Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uwanja mpya AFCON watengewa bilioni 55

Uwanja Mksz Uwanja mpya AFCON watengewa bilioni 55

Fri, 24 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imetenga Sh. bilioni 55.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja mpya wa mpira wa miguu jijini Dodoma utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000.

Idadi hiyo ya watazamaji ni sawa na ya Uwanja wa Samia unaojengwa jijini Arusha kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 112 (Sh. bilioni 286).

Kutengwa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja wa kisasa jijini Dodoma kulitangazwa jana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbalo alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema uwanja huo unajengwa katika eneo changamani la michezo Dodoma kama ilivyo kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Alitaja shughuli zitakazotekelezwa katika ujenzi wa uwanja huo wa Dodoma ni pamoja na kuanza ujenzi wa kiwanja cha mpira wa miguu.

Ndumbaro alisema uwanja huo utajumuisha miundombinu ya uwanja wa ndani (indoor stadium), viwanja vya mpira wa mikono, pete na netiboli.

"Huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 hadi 2025," Ndumbaro alisema na kueleza kuwa serikali pia inaendelea na ujenzi wa Uwanja mpya wa Samia, jijini Arusha, ikitenga Sh. bilioni 125.3 kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema serikali inatekeleza miradi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambayo Tanzania ni mwenyeji ikishirikiana na majirani Kenya na Uganda.

Mchakato wa ujenzi wa uwanja wa kisasa Dodoma ulianza wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli, aliyeahidi kwamba Mfalme wa Morocco angetoa fedha kwa ajili ya mradi huo, lakini sasa serikali imeamua yenyewe kuutekeleza.

WASANII Katika hotuba yake, Ndumbaro pia alisema Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania katika mwaka 2024/25 umepangiwa Sh. bilioni tatu ambazo zitatumika kutoa ruzuku na mikopo kwa wasanii nchini.

Alisema serikali pia itaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau kwa ajili ya kuongeza mtaji ili wasanii wengi waweze kunufaika na kuwajengea uwezo ili kurasimisha kazi zao pamoja na kuziendeleza kibiashara.

"Kuhusu mradi wa ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, katika mwaka 2024/25 umetengewa jumla ya Sh. bilioni 1.5," Waziri Ndumbaro alisema na kuongeza kuwa:

"Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha ujenzi wa chuo kwa kufanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ikiwamo madarasa mawili, ukarabati wa uwanja wa ndani, ununuzi wa samani za chuo katika hosteli mpya iliyojengwa vikiwamo vitanda, magodoro na kabati pamoja na vitendea kazi vya chuo vinavyohusisha kompyuta na vifaa vya michezo."

Pia alisema mradi wa ujenzi wa Akademia ya Michezo Malya kwa mwaka 2024/25 umetengewa Sh. bilioni 10.2 kujenga miundombinu 193 vikiwamo viwanja vya mpira wa miguu, netiboli, kikapu, mikono, madarasa, bwalo la chakula, jengo la utawala na hosteli.

SIMBA, YANGA Daktari huyo wa sheria alisema watashirikiana na wadau wengine kuhakikisha Ligi Kuu Tanzania, hususan michezo za watani wa jadi, Simba na Yanga, inakuwa na thamani kubwa, timu zinatengeneza uchumi na zinafanikiwa kufika zaidi ya robo fainali katika mashindano ya kimataifa.

"Tutahakikisha tunaondoa migogoro kwa wadau wa utamaduni, sanaa na michezo kwa kuwa na katiba mfano kwa vyama na mashirikisho yote itakayotumiwa na wote ili kuboresha usimamizi katika utekelezaji majukumu kwa vyama na mashirikisho ya utamaduni, sanaa na michezo nchini," alisema.

Waziri huyo alisema watatunga kanuni za uwazi katika matumizi ya fedha kwa vyama na mashirikisho ya michezo, pia kutunga na kuhuisha sera, mikakati, sheria, miongozo na kanuni za usimamizi wa sekta za utamaduni, sanaa na michezo ili kuzifanya zijiendeshe kibiashara zaidi, kuzalisha ajira na kujenga uchumi.

Alisema serikali itaendelea kuwezesha na kuzigharamia timu 10 za taifa kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Ili kutekeleza mikakati hiyo, Waziri Ndumbaro aliomba Bunge kuidhinisha Sh. bilioni 285.318 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka ujao wa fedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live