Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utatu tishio Ligi Kuu Bara 2023

Baleke Simba Nsd Utatu tishio Ligi Kuu Bara 2023

Thu, 11 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Zimebaki kama wiki mbili tu kabla ya pazia la Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023 halijafungwa rasmi mnamo Mei 28 kwa mujibu wa kalenda inavyosomeka kwa sasa.

Tayari dalili zinaonyesha Yanga inalitetea taji hilo kwa msimu wa pili mfululizo kutokana na pointi ilizonazo kwa sasa na idadi ya mechi zilizosalia, licha ya watani wao, Simba kuwafukuzia nyuma yao kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.

Kwa eneo la mkiani, ni miujiza pekee inayoweza kuzinusuru timu za Ruvu Shooting inayoburuza mkia, Polisi Tanzania inayoafuata juu yake na KMC kuepuka kushuka daraja moja kwa moja au kuingia kwenye play-off ya kupambana kuepuka kwenda Ligi ya Championship.

Hata hivyo, wakati ligi ikiwa ukingoni, mashabiki wa soka wameshuhudia vita nzito ya ufungaji mabao kwa mastaa wa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo ambayo huu ni msimu wa 59 tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mnamo mwaka 1965.

Mapro wa kigeni na wazawa wamekuwa wakichuana kutupia nyavuni ili kuwania tuzo ya Mfungaji Bora ambayo msimu uliopita ilibebwa na George Mpole aliyekuwa Geita Gold aliyemaliza na mabao 17, moja zaidi na yale yaliyofungwa na Fiston Mayele wa Yanga ambaye kwa sasa ndiye kinara.

Mayele anaongoza orodha ya wafungaji kwa sasa akiwa na mabao 16, idadi aliyomaliza nayo msimu uliopita, lakini akiwa na nafasi ya kuyaongeza iwapo atazitumia vyema mechi tatu zilizosalia za timu hiyo kabla ya msimu huu kumalizika zinazoweza pia kuipa Yanga taji lao la 29 la Ligi Kuu.

Achana na vita hiyo ya ufungaji wa mabao kwa wazawa na mapro wa kigeni, hapa chini ni orodha ya Tabo Bora ya utatu tishio katika kutupia mipira kambani kwenye Ligi Kuu Bara, huku safu za Simba na Yanga zikiwa tishio zaidi kutokana na kasi yao kuwa ya kiwango cha Pro-max. Endelea nayo...!

1) BALEKE, PHIRI NA BOCCO (SIMBA)

Hii ndio safu ya pili katika Ligi Kuu Bara hadi sasa, licha ya Simba kuwa kinara wa mabao katika ligi hiyo, japo washambuliaji Moses Phiri na John Bocco hawajafunga muda mrefu.

Utatu huo ni balaa kwani hadi sasa umezalisha mabao mengi ambao kwa sehemu kubwa imeifanya Simba iwe tishio zaidi msimu huu kwa kucheka na nyavu ikifunga jumla ya mabao 63.

Utatu huo umefunga jumla ya mabao 27 na hapo hajajumuishwa Saido Ntibazonkiza ambaye tangu atue Msimbazi katika dirisha dogo akitokea Geita Gold amekuwa na mchango mkubwa wa kufunga na kuasisti mabao ya timu hiyo iliyocheza jumla ya mechi 27 hadi sasa ikishika nafasi ya pili nyuma ya Yanga.

Phiri licha ya kutofunga tangu alipofanya hivyo mara ya mwisho Desemba 3 mwaka jana alipofunga mara mbili wakati Simba ikiizamisha Coastal Union kwa mabao 3-0 jijini Dar es Salaam, lakini mwamba huyo ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akifunga 10.

Mzambia huyo anafuatiwa kwa karibu na nahodha wa timu hiyo, Bocco mwenye mabao tisa, huku akiwa pia ndiye kinara wa hat trick hadi sasa akiwa amefunga mbili na kuendelea rekodi yake ya kufunga mabao katika misimu 14 mfululizo akifikisha jumla ya mabao 150. Kwa sasa Bocco hapati nafasi mara kwa mara lakini ni mmoja ya washambuliaji tishio na wasiotabirika katika kucheka na nyavu kwani nafasi yake kwa sasa inamilikiwa kibabe na Baleke.

Ndiyo, Baleke aliyesajiliwa dirisha dogo kama Saido, ndiye anayekamilisha utatu huo wa Msimbazi akifunga mabao manane pamoja na hat trick moja kwenye Ligi Kuu Bara na kama ataendeleza moto kwenye mechi tatu zilizosalia sio ajabu akawapiku wenzake wawili hao kwenye kutupia nyavuni.

Timu pinzani zinapata wakati mgumu zinapokutana na Simba kutokana na ukweli timu hiyo haitegemei mfungaji mmoja kama baadhi ya timu kwa vile ukiacha utatu huo pamoja na Saido mwenye jumla ya mabao 10 kwa msimu huu akiwamo manne aliyotoka nayo Geita, akiwa pia ni mkali wa kuasisti, lakini kuna Clatous Chama mwenye mabao matatu na kuasisti 15. Pia kuna kina Augustine Okrah aliyerejea upya uwanjani, Pape Ousmane Sakho, Kibu Denis na Habib Kyombo ambao wamechangia mabao 63 ya Simba hadi sasa.

2) MAYELE, AZIZ KI NA MZIZE (YANGA)

Licha ya Simba ndio inayoongoza kwa mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara, lakini ukweli safu tishio kwa kucheka na nyavu ni hii ya Yanga ambao utatu huo umefunga jumla ya mabao 30 na hapo imemkosa Feisal Salum 'Fei Toto' aliyejiondoa klabuni tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Hadi Fei Toto anajiondoa katika timu hiyo kwa maelezo amevunja mkataba na kugomewa na mabosi wake, mwamba huyo alikuwa amefunga jumla ya mabao sita na kama angekuwa anaendelea kuitumikia timu hiyo huenda angekuwa na mabao zaidi na pengine Clement Mzize asingeingia hapo.

Mayele ndiye baba lao kwa msimu wa pili mfululizo sasa ndani ya Yanga kwa kufunga mabao, kwani hadi sasa ana mabao 16, huku akizifunga karibu klabu zote Ligi Kuu tangu atue nchini isipokuwa Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons kwenye michezo ya Ligi Kuu.

Hata hivyo Mayele ameifunga Simba katika mechi mbili mfululizo za Ngao ya Jamii, huku akiwa ni mmoja ya wachezaji wenye hat trick kwenye Ligi Kuu.

Stephane Aziz KI ambaye alianza akiwa chini mara aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu ndiye anayefuata kwa mabao Jangwani akiwa na tisa pamoja na hat trick, huku akiwa na asisti nne kuonyesha namna mshambuliaji huyo kutoka Burkina Faso ni balaa kwa mabeki wa timu pinzani.

Straika chipukizi, Clement Mzize anaingia kwenye utatu huu kutokana na kuaminiwa zaidi kwa sasa na kocha Nabi akiwa amefunga mabao matano na kuasisti moja, akimweka kando Mzambia Kennedy Musonda aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo. Mzize pia ndiye kinara wa mabao wa Yanga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) akiwa na sita akishika nafasi ya pili nyuma ya Andrew Simchimba wa Ihefu iliyotolewa katika michuano hiyo mwenye mabao saba akiongoza orodha.

3) MBOMBO, DUBE NA SOPU (AZAM)

Ukiacha Simba na Yanga zinazofukuzana kwenye vita ya kufumania nyavu, lakini safu ya Azam FC nayo sio ya mchezo mchezo, ingawa timu hiyo ilijiondoa mapema kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu huu baada ya kuteleza katika mechi za duru la pili la ligi hiyo.

Utatu wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu, inaundwa na Idris Mbombo straika kutoka DR Congo umefunga jumla ya mabao 19, huku Mkongomani huyo ambaye naye ana muda mrefu hajafunga kwani tangu alipofunga mara ya mwisho bao lake la saba mnamo Desemba 16 mwaka jana wakati Azam ikitoka sare ya mabao 2-2 na Kagera Sugar ikiwa ugenini, hajafunga tena hadi sasa.

Mbali na Mkongoman huyo, lakini safu ya Azam ina Prince Dube mwenye mabao sita kama aliyonayo mkali mwingine aliyekamilisha utatu wa timu hiyo, Abdul Suleiman 'Sopu', huku Mzimbabwe huyo akiwa pia na asisti tatu.

Hadi sasa Azam ndio timu ya tatu kwa kufunga mabao mengi (44) kwenye Ligi Kuu Bara nyuma ya Simba yenye 63 na Yanga iliyokwamisha wavuni 52, huku ikiwa na wakali wengine wa kutupia kama Ayoub Lyanga mwenye mabao manne na asisti saba, Idd Seleman 'Nado' mwenye mabao matano, mbali na Kipre Junior, Tepsie Evance aliyeanza na moto akifunga na kuasisti kabla ya kuzimika.

4) BRUNO, KAGERE, FIGUIREDO (SINGIDA BIG STARS)

Licha ya kushiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa kwanza, lakini Singida Big Stars ni moja ya timu tishio kwa kufumania nyavu ikishika nafasi ya tano, ikiongozwa na kiungo mshambuliaji wa Kibrazili, Bruno Gomes mwenye mabao tisa kati ya 32 iliyonayo timu hiyo ya mkoani Singida.

Bruno amekuwa tishio kwa mabeki na makipa wa timu pinzani kwa umahiri wake wa kufunga mabao kwa mikwaju ya friikiki, akifuatiwa na straika mkongwe aliyewahi kuwika timu kadhaa za Afrika Mashariki na Kati ikiwamo Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na Simba ya Tanzania, Meddie Kagere mwenye mabao saba na kuufanya utatu huo kufunga jumla ya mabao 18.

Nyota mwingine anayefunga utatu huu wa Singida Big Stars ni Rodrigo Figuiredo pia kutoka Brazil ambaye ana mabao mawili kama aliyonayo Amissi Tambwe na nahodha Deus Kaseke, lakini akiwa ameasisti mara tatu akimfuata kwa mbali Mghana Nicholas Gyan mwenye asisti tano hadi sasa.

Utatu huo kwa kiasi kikubwa umeisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ikijiandaa kucheza na watetezi Yanga ili kuandika rekodi ya kucheza fainali, huku ikiwa tayari imejihakikishia tiketi ya mechi za kimataifa za CAF kwa msimu ujao sambamba na Simba, Yanga na Azam FC.

5) SABILO, TARIQ NA NG'ONDYA (MBEYA CITY)

Japo sio kati ya timu zilizopo kwenye Tano Bora kwa zenye mabao mengi kwa msimu huu, lakini utatu wao ni tishio ukiongozwa na nahodha, Sixtus Sabilo mwenye mabao tisa na kuasisti saba.

Utatu huu umefunga jumla ya mabao 17 kati ya 30 yaliyofungwa na timu hiyo katika Ligi Kuu Bara, ikiwa ni timu ya sita hadi sasa kutumia mabao mengi nyavuni nyuma ya Simba (63), Yanga (52), Azam (44), Geita Gold (33) na Singida Big Stars (32).

Hata hivyo, Mbeya City ni kati ya timu zinazopambana kwa sasa kujichomoa kwenye janga la kushuka daraja au kucheza play-off kutokana na kushika nafasi ya 13 ikikusanya pointi, lakini nahodha wake akichangia jumla ya mabao 15 kwa kufunga tisa na kuasisti sita, huku akifuatiwa na Tariq Seif mwenye matano na asisti tatu.

Nyota mwingine anayekamilisha utatu huo wa Mbeya City ni Richardson Ng'ondya ambaye licha ya kwamba hakucheza mechi za mwanzoni mwa msimu kutokana na kuwa majeruhi, lakini amekuwa na mchango kwa timu hiyo hadi sasa akiwa amefunga mabao matatu na asisti mbili.

SAFU NYINGINE

Mbali na Tano Bora hiyo ya utatu tishio ya kucheka nyavu kwa timu za Ligi Kuu msimu huu, lakini kuna timu nyingine nazo ni balaa kwenye kufunga mabao, ikiwamo Geita Gold yenye mabao 33, ikiwa ni timu ya nne msimu huu yenye mabao mengi ikifunga 33, ikiizidi hadi Singida Big Stars yenye 32.

Safu hiyo inaongozwa na kinara Elias Maguri aliyesajiliwa dirisha dogo anayeshirikiana na Edmund John na Juma Liuzio 'Ndanda', waliofunga jumla ya mabao 12, japo imezidiwa ujanja na utatu wa Tanzania Prisons na Namungo wenye mabao mengi zaidi yao.

Utatu tishio baada ya Tano Bora ni wa Tanzania Prisons unaoongozwa na kinara wa mabao wa timu hiyo, Jeremiah Juma mwenye mabao tisa akifuatiwa na Samson Mbangula mwenye mabao sita na Zabona Mayombya mwenye mawili kama Edwin Balua, ikiifanya safu hiyo iwe na jumla ya mabao 17.

Pia kuna utatu wa Namungo unaoongozwa na nahodha Reliants Lusajo ambao umezalisha jumla ya mabao 16 kati ya 26 ya timu hiyo. Lusajo amefunga manane huku, Shiza Kichuya na Ibrahim Ally 'Mkoko' kila mmoja akifunga manne.

Chanzo: Mwanaspoti