Kitendo cha Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima kuitaja klabu ya Yanga wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, wabunge wametumia sekunde kadhaa kushangilia.
Jana klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAFCC) baada ya kuindoa Marumo Gallants kwa jumla ya mabao 4-1.
Katika mchezo wa fainali, Yanga itakipiga na USM Alger ambayo nayo iliiondoa Asec Mimosas kwa jumla ya mabao 2-0.
Dk Gwajima aliitaja Yanga wakati akiwasilisha bajeti hiyo wakati akitaja wadau waliuongana na Wizara hiyo kutoa uelewa dhidi ya vitendo vya ukatili katika jamii.
Azam FC ni klabu nyingine ya Ligi Kuu Bara ambayo inaunga mkono juhudi hizo huku akiitaka Simba nayo kufuata mfano huo.
Mara baada ya kuitaja Yanga, Waziri alilazimika kusubiri wabunge wamalize kupiga makofi, kama ishara ya kuunga mkono mafanikio ya klabu hiyo.
“Mheshimiwa Spika, naungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuipongeza klabu ya mpira wa miguu Yanga kwa ushindi ilioupata jana (Jumatano). Mungu amewabariki kwa maana wamebeba ajenda ya kuwatetea wanawake na watoto,” Waziri amesema.