Hebu tuanze hapa. Umeshawahi kuona filamu ya Escape to Victory? Ni filamu moja iliyoigizwa na mastaa wakubwa na kupata umaarufu mkubwa katika miaka ya 80’.
Kinachofanya niikumbuke filamu hiyo ni wahusika wake ambao baadhi yao walikuwa ni wachezaji wa soka zaidi ya 14 ambao walikuwa wafungwa waliocheza mechi dhidi ya timu ya Ujerumani.
Baadhi ya wahusika walikuwa ni pamoja na mwanasoka maarufu, aliyekuwa akiichezea Santos, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’, Bobby Moore ambaye alikuwa mchezaji wa West Ham ya England.
Baadhi ya nyota wengine ni wa Manchester City, Mike Summerbee, Kiungo wa Kiargentina, Osvaldo Ardiles na straika wa Kidenmark, Soren Lindsted, beki wa kati wa Ipswich Town, Kevin Beattle. wengine ni beki wa New York Cosmos ya Marekani, Werner Roth na beki wa kati wa Ipswich Town, Russell Osman.
Ndani ya filamu hiyo mbali na kuwashirikisha mastaa wa soka, pia alikuwapo na nyota mwingine wa filamu za mapigano, Sylvester Stallone ‘Rambo’.
Rambo alikuwa golikipa wa timu hiyo ya wafungwa dhidi ya Ujerumani.
KUHUSU ABDALLAH LUO
Hebu turudi kwa Luo. jina lake kamili ni Abdallah Omary alikuwa mchezaji wa soka hapa Tanzania na aliwahi kuitumikia timu ya African Sports ya Tanga katika miaka ya 70.
Inadaiwa alipewa jina la Luo kutokana na mwonekano wake, ambao watu walimfananisha na kabila moja wapo kutoka Kenya.
ALIKUWA KAMA TEKELO
Unamkumbuka Abeid Mziba ‘Tekelo’? Basi Luo alikuwa kama nyota huyo wa zamani wa Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Hakuwa mzuri kwenye kuitumia miguu yake, bali alikuwa fundi sana katika kukitumia kichwa chake kwa kupachika mabao.
ALIFUNGWA JELA
Luo alikuwa mmoja kati ya wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania waliopiga picha na Rais Nyerere (angalia picha). Akiwa mfanyakazi wa Manispaa ya Tanga, yeye na baadhi ya wafanyakazi wenzake waliingia matatani baada ya kutokea kwa ubadhirifu wa pesa katika ofisi yao.
Kesi ilipoenda mahakamani Luo na wenzake hao walihumikiwa kifungo gerezani. Wengi waliamini huo ndio ungekuwa mwisho wake wa kucheza soka.
Wakati akiwa gerezani huku nyuma Timu ya Taifa ya Mkoa wa Tanga ilikuwa ikicheza Mashindano ya Taifa Cup ambayo yalikuwa yakishindaniwa na timu za mikoa.
Timu hiyo ya Mkoa ‘Tanga Stars’ ilikuwa inacheza fainali ya Taifa Cup dhidi ya Timu ya Mkoa wa Kilimanjaro.
ATOLEWA JELA
Baadhi ya wadau wa soka wa Mkoa wa Tanga walitaka kuona mkoa wao unabeba taji hilo, hapo ndipo ilipoanza mipango ya kumtoa Luo gerezani.
Wakati huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga alikuwa Kingunge Ngombale Mwilu aliyepokea nafasi hiyo kutoka kwa Alhaj Rajabu Kundya. Wadau wakamfuata Mzee Kingunge na kumsomesha ili Tanga Stars iweze kubeba taji hilo, basi Luo atolewe gerezani na ashiriki mchezo huo.
AFUNGA BAO KWA KICHWA
Luo hakuwaangusha waliofanya mipango ya kumtoa gerezani, kwani alifanikiwa kufunga bao lililoipa Tanga Stars ushindi katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali.
Baada ya hapo Luo alikuwa huru na kuendelea na maisha yake mengine na alibeba sifa nyingi sana za mkoa.
HATMA YA MAISHA YAKE
Mbali na kucheza soka na kufanya kazi Manispaa ya Tanga, Luo alijiingiza katika kazi ya ubaharia na kufanikiwa kupata kazi katika meli moja ya Kigiriki.
Inadaiwa Luo akiwa katika meli hiyo kama mfanyakazi hahali, ilitokea ndani ya meli hiyo alipatikana kijana wa Kiafrika aliyekuwa amezamia ndani yake.
Wagiriki waliomuona kijana huyo wakaamua kumtosa baharini lakini Luo aligeuka na kumtetea kijana huyo asitoswe bali ufanyike utaratibu mwingine wa kuweza kumwacha hai.
Inadaiwa mzozo mkubwa uliibuka kati ya Wagiriki na Luo na hatimaye, wamiliki mabahari wa Kigiriki wa meli hiyo waliamua kuwatosa wote wawili Luo na yule kijana aliyezamia.
Na huo ndio ukawa mwisho wa maisha wa Abdallah Luo.