Usajili wa dirisha dogo la Januari unaendelea kubamba na tayari timu za Ligi Kuu England zimeendelea kufanya usajili wa kufa mtu.
Chelsea imedhihirisha hilo baada kufanya usajili wa Mykhaylo Mudryk kwa kitita cha Pauni 88 milioni akitokea Shakhtar Donetsk. Awali, taarifa ziliripoti nyota huyo wa Kimataifa wa Ukraine angejiunga na Arsenal, lakini uhamisho huo ukabuma baada ya The Blues kuingilia kati na kupindua meza.
Usajili wa Mudryk unakuwa wa tano kwa Chelsea katika dirisha hili dogo la usajili, mmiliki wa klabu hiyo Todd Boehly ametumia pesa nyingi katika kuleta nyota wapya ili kumpa nguvu kocha Graham Potter.
Chelsea imefanya usajili wa wachezaji Joao Felix, Andrey Santos, Benoit Badiashile na David Datro huku kukiwa na uwezekano mchezaji mwingine akasajiliwa.
Mpaka sasa Chelsea ndio klabu iliyotumia pesa nyingi kwenye usajili wa dirisha dogo la Januari kwenye orodha za timu za Ligi Kuu England zilizofanya usajili wa nguvu huku Liverpool na Manchester United zikiwamo.
Mbali na Mudryk kuna usajili hatari wa wachezaji uliowahi kufanyika na kutokea katika dirisha dogo la usajili la Januari ambao umetumia pesa ndefu.
Cody Gakpo (PSV Eindhoven kwenda Liverpool, 2023 – Pauni 37 milioni)
Huu ni uhamisho mpya kwenye orodha ndani ya kikosi cha Liverpool. Gakpo alihusishwa na Manchester United lakini uhamisho huu ukabuma. Nyota huyo wa Kimataifa wa Uholanzi ameanza kwa kusuasua Anfield licha ya kukiwasha kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar. Gakpo alicheka na nyavu mara mbili huko Qatar hata hivyo Uholanzi ikatolewa katika robo fainali dhidi ya Argentina.
Juan Mata (Chelsea kwenda Manchester United, 2014 – Pauni 37.1 milioni)
Mata alicheza jumla ya mechi 285 wakati anakipiga Manchester United, mabao aliyofunga ni matano pamoja na asisti 47. Mata alikuwa usajili wa David Moyes wakati anawanoa Mashetani Wekundu. Ulikuwa usajili mzuri kutokana na kiwango alichokuwa nacho kipindi anatoka Chelsea. Kwasasa staa huyo anakipiga Galatasaray baada ya kutimka Old Trafford. Mata alikuwa na mchango zaidi chini ya kocha Louis van Gaal, Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer.
Bruno Guimaraes (Lyon kwenda Newcastle, 2022 – Pauni 40 milioni)
Guimaraes alisajiliwa na Newcastle katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka jana, uwekezaji mzuri ulifanywa na klabu hiyo inayomilikiwa na Mwarabu kutoka Saudi Arabia. Nyota huyo amekuwa na mchango mkubwa chini ya kocha Eddie Howe tangu aliposajiliwa kwa kitita cha Pauni 40 milioni.
Luis Diaz (Porto kwenda Liverpool, 2022 – Pauni 49.9 milioni)
Liverpool ilipigania sana uhamisho huu hadi ikafanikiwa kunasa saini yake. Tottenham ilimnyemelea kwa karibu lakini ikashinda kuipikua Liverpool. Diaz alionyesha kiwango bora kabla ya kupata majeraha, alifunga mabao 10 na kutoa asisti nane katika mechi 38 alizocheza katika mashindano yote aliyocheza.
Bruno Fernandes (Sporting Lisbon kwenda Manchester United, Pauni 55 milioni)
Huu ni kati ya usajili bora kuwahi kutokea katika dirisha dogo la usajili la Januari na umeendelea kukumbukwa mpaka leo. Kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno ana mchango mkubwa tangu alipojiunga na United akitokea Sporting. Bruno amepewa unahodha wa timu akichukua nafasi ya Harry Maguire kutokana na ushawishi alionao. Bruno amefunga mabao 54, na kutengeneza asisti 44 katika mechi 153 alizocheza katka mashindano yote tangu alipotua Old Trafford na kuweka rekodi.
Pierre-Emerick Aubameyang (Borussia Dortmund kwenda Arsenal, 2018 – Pauni 56 milioni)
Usajili bora uliywahi kutokea Arsenal kwenye usajili wa dirisha dogo la usajili la Januari miaka mitano iliyopita. Aubameyang alikiwasha Dortmund kabla ya kutua Emirates, ambako alifunga mabao 141 katika mechi 213 alizocheza. Uhamisho wake kwenda Arsenal ulivunja rekodi ya usajili katika historia ya klabu hiyo. Aubameyang alipokuwa Arsenal alifunga mabao 93 katika mechi 163 alizocheza kabla ya kuondoka baada ya kukosa namba chini ya kocha Mikel Arteta. Kwasasa anakipiga Chelsea akitokea Barcelona.
Aymeric Laporte (Athletic Bilbao kwenda Manchester City, 2018 – Pauni 57.2 milioni)
Usajili wa Laporte ulivunja rekodi katika historia ya klabu Athletic Bilbao na Manchester City kipindi hicho cha usajili. Laporte amebeba makombe manne ya Ligi Kuu England, Carabao na FA.
Virgil van Dijk (Southampton kwenda Liverpool, 2018 – Pauni 75 milioni)
Ilichukua muda mrefu hadi uhamisho wa Van Dijk kukamilika akitokea Southampton, Liverpool ilitoa kitita cha Pauni 75 milioni na kuvunja rekodi ya usajili. Beki huyo ana mchango mkubwa tangu alipotua Anfield. Aliisadia Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 iliyopita chini ya kocha Jurgen Klopp ndani ya miaka mitano aliyokipiga Anfield.