Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uraia pacha shida Stars

Bernard Kamungoo Vs Messi Bernard Kamungo

Tue, 21 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ishu ya uraia pacha kwa wanamichezo ni kati ya mijadala ambayo imekuwa ikiibuka na kupotea huku wadau wakitamani kuona suala hilo likipitishwa ili wachezaji wenye asili ya Tanzania waanze kutumika kwa kasi kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Suala hili ni pana na limekuwa na mvutano wa aina yake hata kwenye vikao vya Bunge ambako sheria na kanuni mbalimbali za nchi zimekuwa zikijadiliwa na kufanyiwa maboresho lakini kwa bahati nzuri wakati hilo likiendelea ipo hadhi maalumu ya uraia ambayo inaweza kuanza kutumika.

Hadhi hiyo inaweza kumfanya mchezaji mwenye asili ya Tanzania kuwa na uhalali wa kuitumikia Taifa Stars bila ya kulikana taifa lake jingine.

Miongoni mwa wachezaji ambao walikumbana na misukosuko hadi kupata nafasi ya kuichezea Taifa Stars ni pamoja na beki wa Portsmouth ya England, Haji Mnoga ambaye anaichezea Aldershot Town kwa mkopo.

Haji alizaliwa Portsmouth, baba yake ni Mtanzania na mama Mwingereza. Licha ya kuichezea timu ya taifa la England ya vijana wa chini ya miaka 17, beki huyo aliamua katika ngazi ya timu ya wakubwa kuichezea Tanzania na hapo ndipo TFF ilipoanza mchakato wa kumtafutia wepesi mchezaji huyo aanze kutumika maana kuikana England ambako amekuwa akitafuta ugali wake kunaweza kumweka katika mazingira magumu.

NYOTA TULIOWAPOTEZA

Fowadi wa RB Leipzig ya Ujerumani, Yussuf Poulsen aliwahi kuonyesha nia ya kuichezea Taifa Stars kama sehemu ya kumuenzi marehemu baba yake ambaye ni Mtanzania (ambaye alitangulia mbele za haki yeye akiwa mdogo).

Asili ya mchezaji huyo ni Tanga na mama yake ndiye Mdenmark. Nyota huyo aliwahi kuongea na safu yetu Mwanaspoti ya Nje ya Bongo wakati wa fainali za Kombe la Dunia za Russia na kubainisha hilo aliposema, “Nilipenda kuichezea Tanzania lakini haikuwezekana hivyo ilibidi nibadili uamuzi, nikapata nafasi ya kuliwakilisha taifa la upande wa mama.”

Nyota huyo mara kwa mara nyakati za mapumziko yake amekuwa akitua Tanzania kwa ajili ya kutembelea ndugu zake.

Adam Nditi naye ni miongoni mwa vipaji ambavyo Tanzania ilishindwa kuvitumia licha ya kuwa kwenye klabu kubwa kama Chelsea, yote hiyo ni kutokana na ugumu uliopo wa ufuatilia wa wachezaji hao pamoja na sheria ambapo ilikuwa ikiwabidi kukana uraia wa huko ambako wamezaliwa.

WAPO KWENYE HATIHATI

Nestory Irankunda ndilo jina ambalo kwa sasa linaongelewa zaidi na wadau wa soka la Tanzania kutokana na mchezaji huyo ambaye alizaliwa Kigoma kwenye kambi ya wakimbizi kusaini dili la kujiunga na miamba ya soka la Ujerumani, Bayern Munich, ambayo atajiunga nayo msimu ujao.

Irankunda anaweza kuwa kwenye kundi la wachezaji ambao Tanzania inaweza kuwapoteza kwani kuzaliwa kwake Kigoma licha ya wazazi wake kuwa Warundi anaweza kuwa na hadhi ya kuichezea Taifa Stars.

Akiongea na gazeti hili, Irankunda anasema, “Nina furaha sana kujiunga na Bayern moja ya klabu kubwa kwenye soka la Ulaya, bado sijawa na uamuzi wa wapi nitacheza kwenye ngazi kubwa ya soka, naipenda Tanzania kwa kusababu nimezaliwa na hata Burundi maana ndipo walipotoka wazazi wangu.”

Kinda huyo ameanza kutumika katika ngazi ya vijana ya timu ya taifa la Australia ambako anacheza soka la kulipwa, amekuwa huko kwa miaka mingi baada ya familia yake kupata hifadhi kutokana na hali ya machafuko ambayo ilikuwa ikiendelea Burundi ndio maana walikimbilia Tanzania alipozaliwa na wakaondoka.

Yupo pia Bernard Kamungo ambaye anaichezea FC Dallas ya Ligi Kuu Marekani (MLS). Huyu aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars cha kocha Adel Amrouche na kujiandaa kwa mchezo wa kufuzu Afcon dhidi ya Niger, alijifua na wenzake kambini Stars lakini kuna mambo ambayo inadaiwa hayakukamilika ndani ya wakati akaishia kukaa jukwaani katika mechi hiyo dhidi ya Niger.

Wiki chache mbele kinda huyo akacheza na kufunga bao dhidi ya Inter Miami ya mwanasoka bora wa dunia, Lionel Messi na akaanza kuitwa kwenye timu ya vijana ya Marekani kwa ajili ya maandalizi ya Olimpiki.

“Hii ni fursa kwangu, sidhani kama ni vibaya kuitumia maana ni ngazi ya vijana, ingekuwa ngumu kwangu kukataa, mimi bado ni Mtanzania na hilo haliwezi kubadilika,” anasema mchezaji huyo.

WASIKIE TFF

Ofisa habari wa TFF, Cliford Ndimbo anasema hakuna uraia pacha katika nchi yetu japokuwa suala hilo linasemwa sana.

Alisema kuwa mchezaji anatakiwa kuwa na pasipoti yetu ili kuonyesha kuwa ni wa kwetu ingawa wapo wachezaji wenye uraia wa nchi mbili na bado wanapata nafasi ya kuitwa timu ya taifa kwa sababu hawajawahi kuchezea nchi nyingine.

“Wapo wachezaji ambao wanakuja kutoka nje kujiunga na timu ya Taifa na wanashindwa kucheza kwa sababu ya nchi walizokuwepo sheria zake hazijawaruhusu bado. Iko wazi kuwa mchezaji anatakiwa kuchezea timu moja tu ya taifa hata kama ana uraia wa nchi mbili ili kuondoa utata wa asili yake,” anasema Ndimbo.

Ofisa huyo anaongeza kwa kusema benchi la ufundi huwa linafuatilia wachezaji ambao wako nje kwa ukaribu sana lakini wasipoonekana basi ni wazi kuwa imeshindikana kupatikana kwao kutokana na vikwazo mbalimbali.

HADHI MAALUM

Mei mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stergomena Tax aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo moja ya mambo aliyoyasema kwenye hotuba yake ni pamoja na wizara hiyo kuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia hadhi maalum diaspora wenye asili ya Tanzania na uraia wa nchi nyingine.

Chanzo: Mwanaspoti