Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Kibu Denis amejihakikishia nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha msimu ujao, licha ya maingizo mapya ya wachezaji wanaocheza nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Simba SC imewasajili viungo washambuliaji wanne wa kigeni ambao watakuwa na kibarua ya kumpoka namba Kibu aliyejihakikishia nafasi ya kucheza katika msimu uliopita chini ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Oliviera Robert Robertinho’ ambaye kipenzi chake.
Viungo hao washambuliaji waliosajiliwa na Simba SC ni Aubin Kramo, Willy Onana, Fabrice Ngoma na Luis Miquissone aliyetambulishwa juzi Jumanne (Julai 25) huko kambini Uturuki.
Kibu juzi Jumatatu (Julai 24) aliibuka shujaa katika mchezo wa kwanza wa kirafiki ambao Simba SC walicheza dhidi ya Zira FC ya nchini Azerbaijan na kuifungia bao moja katika sare ya bao 1-1.
Akizungumza jijini Dar es salaam, kiungo wa zamani wa Taifa Stars na klabu za Simba SC, Young Africans na Azam FC Amri Kiemba amesema kuwa ngumu kwa Kibu kuondolewa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, licha ya maingizo mapya ya wachezaji.
Kiemba amesema kuwa, kiungo huyo ana faida kubwa katika soka la hivi sasa, ni mchezaji mwenye kasi akiwa na mpira akishambulia goli la wapinzani.
Ameongeza kuwa anaamini kama kiungo huyo hataanza katika kikosi cha kwanza, lakini ngumu kwake kukosa nafasi ya kushiriki katika kila mchezo ambao Simba watauchea mbele ya viungo hao wapya.
“Lipo wazi kabisa kwa aina ya uchezaji ambayo anayo Kibu, hawezi kuwa mnyonge hatakama kuna maingizo mapya kiasi gani bado atapata nafasi ya kucheza.
“Ninaamini hatakama atakosa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza, lakini hawezi kukosa nafasi ya kucheza katika kila mchezo kwa maana ni mchezaji ambaye anaendana na mahitaji ya aina ya soka la kisasa.
“Hivyo viungo hao wapya wana kibarua kigumu mbele ya Kibu ambaye yeye apewi thamani kubwa, licha ya mchango mkubwa ambao amekuwa akiutoa Simba,” amesema Kiemba.