Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uvamizi wa Ukraine wamuweka matatani bilionea wa Chelsea

Images   2022 02 24T200323.jpeg Uvamizi wa Ukraine wamuweka matatani bilionea wa Chelsea

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati mataifa yakiendelea kulaani kitendo cha Russia kuivamia Ukraine, hali inazidi kuwa ngumu kwa bilionea Roman Abramovich baada ya hoja ya kutaka avuliwe umiliki wa Chelsea.

Chelsea ni moja ya klabu kubwa na zenye mafanikio barani Ulaya, hadhi iliyoipata baada ya kuanza kumilikiwa na raia huyo wa Russia, tovuti ya Fortune imeripoti.

Abramovich, ambaye alijivunia mabilioni ya dola kutokana na biashara ya mafuta na ambaye anaripotiwa kuwa mtu wa karibu wa rais wa Russia, Vladimir Putin, aliinunua klabu hiyo ya London mwaka 2003.

Tangu awekeze klabuni hapo, Chelsea imetwaa mataji 18 makubwa, yakiwemo mawili ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Gazeti la The Times liliripoti mapema mwezi huu kuwa mali nyingi za Uingereza zenye thamani ya pauni 1.5 bilioni zilinunuliwa na raia wa Russia ambao wana uhusiano na serikali yao, huku karibu mali za thamani ya pauni milioni 430 zikiwa katikati ya London.

Wakosoaji wamelipachika suala hilo jina la "Londongrad."

Juzi majeshi ya Russia yalivamia Ukraine, huku serikali ikisema wataendelea kuunga mkono waasi wa nchi hiyo na majeshi hayataondoka hadi waone "matokeo".

Wakati suala hilo likiendelea kutikisa dunia, utajiri wa Abramovich unaanza kuangaliwa kwa makini zaidi pamoja na uhusiano wake wa karibu na Putin.

Mbunge wa chama cha Labour, Chris Bryant ndiye anayeongoza kampeni hiyo bungeni, akitaka Abramovich aondolewe katika umiliki wa Chelsea.

Jana alisema wakati wa maswali ya biashara bungeni kuwa aliziona nyaraka za kuanzia mwaka 2019 zikimuhusisha Abramovich na "shughuli chafu", imeandika tovuti ya Fortune.

Mwaka 2021, Abramovich alimshtaki mwandishi wa vitabu, Catherine Belton kwa kuandika katika kitabu chake cha "Putin's People" kuwa Abramovich alifanya shughuli nyingi za kibiashara "kwa maelekezo ya Putin", ukiwemo ununuzi wa Chelsea. Baadaye shauri hilo lilimalizwa.

Chris Bryant ameishauri serikali ya Waziri Mkuu Boris Johnson kutaifisha mali za Abramovich za nchini Uingereza, ikiwemo klabu ya Chelsea na kampuni yake ya uwekezaji ya Millhouse LLC, imeripoti BBC.

"Kwa kweli, Abramovich hatakiwi kuendelea kumiliki klabu katika nchi hii? Hakika, tunatakiwa tuangalie kutaifisha mali zake ... na kuhakikisha kuwa watu wengine wenye visa ya daraja la kwanza kama huyi hawahusiki katika shughuli chafu," Bryant aliliambia gazeti la The Guardian.

Tangu mwaka 1994, wakati Russia ikifungua uchumi hali kadhalika China, wawekezaji wa kigeni walikuwa na uwezo wa kununua ukazi wa Uingereza kwa kutumia programu ya "golden visa".

Lakini mpango huo ulisitishwa wiki iliyopita, wakati Puting alipozidisha tishio dhidi ya Ukraine, ikiwa ni baada ya kutuhumiwa kuendesha shambulizi la kemikali za neva kusini mwa jiji la Salisbury.Mmoja wa wanufaika wa mpango huo ni Abramovich.

Jumanne iliyopita, Boris Johnson alisema tayari Abramovich alikuwa anakabiliwa na vikwazo, lakini baadaye serikali ikakanusha.

Tayari Uingereza imeshaweka vikwazo kwa benki za Russia na matajiri wake.

Utajiri wa mafuta wa Abramovich umekuwa ukichunguzwa kwa miaka kadhaa na mwaka 2018, aliondoa maombi yake ya visa ya mwekezaji baada ya shutuma kuwa kubwa. Amekuwa akitumia hati ya kusafiria ya Israel kuingia Uingereza na hata wakati fulani kuishi kwenye boti zake za kifahari baada ya kukataliwa kuingia Uingereza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: