Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usajili wa Mamelodi yatikisa Simba, Yanga

Onana X Pacome X Usajili wa Mamelodi yatikisa Simba, Yanga

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ukisikia jeuri ya fedha ndio hii. Wababe wa soka wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns imeshusha staa mpya kutoka Latini Amerika, ikiwa ni mikakati yao ya kujiiamrisha kwenye michuano ya ndani na ile ya CAF.

Mabingwa hao wa michuano mpya ya African Football League (AFL) na mabingwa wa Afrika Kusini kwa misimu saba mfululizo, wamemsajili nyota huyo, Matrias Esquivel kwa kiasi cha Randi 46 milioni za Afrika Kusini ambazo ni zaidi ya Sh6.2 bilioni za kitanzania.

Sasa kama hujui ni kwamba fedha hizo ni zaidi ya kiwango cha fedha ambazo klabu ya Simba imekaridiria kutumia katika bajeti yao ya mishahara kwa wachezaji wote kwa msimu wa 2023-2024, ikiwamo mastaa matata kabisa kama Henock Inonga, Luis Miquissone, Clatous Chama pamoja na wafanyakazi wengine na chenji inabaki. Bajeti ya mishahara ya Simba kwa msimu husika ni Sh4.8 bilioni.

Kiwango hicho cha fedha alizolipwa Esquivel zinaweza pia kulipa mishahara ya mastaa wote wa Yanga ambao kwa mujibu wa bajeti ya klabu hiyo kwa mwaka 2023-2024 ilikadiriwa kuwa Sh5.4 bilioni, ikiwa na maana dau hilo la staa huyo mpya wa Mamelodi inawalipa kina Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na wenzao wote kwa mwaka mzima na chenji inabaki.

Ipo hivi. Mamelodi ni moja ya timu zilizopo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama ilivyo kwa Simba na Yanga, jana Alhamisi iliingia kwenye vichwa vya habari kufuatia kukamilisha usajili na kumtambulisha mchezaji huyo kutoka klabu ya Argentina ya Atletico Lanus.

“Jina langu ni Matías Esquivel; Ninajivunia kuwa wa manjano,” alisema staa huyo wa Argentina katika video fupi iliyowekwa kwenye akaunti rasmi ya X (Twitter) ya Mamelodi.

Mamelodi wameonyesha jeuri hiyo ya fedha ikiwa ni siku chache tu tangu kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Simba ambapo pamoja na mambo mengine yaliyofanyika kwa Wekundu wa Msimbazi yaliwekwa wazi mapato na matumizi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mhasibu wa Simba, Suleiman Kahumbu mkwanja ambao umekuwa ukitumika kwa ajili ya kulipa mishahara, wachezaji ikiwemo Clatous Chama, Luis Miquissone, Fondoh Che Malone, Fabrice Ngoma, Henock Inonga pamoja na wafanyakazi wengine ikiwemo benchi la ufundi linaloongozwa na Abdelhak Benchikha ni zaidi ya Sh.4.8 bilioni.

Kimahesabu ina maana usajili wa Esquivel kutua Mamelodi unalipa mishahara wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine kwa mwaka mzima na bado kuna chenji ibaki ambayo ni zaidi ya Sh1.2 bilioni unaweza kufanya matumizi mengine ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji watatu wa maana kwa makadirio ya kila mchezaji kumnasa kwa Sh400 milioni.

Pia kwa Yanga, katika Mkutano Mkuu uliofanyika Julai mwaka jana iliweka bayana kwamba klabu ilikusanya zaidi ya Sh17 bilioni na kutoa mchanganuo wake kwamba ni Udhamini Sh8.1 bilioni, mapato ya mlangoni Sh2 bilioni, ada za uanachama Sh939 milioni, Zawadi Sh1.1 bilioni, mauzo ya wachezaji Sh200 milioni, faida ya jezi Sh337 milioni, Mengine Sh150 milioni na mikopo Sh4.08 bilioni.

Baadhi ya matumizi ya fedha hizo zilizoanishwa ni pamoja na mishahara Sh5.4 bilioni, mbali na ada za wachezaji Sh2.4 bilioni, motisha Sh2.8 bilioni, kambi Sh460 milioni, Chakula na Malazi Sh1.1 bilioni, maandalizi ya mechi Sh1.4 bilioni, usafiri Sh1.6 bilioni, kodi za nyumba Sh290 milioni, Matibabu Sh102 milioni. Jumla matumizi Sh17.3 milioni na kubakiwa na Sh581 milioni.

Hiyo ikiwa na maana kwamba, katika ada ya usajili ya Esquivel ni kwamba inalipa mishahara ya nyota wa Yanga na kusaliwa na Sh800 milioni ambazo zinaweza kusajili wachezaji wengine wawili wa maana kwa dau ya Sh400 milioni kila mmoja.

Kiwango hicho cha fedha kama zikiamuliwa kutaka kuwapa ajira vijana waliopo mitaani kwa kuwanunulia bodaboda ili wapige mishe, ina maana zitawanunuliwa zaidi vijana 2,818 kwa bei ya Sh2.2 milioni.

Bodaboda hizo zikiwekezwa kwenye sekta ya usafirishaji kwa wiki zinaweza kukuingizia zaidi ya Sh210 milioni (kwa malipo ya Sh 20,000 kwa wiki kwa kila moja).

Kiwango hicho cha fedha zinaweza pia kununua zaidi ya IST 442 ambazo ukiingiza kwenye biashara ya usafiri wa kulipwa Sh30,000 kila siku ambapo kwa wiki itakuwa Sh210,000 kwa gari mtu atapokewa kwa wiki jumla ya Sh93 milioni.

STAA MWENYEWE

Kupitia ripoti za mitandao mbalimbali huko Afrika Kusini, Esquivel alitua nchini humo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo, jijini Johannesburg Jumapili iliyopita. Kuwasili kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 hakujaleta tu nguvu mpya kwenye eneo hilo bali ni mchezaji mwingine ghali zaidi kwenye kikosi hicho.

Ikumbukwe kuwa Julai mwaka juzi, Mamelodi maarufu kama Masandawana ilimsajili Marcelo Allende raia wa Chile kutoka Torque kwa Sh7.9 bilioni na ndiye mchezaji ghali zaidi kwenye kikosi hicho.

"Mamelodi Sundowns imethibitisha kumsajili Matías Esquivel kutoka klabu ya Argentina ya Atlético Lanus kwa mkataba wa miaka minne na nusu," ilisema taarifa ya klabu hiyo.

Katika usajili wa mchezaji huyo, Lanus imeweka kipengele cha kupata mgao wa asilimia 10 ikiwa Mamelodi itamuuza mchezaji huyo sehemu nyingine.

Staa huyo anajiunga na Mamelodi ikiwa ni usajili wa pili katika dirisha hili la katikati mwa msimu, kufuatia beki Zuko Mdunyelwa, aliyejiunga Desemba 2023.

WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amesema Mamelodi ni miongoni mwa klabu chache za Afrika ambazo zimejijenga mno kiuchumi hivyo inahitaji muda kwa klabu za daraja la kati kufanya hayo.

"Kiukweli ni kiwango kikubwa sana cha fedha inahitaji muda kwa klabu za daraja la kati kwenye mpira wa Afrika kufanya usajili wa namna hiyo, lakini inavutia kuona mpira wa Afrika unakua na hata uchumi wa klabu zake," alisema kocha huyo wa kimataifa wa Nigeria.

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Yanga, Hans Pluijm alisema; "Simba na Yanga bado zina safari ndefu ya kufika huko, lakini nimeona kadiri siku zinasogea zimekuwa zikikua kwa kasi sana kiuchumi maana wanamudu kusajili wachezaji kutoka sehemu mbalimbali hata nje ya Afrika."

Chanzo: Mwanaspoti