Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ustaraabu uzingatiwe sasa Benjamin Mkapa

Ndymbaro Mkapa Stadium Ustaraabu uzingatiwe sasa Benjamin Mkapa

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Oktoba 20 mwaka huu watu wa boli tunarudi kwenye uwanja wetu pendwa wa Benjamin Mkapa pale Temeke kata ya Chang’ombe.

Siku hiyo kuna matukio mawili makubwa, la kwanza likiwa ni uzinduzi wa mashindano ya African Football League na la pili ni kuanza kutumika tena kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kutotumika tangu miezi mitano iliyopita.

Jambo la kwanza linawahusu Simba zaidi maana siku hiyo watacheza mechi ya ufunguzi wa African Football League dhidi ya Al Ahly, mechi ambayo italeta kundi kubwa la wageni kutoka ndani na nje ya Afrika.

Tukio la pili ni la Watanzania wote hasa wapenzi wa soka ambao Uwanja wa Benjamin Mkapa umekuwa kama eneo letu la kujidai na kwenda kupata burudani ya soka pindi timu zetu zinapocheza hasa Taifa Stars, Simba na Yanga.

Kwa vile uwanja huo unatuhusu sote, ni vyema kuanzia sasa tukaanza kuulinda kwa kujitahidi kuwa wastaarabu ili kulinda miundombinu ya uwanja na mali nyingine zilizopo hapo ili uweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Kumekuwa na tabia isiyofurahisha ya watu kwa makusudi kabisa kufanya uharibifu wa vitu mbalimbali vilivyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jambo linaloleta hasara kubwa kwa serikali ambayo inaumiliki lakini pia kusababisha kutotumika baadhi ya nyakati ili ufanyiwe marekebisho.

Tunaweza kuona tunawakomoa watu fulani kwa kufanya ujinga na upumbavu huo wa uharibifu lakini mwisho wa yote athari zake zitakuwa kwetu wenyewe na sisi ndio tutakaoumia hapo baadaye.

Unapofungiwa maana yake timu zetu haziwezi kuutumia na sisi hatutaweza kuangalia mechi hapo lakini pia gharama za marekebisho zitatumia kodi zetu ambazo zinaweza kufanyia mambo mengine ya maendeleo.

Tuwe wastaarabu, tuutunze Benjamin Mkapa na viwanja vingine. Isifike wakati mechi za nyumbani tukalazimika kwenda kuzichezea nje ya nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live