Mwili wa marehemu Emmanuel Ngowo uliosafirishwa kimakosa na familia nyingine na kupelekwa Songea mkoani Ruvuma, umekabidhiwa kwa familia yake na taratibu za mazishi zinaendelea.
Hata hivyo, usiri umetawala katika hatua zote za familia hizo mbili kuchukua miili yao katika chumba cha kuhifadhia maiti ‘mochwari’ baada ya mwili huo kurejeshwa leo asubuhi kwa ndege ukitokea Songea ulikopelekwa jana.
Jana, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilichanganya miili ya marehemu katika chumba cha kuhifadhia maiti hali iliyosababisha mwili wa Ngowo kusafirishwa kimakosa mpaka Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 20, 2023 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Hospitali ya Muhimbili, Aminiel Aligaesha amesema kila familia imepata mwili wake husika kwa ajili ya kufanya mazishi.
“Songea wameshausafirisha mwili wao wameenda kuzika leo. Familia ya Emanuel Ngowo ambao wanatakiwa kuzika Kilimanjaro wameshaupokea mwili wao na wameshaondoka kwenda kuzika,” amesema Aligaesha.
Alipoulizwa kilichosababisha miili hiyo kuchanganywa, Aligaesha amesema, “Hiyo ndiyo taarifa iliyopo masuala mengine ndugu wamehitaji iishie hapo, kama kuna jingine litapatikana kutoka kwenye hizi familia mbili.”
Hata hivyo, familia ya Ngowo ilipotafutwa kutaka kuzungumzia suala hilo haikuwa tayari kuweka wazi nini kilitokea mpaka mwili wa mpendwa wao kusafirishwa Songea.
Msemaji wa familia hiyo Samwel Ngowo ambaye ni pacha wa Emmanuel (Marehemu) alionyesha utayari wa kuzungumza na Mwananchi, lakini kila alipopigiwa simu hakuweza kupata nafasi ya kuzungumza wala kuonana na mwandishi ndani ya Hospitali ya Muhimbili mpaka mwili ulipoondoka kwa safari ya kuelekea Moshi kwa mazishi.
Hata hivyo, Mwananchi ilipotaka kujua undani kuhusu familia nyingine ambayo ilibeba mwili kimakosa mpaka Songea, haikuweza kufanikiwa kutokana na usiri kugubika sakata hilo.
Jana Alhamisi, alipoulizwa kutaka ufafanuzi wa sakata hilo, Aligaesha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli tukio limetokea hapa hospitalini kwetu, tumeliona na tumeanza kuchukua hatua kadhaa, undani wa tukio hili tutazungumza na wanahabari kesho,” alieleza.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo Mwananchi ilimeipata kutoka ndani ya familia ya Ngowo jana iliesema kuwa familia nyingine yenye mlengo wa dini ya Kiislamu ndiyo iliubeba mwili huo kimakosa kuelekea Songea, wakati ulitakiwa kusafirishwa kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ibada ya mazishi kwa ajili ya Ngowo iliyotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 20 itashindikana, kwani familia hiyo bado inasubiri mwili wao kurudishwa kwa usafiri wa ndege kesho saa tano asubuhi ndipo waanze safari ya kuelekea Moshi kwa mazishi.
Familia ya Ngowo imeeleza kuwa miili hiyo ilichanganywa wakati wa kuihifadhi na kwamba walishindwa kuupata mwili wao na ndipo baadaye walifanya mawasiliano na kubaini mwili wao umesafirishwa kimakosa.
Tukio hilo ni miongoni mwa matukio kadhaa ya kubadilisha miili ya marehemu yaliyotokea hivi karibuni likiwamo la mkoani Mbeya ambako mwili wa mwanajeshi mstaafu, Watson Mwambungu ulikwenda kuzikwa Wilaya ya Busekelo baada ya kuchukuliwa na watu wengine Juni 15.
Mei 26 mwaka huu ndugu wa familia ya marehemu Gudluck Munuo (53) mkazi wa Kijiji cha Mese, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro walichukua maiti ya Eliudi Mbaga (68) mkazi wa Kijiji cha Matadi iliyokuwa imehifadhiwa Hospitali ya Kibong’oto na kwenda kuizika kabla ya kufukuliwa Mei 29.
Katika tukio jingine, Juni 30 mwaka huu ndugu wa Marehemu Steven Massawe (60) walishikwa na butwaa baada ya kufika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na kuukosa mwili wa ndugu yao.
Baada ya kufuatiliwa waligundua kuwa mwili wao ulishachukuliwa tangu Juni 26 na kuzikwa siku hiyohiyo Chalinze mkoani Pwani kwa imani ya Kiislamu.
Tukio jingine lilitokea Mei 19 baada ya ndugu wa marehemu Melkior Ndambale kwenda mahakamani kuomba kibali cha kufukua mwili wa ndugu yao uliokuwa umezikwa kimakosa wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Matukio haya yamekuwa yakitokea kwa kipindi kirefu kama ilivyotokea Kijiji cha Nkwansira Wilaya ya Hai, Kilimanjaro Mei 9, 2021 ambapo ndugu wa marehemu Danielson Lema (72) walipewa maiti ya mtu mwingine, Shanshandumi Kimaro (82) na kwenda kuzika bila kubaini kuwa siyo ndugu yao.
Aprili 13, mwaka 2016, Muhimbili kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walilazimika kufukua maiti hiyo ya Janeth Bambalawe (65), kuirejesha Dar es Salaam ili ikabidhiwe kwa wahusika baada ya kusafirisha maiti ya Amina Msangi (79), ambayo iliachwa kwa makosa katika chumba cha kuhifadhia maiti hadi Usangi.
Februari 12, mwaka 2022 Hospitali ya Rufaa Morogoro ilichanganya miili ya marehemu Mzee Gervas Chondoma na kuipa familia yake mwili mwingine ambao wakauzika Februari 10.
Februari 11 ikaibuka familia ya mtu mwingine ikidai walizika ndugu yao hali iliyosababisha kufukua mwili huo baada ya kubaini walizika mtu mwingine.