Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushindi wa Yanga waipa mzuka Ihefu SC

Ihefu Yanga Ns Ushindi wa Yanga waipa mzuka Ihefu SC

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo ikiwa nyumbani dhidi ya Yanga, imeifanya Ihefu SC kupata mzuka na kuamini hata KMC watakaovaana nao kesho Jumamosi jijini Dar es Salaam watakaa tu mbele yao katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Ihefu ilishinda 2-1 ikiwa nyumbani dhidi ya watetezi Yanga ikiwa ni msimu wa pili mfululizo kufanya hivyo ikicheza Uwanja wa Highland Estate, jijini Mbeya ikiendeleza ubabe wa kuwatibulia wababe hao wa soka nchini, kwani msimu uliopita iliitibulia rekodi ya kucheza mechi mfululizo ikiikwamisha katika mechi ya 49 na safari hii ikiwa mechi ya nne tu, imeituibulia baada ya kushinda awali mara tatu.

Hadi sasa timu hiyo ya mkoani hapa ipo nafasi ya saba kwa pointi sita, huku KMC wakiwa nafasi ya tano kwa alama saba na kufanya mechi ya leo kuwa na upinzani mkali.

Timu hizo zinakutana mara ya nne katika rekodi, ambapo kila upande umeshinda mechi mbili ambapo kila mmoja akipata pointi tatu nyumbani hivyo leo ni historia kwao.

Kocha Mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema baada ya mchezo uliopita kushinda, morali imeonekana kuwa juu kwa wachezaji akisema licha ya mabadiliko ya mbinu, lakini lazima wapite mulemule kuimaliza KMC.

Alisema wanafahamu mechi hiyo kuwa na ugumu, lakini kwa maandalizi waliyofanya watahakikisha wanaendelea kufanya vizuri ili kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

“Kila mchezo na mbinu zake, lakini inapokusadia sehemu si mbaya kuziendeleza matarajio yetu ni kushinda ili kupanda juu, tunajua ugumu utakuwapo kwa sababu kila mmoja anataka pointi tatu,” alisema Katwila.

Straika wa timu hiyo aliyeizingua Yanga juzi kwa kufunga bao la ushindi, Charles Ilanfya alisema kutokana na malengo yao wanahitaji ushindi kila mechi akieleza kuwa anahitaji kuendeleza kasi yake ya ufungaji mabao.

“Kama straika kazi yake ni kufunga mabao, hivyo ninapopata nafasi lazima niitumie ili kuipa matokeo timu yangu lakini kuendeleza ubora kwenye mabao,” alisema Ilanfya.

Hata hivyo, Ihefu inapaswa kuingia Uwanja wa Uhuru utakaotumika kwa mchezo huo kwa tahadhari kwani, KMC imetoka kushinda mechi mbili mfululizo ikizipasua JKT Tanzania na Geita Gold kila moja mabao 2-1, lakini mechi nne baina yao hakuna mbabe kwani kila moja ilishinda mechi mbili na kupoteza mbili.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live