Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwanja mpya wa Afcon waanza kujengwa

Uwanja Mksz Uwanja mpya wa Afcon waanza kujengwa

Tue, 19 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetoa Sh286 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu mkoani Arusha uliopewa jina la Dk Samia Suluhu Hassan utakaojengwa na Kampuni ya China Railway Construction Engineering Group Limited (CRCEG) kutoka nchini China.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amesema hayo leo Machi 19, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa uwanja huo. Dk Ndumbaro amesema kuwa uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuingiza watu 30,000 na ni wa kisasa zaidi katika nchi za Afrika Mashariki.

Amesema Serikali itahakikisha ujenzi huo unafanywa kwa haraka kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon), ifikapo mwaka 2027, ikiwa ni juhudi za Rais Samia.

Amesema kuwa mbali ya mechi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, uwanja huo utachagiza kwa kiasi kikubwa utalii kwani zitafanyika shughuli mbalimbali tofauti na mpira wa miguu kama vile mchezo wa riadha pamoja na biashara zitakazokuwa zinafanyika uwanjani hapo.

"Uwanja huo utakuwa na ubora wa hali ya juu kwani utakuwa na vyumba vya watu mashuhuri pande zote mbili za uwanja zoezi hili limefanyika leo ambapo, Rais Samia akiwa anatimiza miaka mitatu ya uongozi wake,” amesema Dk Ndumbaro.

Ameipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kwa juhudi ilizofanya mpaka kukamilisha kuanza kwa ujenzi huo ambao umechukua muda mrefu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko amewataka wakandarasi wa uwanja huo wahakikishe ujenzi unakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

"Wakandarasi hakikisheni kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025 uwanja uwe umefikia kiwango kinachoridhisha na utekelezaji huo uanze haraka iwezekanavyo ikiwa ni maandalizi kuelekea katika michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon)," amesema.

Amesema kamati itatoa ushirikiano kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kama ilivyokusudiwa na kudai kuwa, Rais Samia anaitendea haki sekta ya michezo kama anavyofanya kwenye sekta nyingine, na kuwataka watu wa Arusha watunze rasilimali za uwanja huo.

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesema uwanja huo utaongeza idadi ya watalii katika Mkoa huo.

"Tunaahidi kuenzi ujenzi huo, tutahakikisha unajengwa usiku na mchana ili usiweze kukwama kwa upande wetu, tumeweka historia kubwa," amesema Mongella.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live