Klabu ya Simba imesema kuwa haiwezi kusema moja kwa moja kwamba imemaliza usajili wa wachezaji wa Kimataifa kwa sababu lolote linaweza kutokea kwa kuwa dirisha la usajili bado halijafungwa.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally wakati akizungumzia kufunga usajili wao wa msimu huu baada ya kumshusha kipa kutoka Morocco, Ayoub Lakred.
"Taarifa nilizo nazo ni kwamba usajili wa kipa kutoka Morocco, Ayoub ndio ulikuwa usajili wa mwisho kwa wachezaji wa kimataifa, lakini inawezekana baada ya kucheza mechi mbili hizi mwalimu ameona kuna hitaji jingine ama viongozi wameona kuna hitaji kwamba lifanyike jambo.
"Kwa hiyo hatuwezi kumaliza maneno kwamba tumemaliza usajili mpaka pale ambapo dirisha la usajili litakapofungwa rasmi Agosti 31," amesema Ahmed.