Klabu ya Yanga imesema hatima ya aliyekuwa kocha wake msaidizi Cedric Kaze, itafahamika mara baada ya kupatikana kwa kocha mkuu, huku pia ikiweka wazi kila kitu kuhusu Yannick na Tuisila Kisinda ndani ya kikosi hicho.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kumpata Kocha Mkuu na atakapokabidhiwa majukumu ndiye atakayeamua kuendelea kufanya kazi na benchi lililopo akiwamo Kaze, au kuja na watu wake.
Kutokana na hali hiyo, hatima ya kocha huyo raia wa Burundi kubaki Yanga au kuondoka, itategemea maamuzi ya kocha atakayekuja.
"Sasa hivi mazungumzo yaliyopo ni kumpata kocha mkuu, tukishampaka ndiyo tunampa fursa mwalimu anayekuja kuchagua wasaidizi wake, akitoa ruhusa tutaendelea na mazungumzo, yeye ndiye atakayetuambia watu gani anaotaka kufanya nao kazi kwenye benchi lake la ufundi.
"Akisema anawahitaji sawa, lakini anaweza kusema anakuja na benchi lake la ufundi, ndiyo dunia ya mpira wa sasa ilipofikia na sisi Yanga ni weledi," alisema Kamwe.
Akizungumzia juu ya taarifa za mchezaji wao Bangala kutaka kuondoka, alisema kwa sasa ni mchezaji wa Yanga aliyebakisha mwaka mmoja, lakini kama akipata ofa nono, yenye maslahi kwa pande zote mbili klabu haiwezi kumzuia.
"Mpaka sasa ana mkataba wa mwaka mmoja, na mwaka wake uliobakia tunapitia ripoti ya benchi la ufundi, tunasubiri kumpata mwalimu mpya, lakini tunaongea na mchezaji mwenyewe, halafu hatima yake itatolewa.
"Apata ofa, klabu ikasikiliza kama inakuwa na maslahi ya pande zote basi itamruhusu, lakini mpaka tunavyozungumza Bangala bado ni mchezaji halali wa Yanga," alisema.
Kuhusu kuachana na Tuisila Kisinda, Kamwe alisema amemaliza mkataba wake wa mwaka mmoja kutoka klabu ya RS Berkane na sasa anarejea huko.