanaondoa ladha ya mchezo wa soka.
Baadhi ya viwanja ambavyo vinahitaji kufanyiwa maboresho katika sehemu ya kuchezea ili vitumike vizuri kwa mechi za Ligi Kuu msimu ujao ni Jenerali Isamuhyo (Dar), Sokoine (Mbeya), Lake Tanganyika (Kigoma), Liti (Singida) na Jamhuri (Dodoma).
Serikali ndiyo imeondoa kodi katika ishu nzima ya uingizwaji wa nyasi bandia hapa nchini lengo likiwa ni kuvifanya viwanja vingi kuwa bora sehemu ya kuchezea, lakini bado hakuna kilichofanyika kuviboresha kwa asilimia kubwa.
Azam Complex (Dar), Mkapa (Dar), Majaliwa (Lindi), Kaitaba (Kagera) ndiyo viwanja vyenye 'pitch' nzuri kutokana na ule wa Mkapa kuwa na nyasi asili, huku hivyo vingine ni bandia. Hivi sasa kuna maboresho yanafanyika kwenye Uwanja wa Mkwakani pale Tanga, tunategemea kuona maboresho hayo yakikamilika mambo yatakuwa mazuri.
Tunaamini msukumo wa kufunga vifaa vya VAR unachangiwa na ukweli kwamba Tanzania itaandaa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, lakini wakati presha hiyo ikiongezeka ni vyema nguvu kubwa ikawekwa kwenye pitch kwa sababu timu zitakazokuja kuweka kambi hapa zitahitaji pia viwanja bora za mazoezi achilia mbali vitakavyotumika kwa mechi za michuano hiyo tutakayoiandaa kwa ushirikiano na Kenya na Uganda.
WADAU WANASEMAJE
Mkurugenzi wa zamani wa soka la Tanzania, Ammy Ninje ambaye aliwahi pia kukinoa kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, anaamini uboreshwaji wa viwanja unatakiwa kuwekewa uzito kabla ya kuanza kutumika kwa VAR katika michezo ya ligi na Kombe la Shirikisho (FA).
"Kuwa na VAR itakuwa ni hatua nzuri lakini ni vizuri kwanza kuboresha viwanja vyetu kwa kasi, viwe katika ubora fulani, isiwe viwanja vichache huku vingine eneo la kuchezea likiwa sio rafiki, naamini viongozi wetu ni wasikivu na mipango yao ni mizuri kwa manufaa ya soka letu," alisema.
Kwa sasa Ninje yupo zake Uingereza huku akifanya kazi kwa karibu na Nottingham Forest katika programu zao mbalimbali ikiwemo kuendeleza vijana.
Kocha wa timu za vijana za Azam FC, Mohamed Badru ameshauri kwa kuanzia teknolojia hiyo ianze kutumika katika michezo maalum kama sehemu ya majaribio wakati tukiboresha miundombinu yetu ya viwanja taratibu.
"Ni kweli kwamba kuna baadhi ya viwanja miundombinu yake hasa maeneo ya kuchezea sio rafiki, sasa sio mbaya kuwa na VAR ila tunatakiwa kuitumia huku tukiboresha maeneo ya kuchezea," alisema kocha huyo wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar.
Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema; "Ni jambo zuri kuendana na teknolojia, tusubiri kwanza tuone itafanya kazi kwa namna gani ndio tutoe maoni yetu."
KUHUSU VAR
Teknolojia ya VAR ilizinduliwa rasmi Aprili 2017 na ilitumiwa kwa mara ya kwanza katika mechi kati ya Sydney FC na Wellington Phoenix kwenye Ligi ya Australia A.
VAR hutumiwa kuchunguza na kufanya uamuzi katika matukio manne muhimu wakati wa mechi ikiwa ni pamoja na bao, kadi nyekundu, uamuzi wa penalti na utambuzi usio sahihi wakati wa kutoa kadi.
Barani Afrika, utekelezaji wa kutumia teknolojia hiyo umekuwa wa taratibu sana kwani hivi sasa hutumiwa katika mashindano ya klabu kuanzia hatua ya robo fainali hadi fainali. Pia imetumika kwenye AFCON sambamba na majaribio ya mashindano mengine yakiwemo ya wasichana.
Sababu ya kutumiwa kwa uchache teknolojia hiyo barani Afrika imeelezwa ni kutokana na gharama kubwa ya kununua vifaa na kuna changamoto ya kuvifunga kwenye viwanja. Suala la kufunga imekuwa changamoto kubwa kwa sababu klabu nyingi barani Afrika hazimiliki viwanja vyao, bali zinakodi kwa muda.
Hata hivyo, Rais wa Fifa, Gianni Infantino amefichua kwamba kuna mpango wa kutengeneza toleo rahisi zaidi la VAR kwa ajili ya nchi za kipato cha chini. Kulingana na Infantino, Fifa linafanya majaribio na teknolojia mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia mataifa ambayo hayawezi kumudu teknolojia ya kawaida.
Shirikisho la Soka la Scotland lilikadiria gharama ya VAR ya kawaida kuwa dola milioni 1.45 (sawa na takribani Sh3.78 bilioni za Tanznaia) kwa msimu kwa Ligi Kuu yao ya timu 12.
Kuna aina mbili zilizobuniwa; 'VAR Lite' itahitaji angalau kamera 4 mpaka 7 wakati nchi zilizo katika hali ya chini kiuchumi zinaweza kutumia kinachoitwa "VAR-zero" ambayo inahitaji kamera moja tu.
Mambo hayo yote yanaifanya teknolojia hiyo ambayo Tanzania tunataka kuitumikia katika ligi yetu inafanya kuwa ni ngumu kutokea kwa sasa.