Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utamu upo hapa EPL

Arsenal Vs Man City Utamu upo hapa EPL

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Habari ndo hiyo. Arsenal sasa imejiweka kwenye kundi la timu siriazi zinazosaka ubingwa wa ligi.

Ushindi wa juzi Jumapili dhidi ya Manchester City umeonyesha mapinduzi makubwa ya kocha Mikel Arteta na chama lake katika kuhakikisha wanachukua pointi tatu kutoka kwa wapinzani wao muhimu kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, ambao msimu uliopita walibeba mataji matatu.

Baada ya miaka kibao ya Arsenal kushindwa kupata ushindi dhidi ya Man City kwenye Ligi Kuu England, safari hii mambo yamepinduka na miamba hiyo ya Emirates imeonyesha kuna kitu inahitaji.

Ligi Kuu England inaingia katika mapumziko kupisha michuano ya kimataifa, Tottenham ikiwa kileleni kwa tofauti ya mabao dhidi ya mahasimu wao Arsenal, baada ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Luton na kufanya kikosi hicho cha kocha Ange Postecoglou kuwa hakijapoteza mechi yoyote hadi sasa.

Man City ipo nyuma kwa pointi mbili dhidi ya vijana hao, lakini pointi moja zaidi ya Liverpool ya kocha Jurgen Klopp baada ya kubanwa na Brighton na kutoka sare ya mabao 2-2.

Wakati ligi hiyo ikiwa imeshuhudiwa raundi nane za mechi, tayari kuna mwangazo umejionyesha kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Kwa vigogo hao wanne, wanaonekana kuwa bize kwenye mbio za ubingwa, ni nani mwenye ratiba ngumu katika mechi sita zijazo?

TOTTENHAM

Mechi sita zijazo: Fulham (nyumbani), Crystal Palace (ugenini), Chelsea (nyumbani), Wolves (ugenini), Aston Villa (nyumbani), Manchester City (ugenini).

Mechi nane kwenye Ligi Kuu England baada ya ujio wa kocha Postecoglou na kila kitu kinaonekana tofauti kwenye kikosi cha Spurs. Imempoteza straika Harry Kane, lakini hilo halijawahi kuwa tatizo.

Mechi zao sita zijazo, watakuwa na shughuli pevu kwelikweli wakiwa na London derby tatu dhidi ya Fulham, Crystal Palace na Chelsea, huku ikiwa na msala pia wa Wolves, Aston Villa na Man City.

ARSENAL

Mechi sita zijazo: Chelsea (ugenini), Sheffield United (nyumbani), Newcastle (ugenini), Burnley (nyumbani), Brentford (ugenini), Wolves (nyumbani).

Kama imeweza kutunisha misuli na kupambana na mabingwa watetezi, Man City, ni wazi shaka yote ya kuhusu uwezo wa Arsenal kwenye Ligi Kuu England itakuwa imefutika. Mechi zao sita zijazo wataanza na Chelsea, huku mchezo wao mwingine mgumu kwenye ratiba yao ni ule wa kuwakabili Newcastle United. Timu nyingine zilizobaki, kwenye karatasi unaweza kuamini Arsenal hii itashinda.

MAN CITY

Mechi sita zijazo: Brighton (nyumbani), Man United (ugenini), Bournemouth (nyumbani), Chelsea (ugenini), Liverpool (nyumbani), Tottenham (nyumbani).

Hakuna ubishi, Pep Guardiola atashukuru kwa mapumziko haya ya mechi za kimataifa ili akatulize akili baada ya kikosi chake cha Man City kukumbana na vichapo viwili mfululizo kwenye ligi. Mechi zao sita zijazo wana shughuli pevu, ikiwa na kipute dhidi ya wagumu Brighton, Manchester United, Chelsea, Liverpool na Spurs. Bournemouth ndio pekee wanaonekana kuwa wepesi kwenye karatasi.

LIVERPOOL

Mechi sita zijazo: Everton (nyumbani), Nottingham Forest (nyumbani), Luton Town (ugenini), Brentford (nyumbani), Man City (ugenini), Fulham (nyumbani).

Licha ya kwamba wamevuna pointi moja tu kutoka kwenye mechi zao mbili za mwisho, chama la Jurgen Klopp, Liverpool lipo kwenye nafasi nzuri ya kuweka ushindani mkali kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Miamba hiyo ya Anfield, ratiba yao inaonekana kuwa na unafuu kwenye karatasi, ambapo ugumu unaweza kuwa watakapocheza na mahasimu wao Everton na mabingwa Man City.

Chanzo: Mwanaspoti