Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usipojipanga, utapangwa iko hivyo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa

Skysports Liverpool Arsenal 6110338 Usipojipanga, utapangwa iko hivyo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mechi 62 zimepigwa. Mmoja kashinda 25, mwingine 17. Sare ni 20.

Aliyeshinda 25, mara 16 alifanya hivyo nyumbani na 9 ugenini. Aliyeshinda 17, mara 11 nyumbani na sita ugenini.

Na safari hii, aliyeshinda mara nyingi atakuwa nyumbani. Na mgeni huyu ameshinda mara sita tu kwenye uwanja huo. Itakuwaje?

Hao ni Liverpool na Arsenal. Watamalizana usiku wa leo Jumamosi.

Patachimbika. Arsenal itasafiri kwenda Anfield kwenye mechi kali ya kuwania kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England.

Miamba hiyo miwili inayofukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England, itakuwa kwenye vita ya kushika usukani wa ligi hiyo, ambapo Arsenal inaongoza kwa tofauti ya pointi moja. Sare itawabakiza Arsenal na kula Krismasi wakiwa kileleni. Lakini, Liverpool nayo inataka nafasi hiyo. Hapo ndipo panapoleta utamu.

Kocha Mikel Arteta atasherehekea miaka yake minne tangu alipoteuliwa kuinoa Arsenal. Lakini, mbele yake amesimama Jurgen Klopp, atatoboa au sherehe itaharibika. Kama Arteta na chama lake la Arsenal wataibuka na ushindi uwanjani Anfield, basi hapo wataingia moja kwa moja kwenye orodha ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Lakini, takwimu zinawakataa Arsenal kwenye Uwanja wa Anfield. The Gunners haijashinda mechi yoyote ya ligi uwanjani hapo tangu mwaka 2012, wakati Lukasz Podolski na Santi Cazorla walipofunga na kuiwezesha Arsenal kushinda 2-0.

Arsenal inaingia uwanjani katika mchezo huo ikitokea kuwachapa Brighton 2-0 uwanjani Emirates, wakati Liverpool, wao wanaingia uwanjani baada ya kuangusha pointi wiki iliyopita mbele ya Manchester United baada ya sare ya bila kufungana, Anfield.

Kocha, Klopp amewataka mashabiki waje kuishangilia timu kwenye mchezo wao dhidi ya Arsenal. Kocha huyo Mjerumani anaona mashabiki walidorora kwenye mechi dhidi ya Man United na West Ham United.

Klopp alisema kama shabiki mwenye tiketi haendi uwanjani, basi ampe anayetaka kuja. Mambo ni moto kwelikweli.

Viwango vyao vikoje?

Liverpool inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa haijapoteza katika michezo mitano iliyopita ya Ligi Kuu na usiku wa Jumatano ilionyesha makali zaidi, ilipofunga mabao 5-1 dhidi ya West Ham kwenye robo fainali ya Kombe la Ligi. Klopp anaamini kikosi chake kitaendelea kukipiga kwenye ubora mkubwa na kuendeleza rekodi yao tamu dhidi ya Arsenal uwanjani Anfield.

Arsenal yenyewe imeshinda mechi nne kati ya tano zilizopita. Imepoteza moja. Kichapo hicho kimoja katika mechi tano zilizopita Asrsenal ilikipata kutoka kwa Aston Villa uwanjani Villa Park. Arsenal ilishinda Anfield mwaka 2020, ilipowatupa nje Liverpool kwa mikwaju ya penalti kwenye Kombe la Ligi.

Mzuka wa timu zenyewe

Liverpool ina orodha ndefu ya wachezaji watakaokosa mechi hiyo ya Arsenal. Staa wao mpya, Alexis Mac Allister atakosa na huenda akawa nje ya uwanja hadi mwakani. Andy Robertson, Stefan Bajcetic na Thiago Alcantara ni mastaa wengine watakaokaa nje ya uwanja kwa muda mrefu. Diogo Jota anakaribia kurudi uwanjani, lakini mechi ya Arsenal itakuja haraka sana kwa upande wake.

Arsenal yenyewe inaweza kukosa huduma ya wachezaji sita kwenye mechi hiyo ya Anfield. Mohamed Elneny, Jurrien Timber, Takehiro Tomiyasu na Fabio Vieira wote hawatakuwapo, wakati Jorginho na Thomas Partey wapo kwenye hatihati kubwa kuwapo kwenye mechi hiyo.

Kipute kicho kinashuhudiwa upinzani mkali wa mastaa Martin Odegaard na Dominik Szoboszlai. Odegaard amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu, akifunga mabao manne na kuasisti mara mbili, lakini Szoboszlai bado anaendelea kuzoea mazingira, lakini usiku wa Jumatano alifunga bao matata kabisa dhidi ya West Ham kwenye mchezo wa Kombe la Ligi.

Mechi nyingine

Mchakamchaka wa Ligi Kuu England utaendelea kwenye viwanja vingine, ambapo huko London, West Ham United itakuwa nyumbani kuwakaribisha Man United wanaojitafuta. Rekodi zinaonyesha kwamba miamba hiyo imekutana mara 54 kwenye mechi za Ligi Kuu England, ambapo West Ham imeshinda nane tu, sita nyumbani na mbili ugenini, huku Man United ikishinda 33, mechi 22 nyumbani na 11 ugenini. Mechi 13 baina yao zilimalizika kwa sare.

Fulham itakipiga na Burnley, huku Luton Town itakuwa nyumbani kukipiga na Newcastle United. Mambo ni moto. Nottingham Forest wao watamaliza ubishi na Bournemouth.

Tottenham Hotspur itakuwa nyumbani kucheza na Everton katika moja ya mechi za kibabe kabisa..

Chanzo: Mwanaspoti