Mashabiki wa The Gunners ‘Arsenal’ wamewacheka wale wa Chelsea baada ya kufahamika Brighton wanataka zaidi ya Pauni 100 milioni kumuuzaMoises Caicedo.
Kiungo huyo wa Ecuador aliigharimu Seagulls Pauni 4 milioni mwaka 2021 kutoka Independiente Delvalle, lakini sasa inataka mara 25 ya pesa hizo ili kumuuza.
Brighton ilikataa ofa mbili za Arsenal kwa ajili ya Caicedo dirisha la Januari, huku ikielezwa moja ya ofa hizo ilikuwa Pauni 70 milioni.
Baada ya hapo, staa huyo alisaini mkataba wa mwaka mmoja zaidi kuendelea kubaki Amex hadi 2027, lakini hilo halikufanya timu zinazomtaka kuacha kumfukuzia. Caicedo yupo kwenye mipango ya Chelsea, waka- ti kocha mpya Mauricio Pochettino akiamini atamnasa.
Lakini, ripoti zinadai mabosi wa Brighton wanamlinganisha Caicedo na Declan Rice huku staa wao mwenye umri wa miaka 21 ni mdogo kwa miaka mitatu dhidi ya nahodha wa West Ham.
Arsenal wapo kwenye hatua za mwisho kumchukua Rice kwa Pauni 105 milioni na Brighton wanaamini hata Caicedo thamani yake ni kama hiyo.
Shida sasa inakuja, Chelsea Januari ilivunja rekodi ya uhamisho Ligi Kuu England iliponasa saini ya Enzo Fernandez kutoka Benfica kwa ada ya Pauni 107 milioni.
Na baada ya kuondoka kwa N’Golo Kante, Mateo Kovacic na Ruben Loftus-Cheek, Pochettino anamtazama Caicedo kama mtu sahihi kwenda kucheza na Enzo. Lakini, bei anayouzwa Caicedo ndiyo iliyowafanya mashabiki wa Arsenal wawacheke wenzao wa Chelsea kwenye kurasa zao za Twitter.
Shabiki wa kwanza alianza: “Chelsea wamechafukwa,” wakati mwingine aliongeza: “Oops mashabiki wa Chelsea. Hahahahahaha. Klabu nyingine ngumu badala ya West Ham ni Brighton. Hahahaha.”
Shabiki wa tatu aliandika: “Vitu vinavyopenda kuona,” huku shabiki mwingine wa Arsenal akisema: “Looh! Hii tumeshaifuta kwa Chelsea!”