Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushirikina watawala Kigoma 

6d1e72bcc823e70c6862bc696bb84a56.jpeg Ushirikina watawala Kigoma 

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUELEKEA pambano la fainali za michuano ya kombe la Shirikisho la Azam itakayofanyika kwenye uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, ulinzi mkali umewekwa uwanjani hapo kuzuia watu wanaokuja kufanya mambo ya kishirikina.

Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini inatarajiwa kuchezwa Julai ikizishirikisha Simba na Yanga.

Katibu wa Chama cha soka mkoa Kigoma (KRFA) Omari Gindi alisema jana kuwa kumekuwa na kupishana kwa watu wanaofika uwanjani hapo wakichukua mchanga wa sehemu mbalimbali za uwanjani ikiwemo ndani ya eneo la kuchezea na kuchukua nyasi.

Akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo Gindi alisema kuwa kutokana na hali hiyo kwa sasa wamezuia watu wasiohitajika kuingia uwanjani hapo.

"Naamini mazoezi ya walimu na hali ya wachezaji ndiyo yanayoweza kuleta matokeo kwa sisi kama chama cha soka hatuamini kwenye mambo ya ushirikina na hivyo tumezuia wote ambao wanataka kuingia uwanjani kwa ajili ya jambo hilo,"alisema Gindi.

Akizungumzia maandalizi na marekebisho yanayofanyika uwanjani hapo, Gindi alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kwa sasa wanamalizia ukarabati wa vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kuweka sawa eneo la kuchezea ambalo limekidhi vigezo kwa taratibu za TFF.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mashindano wa shirikisho la soka nchini (TFF),Salum Madadi alisema, maandalizi ya mechi hiyo ya fainali yanaendelea vizuri na kwa saa uthibitisho ni kwamba mechi hiyo itachezwa uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Madadi alisema kuwa ukaguzi umefanyika na marekebisho madogo yanafanywa lakini amebainisha kuwa kazi kubwa imefanywa na serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wamiliki wa uwanja CCM mkoa Kigoma na chama cha mpira mkoa Kigoma kuhakikisha taratibu zote zinakamilika.

"Kwa sasa hatuwezi kutoa tamko lolote lakini kwa kifupi imekubalika fainali itafanyika uwanja wa Lake Tanganyika na Ijumaa (keshokutwa) kutakuwa na kikao baina ya serikali ya mkoa chini ya mkuu wa mkoa,TFF na wamiliki wa uwanja na taratibu mbalimbali za mchezo huo zitatangazwa,"alisema Madadi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz