Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uzembe ulivyoiponza Simba, Kagera sare

Simba Kaitaba Mchezo wa Kagera vs Simba ulimalizika kwa sare ya bao 1-1

Sun, 25 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa msimu wa pili mfululizo, Simba imeshindwa kuondoka na pointi tatu kwenye Uwanja wa Kaitaba, dhidi ya Kagera Sugar, baada ya juzi usiku kulazimishwa sare ya bao 1-1 na wenyeji wao.

Simba ambayo iliingia katika mchezo huo ikiwa imetoka kupata ushindi mnono wa ugenini wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Gold, iliwalazimu kutoka nyuma na kusawazisha bao la kuongoza la Kagera Sugar na kufanya mechi hiyo imalizike kwa sare hiyo ambayo imeifanya Simba kupunguzwa kasi katika mbio za ubingwa, ikijikuta imeachwa kwa pointi sita na vinara Yanga wenye pointi 44 huku wao wakiwa na pointi 38.

Makosa mepesi yaamua matokeo

Mabao yote mawili ya mchezo huo wa juzi yalisababishwa na makosa ya kizembe ambayo kama wachezaji wa timu hizo mbili wangetimiza wajibu wao wa kawaida wa kujilinda, pengine yasingepatikana kirahisi.

Bao la Kagera Sugar lililofungwa na Deus Bukenya katika dakika ya 15, lilitokana na kujipanga na kusimama vibaya kwa wachezjai wa Simba wakati wapinzani wao walipokuwa wanapiga mpira wa kona.

Mfungaji wa bao, alitokea nyuma ya ukuta wa Simba pasipo kudhibitiwa na mchezaji yeyote na akamalizia kwa kichwa bila bughudha mpira ambao haukuokolewa na walinzi wa Simba pamoja na kipa wao Aishi Manula.

Goli la kusawazisha la Simba lililopachikwa na Henock Inonga katika dakika ya 39, ni matokeo ya wachezjai wa Kagera Sugar kumuacha mfungaji aruke akiwa huru kuunganisha mpira wa faulo uliochongwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ akiandika asisti yake ya tano kwenye ligi msimu huu.

Kabla ya hapo, beki Abdallah Mfuko alifanya kosa la kizembe la kumchezea rafu, Mzamiru Yassin ambaye hakuwa katika eneo ambalo lingeleta madhara langoni mwake na alikuwa ameshalipa mgongo goli.

Simba ilikosa ubunifu

Moja ya mbinu ambazo zimekuwa zikiigharimu Simba inapochelewa kupata ushindi ni ile ya kutumia mipira ya juu kuwalisha wachezaji wake wa nafasi ya ushambuliaji.

Kwa mara nyingine hilo lilijitokeza juzi ambapo licha ya kutokuwa na namba kubwa jirani na lango la Kagera Sugar, Simba ililazimisha kutumia mbinu hiyo ambayo iliwasaidia wapinzani wao katika kujilinda. Huku kiungo mbunifu wa Simba, Clatous Chama akipewa Abdallah Seseme ambaye alimganda kama kivuli na kumnyima uhuru wa kuidhuru Kagera.

Makame ni yuleyule wa juzi, jana na leo

Abdulaziz Makame ni mchezaji mwenye umbo na uwezo mzuri wa kucheza katika nafasi ya kiungo mkabaji lakini amekuwa na tabia ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikimrudisha nyuma na kuathiri mafanikio katika kazi yake ya kucheza soka.

Tabia hiyo ya Makame ni kucheza rafu zisizo na ulazima ambazo nyingi huwa za hatari ambazo zimekuwa zikimsababishia kadi pamoja na kuigharimu timu yake. Hilo lilijidhihirisha juzi ambapo muda mfupi tu baada ya kuingia alifanya faulo mara mbili tofauti ambazo hazikuwa na ulazima jirani na lango lake, ambazo kama Simba ingezitumia vyema, ingepata mabao zaidi.

Kagera yatoa darasa

Kwa mara nyingine tena dhidi ya timu iliyo katika nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa ligi, Kagera Sugar ilionyesha kiwango bora kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu na kupiga pasi nyingi zilizofikia walengwa kwa usahihi na kuilazimisha Simba itumie mipira mirefu ya juu baada ya kuzidiwa katika umiliki wa mpira. Huu ni utamaduni wa kocha Maxime ambao amekuwa akiendelea nao na kuuonyesha katika kila timu ambayo amekuwa akiifundisha.

Hili ni somo kwa makocha na timu nyingine kujitahidi kuwa na falsafa zao ambazo zitakuwa zinawatambulisha pasipo kujali aina ya matokeo ambayo yatakuwa yanapatikana kama ilivyo kwa Kagera Sugar ambayo iwe imefungwa, imeshinda au imetoka sare, itamiliki mpira.

Chanzo: Mwanaspoti