Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utalii wa michezo ndo huu hapa, tujipange sawasawa

UTALIII Utalii wa michezo ndo huu hapa, tujipange sawasawa

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ni mida ya saa 10 jioni hivi, timu ya taifa ya Gambia ‘The Scorpions’ au nge wanavyojiita, iko kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ikifanya mazoezi kujiandaa na mchezo wa kimataifa wa kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Burundi Alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa ambao unatumiwa na Burundi kama uwanja wa nyumbani.

Mara wanawasili Al-Hilal Omdurman ya Sudan ambao nao wanapaswa kufanya mazoezi hapo kwa ajili ya kujiweka sawa, huku wakitarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC ya Kinondoni jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Gambia watarudi Gymkhana baada ya mechi na Burundi kwani Jumatatu ijayo watakuwa wenyeji wa Ivory Coast kwenye Uwanja wa Mkapa ikiwa ni siku moja kabla ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kuwa wenyeji wa Morocco kesho yake kwenye uwanja huohuo katika mashindano hayo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la Marekani ya Kaskazini 2026.

Timu hizi zinalipa fedha kwa kila saa zinapofanya mazoezi kwenye viwanja vyetu ambavyo kwa kweli ni vichache kulinganisha na mahitaji. Watoaji wa huduma za usafiri kama mabasi makubwa yanayotumiwa na timu na magari madogo ya viongozi nao pia hujipatia kipato bila kusahau madereva. Kwa wastani timu ya mpira wa miguu inayokaa nchini kwa siku tatu hutumia katoni 50 za maji na hivyo kuchangia mapato ya wenye maduka na viwanda vya maji. Mahitaji ya mpira ni mengi zaidi ya hapo, hivyo ni fedha nyingi za kigeni zinazoingia kutokana na ziara hizi.

Piga picha akilini urudi nyuma miaka siyo mingi sana, timu ya Yanga iliyokuwa na fedha za Yusuf Manji ikienda Antalya, Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na msimu wa ligi. Timu ya Taifa ikaenda Uturuki, Morocco na kwingineko. Na hivi karibuni, imekuwa kawaida kwa timu zetu kuweka kambi ughaibuni kwa ajili ya kujiandaaa na mashindano mbalimbali.

Haya mambo yalitupa picha kuwa ni Uturuki au Morocco tu ndiko kuna mazingira mazuri ya kuweka kambi za michezo. Kabla ya hapo timu zetu za soka zilienda Brazil au Ulaya kwa safari za kuweka kambi nasi tukiamini kwamba ni huko tu tunakoweza kupata huduma ya namna hiyo.

Sasa mambo yamebadilika, watu wanapenda kuja kwetu isipokuwa maswali yanakuja kama kweli tuko tayari kuwapokea na kuendelea kuwapokea? Je, tuna mazingira mazuri na endelevu ya kimichezo? Je, tuna miundombinu thabiti na endelevu katika majiji na miji yetu? Je, sekta ya ukarimu ikoje? Je, rasilimali watu iko tayari?

Michezo ni sekta muhimu katika dunia ya sasa. Michezo hutoa ajira, huingiza kipato, huingiza kodi, hujenga afya ya jamii, hujenga uhusiano katika jamii, husaidia ukuaji kielimu kwa watoto na vijana na ni nyenzo muhimu sana katika diplomasia ya kimataifa.

Sekta ya michezo ni moja ya sekta za kiuchumi zinazokua kwa kasi sana duniani. Mathalani katika nchi ya Marekani (USA) michezo huingiza takribani dola 15 bilioni kwa mwaka kama pato la moja kwa moja kwa watu takribani laki 5 walioajiriwa katika sekta hiyo.

Michezo inachangia karibu asilimia 2 katika pato ghafi la taifa (GDP) huku ikitajwa kama moja ya sekta zinazokua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa sana. Rais Samia Hassan Suluhu alichukua uongozi wa nchi wakati dunia ikiwa kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19.

Uchumi wa dunia ulikuwa katika hali mbaya na sekta ya michezo kimataifa na hapa nyumbani ilikuwa katika wakati mgumu. Mwaka mmoja baadaye tunaona sekta binafsi ikijiingiza kwa nguvu katika uwekezaji. Unaweza kuona mathalani katika soka namna kampuni binafsi kama GSM, METL, Azam Pay TV na nyinginezo nyingi zikishirikiana na zile za umma kama CRDB, NBC, NMB n.k zinavyowekeza kwa nguvu katika mchezo huo.

Hii ni kutokana na serikali kuviacha vyama vya michezo, klabu na kampuni kufanya shughuli zao kwa uhuru. Sote tu-mashahidi namna nyuma kidogo wafanyabiashara waliojihusisha na udhamini wa michezo walivyopata msukosuko kidogo kiasi cha kupunguza udhamini au kujitoa kabisa. Chini ya Rais Samia nchi inaonekana kusogea zaidi kutoka kwenye michezo kutegemea zaidi ufadhili kuelekea kwenye kuwa na udhamini na miradi ya kibiashara.

Fursa nyingine zinazoonekana chini ya Rais Samia ni kuondolewa kodi kwa vifaa vya miundombinu ya michezo kama nyasi bandia, mpango wa serikali kukarabati na kujenga viwanja na pia kutengeneza kumbi kubwa za sanaa za maonyesho na filamu.

Angalia mfululizo wa matukio yaliyopita hasa yale ya African Football League, haya ya juma hili na ya juma lijalo katika upande wa mpira wa miguu tu. Ni matukio mengi na makubwa ingawa kiukweli baadhi hayajatangazwa vya kutosha. Mathalani timu za kigeni zinapotumia viwanja vyetu kama viwanja vyao vya nyumbani, bado hatushirikishi vyombo vya habari vya kutosha kuhakikisha umma unakwenda kushuhudia.

Watanzania wanapenda michezo wakati mwingine bila kujali nani wanacheza ili mradi wahamasishwe. Hivi majuzi Shirikisho la Soka Africa (CAF), liliizawadia timu ya Simba tuzo ya mashabiki bora wa mashindano ya AFL ikiwa ni ushahidi wa kufika kwao na kushiriki matukio ya uwanjani, hiyo ni fursa, itumike.

Pamoja na kuhitaji miundombinu ya michezo, utalii wa michezo pia unahitaji miundombinu wezeshi kama usafiri, hoteli na pia kuunganishwa na vivutio vingine kama sehemu za manunuzi, starehe n.k. Wadau wote wa sekta hii wanatakiwa kujipanga sawasawa ili kuhakikisha si tu wageni wanakuja bali kuwafanya wajisikie nyumbani na wakienda watangaze uzuri wa huduma wanazopata kwetu.

Jambo baya huenea haraka, leo mgeni anaweza kuja akapata kila kitu lakini huduma mbaya kwenye hoteli au usafiri au kukosekana huduma ya afya kukamsahaulisha mazuri mengi aliyoyaona.

Mazingira ya utalii wa michezo kusema ukweli yanaimarika. Serikali imeonyesha nia thabiti ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo. Wageni wanakuja wakivutiwa na miundombinu ya michezo na zaidi uwepo wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mwandishi wa Makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Unaweza kumtumia maoni yako kupitia namba yake ya simu iliyoko hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti