Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usajili wa Azam ulifeli wapi?

Sopu Atua Azam Usajili wa Azam ulifeli wapi?

Thu, 29 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama kuna timu ilikuwa na mbwembwe wakati wa maandalizi ya msimu mpya wa 2022/23 basi ni Azam FC.

Matajiri hao wa Chamazi walianza kwa kishindo siku moja tu baada ya kukamilika kwa msimu wa 2021/22 ambao ulikuwa mgumu sana kwao kiasi cha kutokuwa na uhakika wa tiketi ya mashindano ya kimataifa hadi siku ya mwisho ya msimu wa ligi, Juni 29/2022.

Siku moja tu baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi, Azam FC wakaanza kuchafua hali ya hewa. Walianza kwa kumtangaza Kipre Junior kama usajili mpya wa 2022/23 huku Bosi wa timu, Yusuf Bakhresa, akionekana kwenye picha ya utambulisho wa wachezaji.

Hii ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo, mmoja wa wakurugenzi wake kuonekana hadharani akitambulisha mchezaji. Saa chache baadaye, Yusuf kupitia Instagram yake akachapisha kikosi bora cha msimu wa ligi kuu ya Ivory Coast kikimuonesha Kipre Junior.

Halafu akaweka maneno yafuatayo, Hiki ni kikosi bora cha ligi kuu ya Ivory Coast, chuma kimoja tayari kishatambulishwa. Kingine kioo hapo nakishusha baada ya saa. Mtawasearch wenyewe mtandaoni. Na kweli, baada ya saa Azam FC wakamtambulisha Tape Edigno.

Moto huo waliuwasha mfululizo na kumtambulisha jumla ya wachezaji 8 kama usajili mpya. Mtindo walioutumia kutangaza ukaweka juu sana matarajio ya watu kwamba msimu huu Azam FC wana kitu, hasa ukizingatia uwepo wa Bosi Yusuf mwenyewe.

Lakini baada ya msimu kukamilika, Azam FC imemaliza pale pale kwenye nafasi ya tatu, kama ilivyokuwa misimu mitatu nyuma yake. Je, usajili wa Azam FC ulifeli? Hii ni tathmini ya jumla ya usajili huo wa Azam FC, ukimuangalia mchezaji mmoja mmoja.

1. Ali Ahamada - 4/10

Aliwasili nchini Julai 13 na kwenda kupokewa uwanja wa ndege na Yusuf Bakhresa mwenyewe. Hii pia ikawa mara ya kwanza kwa wakurugenzi wa klabu hiyo kwenda kumpokea mchezaji uwanja wa ndege.

Akatambulishwa siku hiyo hiyo na kuleta matumaini makubwa kwamba sasa Azam FC wametibu tatizo lao la muda mrefu la mlinda lango. Lakini msimu ulipoanza, akaanza kutoa shaka katika mchezo wa kwanza kabisa, alipofungwa bao na Anuary Jabir wa Kagera Sugar, japo Azam FC walishinda mechi hiyo.

Mechi ya pili dhidi ya Geita Gold ikaongeza shaka ya waja, alipofungwa bao la mkwaju wa adhabu ndogo na Adeyum Ahmed. Alikuja kukera watu kwenye mchezo wa matokeo ya 2-2 dhidi ya Yanga alipofungwa bao la 'kawaida sana' na Feisal Salum.

Baada ya hapo waliokuwa na shaka naye wakahitimisha kwamba yaliyomo hayamo kwa kipa huyo. Na kwenye mchezo wa mzunguko wa pili dhidi ya hao hao Yanga, kipa huyo akafanya makosa mengine yaliyowafanya Azam FC wenyewe pia wapigie mstari kwamba hapo 'walipigwa.'

Haikushangaza kuona Azam FC wakisajili kipa mpya, Abdullahi Idrisu, kwenye dirisha dogo na kuanzia hapo Ahamada akabaki jina. Ali Ahamada amecheza mechi 16 za ligi na 2 za Kombe la Shirikisho la CAF, akitumia jumla ya dakika 1620; dakika 1440 kwenye ligi na 180 kwenye CAF.

Amefungwa mabao 17; mabao 14 kwenye ligi na 3 kwenye CAF. Ametoka na hati safi mara 7, hati safi 6 kwenye ligi na moja CAF.

2. Nathan Chilambo - 4/10

Zao la timu ya vijana ya Ruvu Shooting, Chilambo alianza vyema sana Azam FC, hadi kuitwa timu ya taifa. Mechi za kwanza zote zilikuwa zake, hadi mabadiliko ya benchi la ufundi yalipomuathiri.

Kuondoka kwa kocha Abdihamid Moallin kukaingiliana na wito wa timu ya taifa. Wakati akiwa huko, Azam FC ikawa inajiandaa na mchezo dhidi ya Yanga. Timu ilikuwa chini ya Mohamed Badru ambaye alimuandaa Lusajo Mwaikenda kwa sababu ndiye beki aliyebaki kambini katika nafasi yao.

Lusajo akafanya vizuri sana na kuonekana anaweza kuhatarisha nafasi ya Chilambo.

Lakini Lavagne kwa kuheshimu jina la 'Timu ya Taifa', akaamua kuendelea naye kama chaguo lake katika eneo hilo.

Lakini baada ya kiwango cha chini kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Akhdar kule Libya, Lavagne akamuweka nje 'dogo' huyo wa miaka 19 na kumpa nafasi Lusajo Mwaikenda.

Baada ya hapo, Chilambo akawa chaguo la pili hadi mwisho wa msimu. Lakini alipopata nafasi moja moja, kama kwenye mchezo wa sare ya 1-1 dhidi ya Simba ambapo alicheza kama mlinzi wa kushoto, alifanya vizuri sana.

Kutokana na umri wake ambao sasa ni miaka 20, Lusajo anao muda wa kuendelea kukua kama mchezaji na kuipa mafanikio timu. Chilambo amecheza jumla ya mechi; mechi 16 za ligi kuu, moja ya CAF na akitumia dakika 980.

3. Malickou Ndoye - 4/10

Mchezaji wa timu ya CHAN ya Senegal kabla ya kuja Tanzania. Alijiunga na Azam FC akitokea timu hiyo ya taifa iliyotoka kushiriki Cosafa kama timu mwalikwa. Na bila shaka alianza vizuri sana. Ni beki anayejua kupiga pasi ndefu yaani kuhamisha mpira, na ana nidhamu ya nafasi.

Tatizo lake kubwa ni kwamba hana kasi...yaani Yuko taratibu. Alianza vizuri sana hata kufunga goli kwenye mchezo wa 2-2 dhidi ya Yanga. Matatizo yalianzia Mbeya alipoumia dhidi ya Tanzania Prisons na kukaa nje kwa miezi mitatu.

Aliporudi uwanjani baada ya kupona, alianza taratibu na kurudi kidogo kidogo kwenye kiwango. Lakini kadi nyekundu ya shambulio aliyoipata dhidi ya Dodoma Jiji, ikamfanya akose mechi tatu mfululizo. Baada ya hapo hakuwa tena Ndoye yule aliyeonekana mwanzoni.

Matumaini pekee kwake na kwa uwekezaji wa Azam FC kwake, ni ujio wa kocha Yousouph Dabo, ambaye alikuwa naye klabuni Tengueth kule Senegal akiwa nahodha wake.

4. Isa Ndala - 6/10

Kiungo fulani hivi ambaye huwezi kumuelezea. Anakuja, anakataa...anakuja anakataa.

Ni mzuri sana akiwa na mpira lakini japo anacheza kama kiungo wa ulinzi, hana machale (instincts) ya kiulinzi. Mara nyingi hucheza pacha na Sospeter Bajana katika mtindo wa double six, yaani namba sita wawili.

Lakini hata hivyo, huwa anafanya vizuri sana katika kukaa na mpira lakini siyo kuilinda timu au kuipeleka mbele. Kitu pekee alichofanikiwa ni kumtoa kikosini Kenneth Muguna, na sasa ameondoka kabisa.

5. Kipre Junior - 7/10

Ni winga mwenye sifa zote za kuwa winga. Ana mbio, anaficha mali, ana chenga na anamfuata beki badala ya kumkimbia. Tatizo lake kubwa ni kwamba alichelewa sana kuingia kwenye maisha ya mpira wa Tanzania. Kutoka mpira wa nafasi kule Ivory Coast hadi mpira wa mabavu Tanzania, alikuwa na wakati mgumu sana.

Mabeki wa Tanzania wanafika jumla jumla mguuni kwako kama hutoi mali mapema. Kutokana na hilo, Kipre amekuwa mmoja wa wachezaji waliofanyiwa madhambi mengi zaidi kwenye msimu. Amecheza mechi 21, alizoanza ni 17 na 4 ametokea benchi.

Jumla amecheza dakika 1449, amefunga mabao 2 nakutoka pasi za 5 mabao. Amehusika katika mabao 7 ambazo ni wastani wa dakika 207 kwa kwa kila kuhusika kwa bao.

Katika umri wa miaka 22, Kipre ndiye mchezaji mdogo zaidi aliyemaliza na pasi nyingi za mabao kwenye msimu huu wa NBC Premier League 2022-23.

Ndani ya kikosi chake, analingana pasi za mabao na James Akaminko. NI Ayoub Lyanga pekee aliyemaliza na pasi nyingi za mabao kuliko yeye ndani ya kikosi cha Azam, kwenye msimu huu. Bila shaka kuna mengi yanakuja kumhusu Kipre.

6. Cleophace Mkandala - 4/10

Kiungo fundi anayejua sana kuzifingua safu za ulinzi kwa aidha pasi zake, chenga zake au kuvuta subira watu wafunguke wenyewe huku akiendelea kulinda mali.

NI bahati mbaya sana hakuwa na wasifu (profile) mkubwa mbele ya aliokuwa akigombania nao namba. James Akaminko au wakati mwingine Isa Ndala hasa pale timu ikicheza na double six, kwa hiyo akajikuta muda mwingi anaumia kukaa benchi.

7. Tape Edihno - 3/10

Jina lake la kibrazil na hata sura yake pia, Tape ni mmoja wa wachezaji waliotabiriwa makubwa Tanzania. Ilipotangazwa tu kwamba anakuja nchini, video zake zikaanza kusambaa zikimuonesha akifanya balaa kama la Maradona kwenye Kombe la Dunia la mwaka 1986 nchini Mexico.

Ukizingatia pia alikuwa akivaa jezi namba 10 huko kwao kama Maradona, Edigno alisibiriwa kwa hamu sana. Mara zikaja video zake wakiwa Misri kwenye maandalizi ya msimu mpya, Tanzania inasubiri kwa hamu. Mechi dhidi ya Yanga iliyoisha kwa sare ya 2-2 ilikuwa moja ya mechi zilizomtambulisha nyota huyo.

Lakini bahati sana kwake, alicheza vizuri dakika 20 tu, baada ya hapo akapoteza nidhamu ya kucheza kitimu na kwa nafasi na baadaye akachoka...akabaki kuzurura na kupoteza mipira.

Na hicho ndicho kilichoendelea baada ya hapo, na ujio wa kocha Lavagne ukamtoa mchezoni na kuanzia hapo hakuonekana tena hadi Disemba alipotolewa kwa mkopo kwenda Stella Abidjan ya kwao Ivory Coast.

8. Abdul Sopu - 8/10

Ni usajili bora zaidi kwa Azam FC msimu huu. Alichelewa kuingia kwenye timu na baadaye akasakamwa na majeraha. Hii ilitokana na ukweli kwamba hakupata muda wa kupumzika baada ya kumalizika kwa msimu wa 2021/22.

Aliendelea na majukumu ya timu ya taifa chini ya miaka 23 na baadaye Taifa Stars halafu akaunga moja kwa moja kwenye maandalizi ya msimu mpya kule Misri.

Akiwa huko, akaumia na kumfanya kukosa mechi za kwanza, ikiwemo ile ya Azamka dhidi ya Zesco United ya Zambia kiasi cha mashabiki kupaza sauti wakimtaka kocha kumuingiza bila kujua kama alikuwa majeruhi.

Akapona na kuanza kuingia kwenye timu kidogo kisodo lakini akaumia tena kwenye mchezo dhidi ya Al Akhdar na kukaa nje kwa muda mrefu. Alijitambusha rasmi kwa Azam FC kwenye mchezo dhidi ya Yanga alipofunga mabao mawili mbele ya mdaka mishale, Djuigui Diarra.

Baada ya hapo gari ikawaka na kumfanya amalize msimu akiwa kwenye kiwango bora.

Hitimisho

Usajili wa Azam FC wa msimu huu haikulipa kwa asilimia nyingi sana, japo haukuwa mbaya. Wachezaji waliosajiliwa, kwa asilimia kubwa wataonwsha uwezo wao kuanzia msimu ujao na kuwa balaa hapa nchini.

Mafanikio ya kupata alama nyingi msimu huu kuliko uliopita (49 kwa 59) na fainali ya Azam Sports (kutoka nusu fainali ya msimu uliopita), inaonesha kwamba kuna kitu kimeongezeka. Lakini kuanzia musimu ujao, hawa wakina Kipre watakuwa balaa zaidi kwa sababu watakuwa wamezioea ligi na hakuna cha kuwasimamisha.

Chanzo: Mwanaspoti