Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VAR kutua leo Dar

Var Pic Data.png VAR kutua leo Dar

Thu, 14 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Leo Alhamisi wataalamu wa teknolojia ya Video Assistants Referee (VAR) kutoka Misri wanatinga nchini tayari kwa kufunga mitambo yao na kuijaribu kwa ajili ya mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayozikutanisha Simba na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Jumapili ijayo.

Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na vigogo wa Simba wamesema kufungwa kwa teknolojia hiyo kutasaidia kuondoa makandokando yote yanayojitokeza kwenye mechi kubwa hasa za mtoano.

Simba sasa imeingia kambini ikijiandaa na mechi hiyo na lengo lao kubwa ni ushindi mnono nyumbani ili kujipa kazi rahisi ugenini wakati wa marudiano Aprili 24 mwaka huu.

Meneja wa Uwanja wa Mkapa, Godon Nsajigwa aliliambia Mwanaspoti wataalamu hao wataingia nchini kati ya siku hizo mbili Alhamisi ama Ijumaa ili kuweka sawa kila kitu uwanjani hapo.

Teknolojia hiyo itawahusisha CAF, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Azam TV na Simba ambao ndio wenyeji wa mechi hiyo.

Wakati meneja huyo akielezea hilo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Ngh’ambi aliliambia Mwanaspoti VAR itawasaidia kuwa haki yao na kwa kila mdau wa mechi hiyo.

“Si kwetu tu, hata kwao na wadau wote wa soka, maana kuna mambo mengi yanatokea ambayo watu hawawezi kuyaona kwa urahisi lakini kupitia VAR itawarahisishia, mfano mechi iliyopita ilikuwa na mambo kama manne hivi ambayo hayakuwa sahihi kwetu lakini hakuna aliyeyaona,” alisema na kuongeza.

“Kupitia hili ni faida kubwa kwetu hata tutakapoenda kucheza mechi ya marudiano itatusaidia kwa kila timu kupata haki sawa, umakini utakuwa mkubwa uwanjani,” alisema Mulamu.

Kuhusu maandalizi yao bosi huyo alisema kila kitu kinakwenda sawa kwani timu yao imeanza kujifua.

“Timu ipo kambini, tunaamini kila mmoja anatambua umuhimu wa hii mechi, tunataka ushindi mnono kwani hatua tuliyofikia ni mtoano hivyo ni lazima tuwatoe Orlando.

“Watu wakumbuke kuna mambo mawili, ushindi na kumtoa Orlando, hivyo sisi tunataka kumtoa Orlando kwenye michuano hii na njia pekee ni kufanya vizuri nyumbani na ugenini,” alisema

Mulamu alisema kuelekea mechi hiyo muhimu kutakuwa na bonasi kama kawaida yao lakini huenda ikaongezekana kulingana na ukubwa wa mechi. “Bonasi ni kawaida hasa tunaposhinda ama sare lakini ongezeko la bonasi inategemea na namna ambavyo bosi anaamua, ila hii ni mechi muhimu sana kwetu ambayo tunapaswa tushinde,” alisema

Imeelezwa kwamba Orlando huenda wakaingia Ijumaa asubuhi ingawa wenyeji wao hawana taarifa hadi sasa; “Sio lazima umpe taarifa mwenyeji wako kama kila kitu unajigharamia mwenyewe, hivyo wataingia kwa ratiba yao.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz