Anajulikana kama Salima Rhadia Mukansanga. Ni mwanamke ambaye nyota yake imeng’aa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka minane iliyopita.
Salima alitajwa kuwa miongoni mwa waamuzi 129 waliochaguliwa kuwa marefa katika Kombe la Dunia la Fifa la 2022 ambalo litaanza Novemba 21 hadi Desemba 18 mwaka huu nchini Qatar. Waamuzi wa kati 36, waamuzi wasaidizi 69 na maofisa wengine 24 waliochaguliwa kutoka mashirikisho sita, ni pamoja na wanawake sita ambao watakuwa wasimamizi wa kwanza wanawake kwenye fainali hizo.
Waamuzi wa kati, Stephanie Frappart wa Ufaransa na Yoshimi Yamashita kutoka Japan wanaungana na Salima, ambaye Januari alikuwa mwanamke wa kwanza kuchezesha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanaume (Afcon) zilizofanyika nchini Cameroon.
Nyuma Neuza (Brazil), Karen Diaz Medina (Mexico) na Kathryn Nesbitt (Marekani) wanakamilisha orodha kama waamuzi wasaidizi.
“Tumefanikiwa kuwaita maafisa wa mechi wa kike kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia la Fifa. Kwa njia hii, tunasisitiza kwa uwazi kuwa kwetu kinachozingatiwa ni ubora na si jinsia,” Pierluigi Collina, Mkuu wa Kamati ya Waamuzi ya Fifa, alisema.
Fifa ilisema kila afisa wa mechi atafuatiliwa kwa uangalifu katika miezi ijayo na tathmini ya mwisho ya masuala ya kiufundi, kimwili na matibabu kufanywa muda mfupi kabla ya Kombe la Dunia.
Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) linasema jambo hili litasaidia kuhakikisha kuwa maafisa walioteuliwa wanakuwa katika hali bora wakati mpira utakapoanza kupigwa nchini Qatar.
Huyu Salima ni nani?
Ni mwamuzi wa mpira wa miguu kutoka Rwanda, ambaye alizaliwa mwaka 1988 katika Wilaya ya Rusizi. Kwa mujibu wa gazeti ‘New Times’ la Rwanda, Salima, ambaye alilelewa katika Wilaya ya Rusizi, Mkoa wa Magharibi, ana shahada ya kwanza ya Uuguzi na Ukunga aliyopata kutoka Chuo Kikuu cha Gitwe, kilichoko Mkoa wa Kusini mwa Rwanda, Wilaya ya Ruhango.
Matarajio yake alipokuwa shuleni yalikuwa kuwa mchezaji wa mpira wa vikapu, lakini haikuwa hivyo kwa sababu alikosa mahitaji mengi ya kimsingi ikiwa ni pamoja na vifaa vya mpira wa vikapu.
Hata hivyo, alielekeza nguvu zake kwenye soka, na katika mwaka wake wa mwisho katika Shule ya Sekondari ya St Vincent de Paul Musanze, alisimamia mchezo wa fainali ya mashindano ya shule na hapo ndipo ambapo njia yake ya kuelekea urefa wa soka ilianza.
“Nilipenda mpira wa vikapu, na nilitaka kuuchukua kwa uzito mkubwa, lakini upatikanaji wa vifaa vya mpira wa vikapu na makocha ulikuwa mgumu. Ndivyo nilivyoishia kwenye urefa, jambo ambalo pia sijawahi kujutia. Napenda urefa,” Mukansanga aliambia ‘New Times’ wakati wa mahojiano mwaka 2019. Mwanamke wa kwanza kuwa mwamuzi katika Kombe la Mataifa ya Afrika, ndiye mwamuzi wa kwanza mwanamke Mwafrika kuteuliwa kuchezesha Kombe la Dunia mwaka 2022.
Alianza kazi yake ya kimataifa kama mwamuzi mwaka wa 2012, kwanza kama mwamuzi msaidizi na kisha kama mwamuzi wa kati. Mechi yake ya kwanza ya kimataifa kama mwamuzi wa kati ilikuwa kati ya Zambia na Tanzania katika kufuzu kwa Mashindano ya pili ya Soka ya Wanawake ya Afrika 2014. Kisha akasimama katika Michezo ya Afrika ya 2015 huko Brazzaville, Jamhuri ya Kongo. Anasimamia mechi ya ufunguzi ya mashindano ya wanawake kati ya Nigeria na Tanzania, pamoja na nusu fainali kati ya Ghana na Ivory Coast. Pia alisimamia michuano ya CECAFA ya Wanawake ya 2016 nchini Uganda.
Jumatano, Novemba 2, 2016 Salima aliteuliwa kuwa mmoja wa marefa 10 wanawake waliosimamia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake. Wengine waliochaguliwa siku hiyo ni pamoja na Maria Packuita Cynquela (Mauritius), Gladys Lengwe (Zambia), Lidya Tafesse (Ethiopia), Akhona Zennith Makalima (Afrika Kusini), Jeanne Ekoumou (Cameroon), Aissata Ameyo Amegee (Togo), Suavis Iratunga (Burundi), Carolyne Wanjala (Kenya) na Jonesia Rukyaa Kabakama (Tanzania).
Jumatano ya Novemba 22, 2017 Shirikisho la Soka duniani FIFA lilitoa orodha ya waamuzi wa kimataifa wa Rwanda na waamuzi wasaidizi walioidhinishwa kuchezesha mechi za ndani na kimataifa mwaka 2018.
Orodha ya mwaka 2018 ilijumuisha waamuzi ishirini (20) na waamuzi wasaidizi ambao waliidhinishwa kwa beji za FIFA za 2018. Sura mpya kwenye orodha hiyo ilikuwa ni mwamuzi msaidizi Mutuyimana Dieudonne ambaye alichukua nafasi ya Niyiyegeka Jean Bosco.
Uongozi wa Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA) uliwapongeza viongozi waliochaguliwa na kuwataka kudumisha viwango vya juu wanaposimamia mechi za ndani na nje ya nchi.
Katika orodha ya waamuzi wanawake wa FIFA wa Rwanda mwaka 2018 walikuwamo Salima, Umutoni Aline na Tuyishime Angelique. Waamuzi wa kiume walikuwa ni pamoja na Hakizimana Louis, Twagirumukiza Abdoul Karim, Ishimwe Jean Claude, Ruzindana Nsoro na Uwikunda Samuel.
Waamuzi wasaidizi walikuwa ni Ndagijimana Theogene, Hakizimana Ambroise, Bwiliza Raymond Nonati, Niyonkuru Zephanie, Simba Honore, Karangwa Justin na Mutuyimana Dieudonne.
Waamuzi wasaidizi wanawake walikuwa ni Nyinawabari Speciose, Murangwa Usenga Sandrine, Umutesi Alice, Ingabire Francine na Mukayirangwa Regine.
Jumanne ya Desemba 19, 2017, kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Rwanda (ARPL) nchini Rwanda, Salima aliteuliwa kuwa ndiye atakayechezesha mechi ya raundi ya kwanza kati ya Sunrise FC na Kirehe huko Nyagatare.
Ijumaa ya Aprili 20, 2018 Salima alikuwa miongoni mwa wanawake walioingia katika mafunzo ya kutumia mfumo mpya wa teknolojia katika mchezo wa soka, Video assistant Referee (VAR) kwa mara ya kwanza kwenye Kombe la Dunia la Wanawake 2019. Mafunzo hayo yalifanyika Jijini Cairo, Misri.
Kombe la Dunia la Wanawake lilianza Ijumaa ya Juni 7, 2019 nchini Ufaransa na kumalizika Jumapili ya Julai 7 mwaka huo. Katika maandalizi ya mashindano hayo, Jumamosi Agosti 25, 2018 Salima aliorodheshwa kuwa mmoja wa waamuzi katika fainali hizo zilizofanyika huko Grenoble, Le Havre, Lyon, Montpellier, Nice, Paris, Reims, Rennes na Valenciennes. Fainali zilifanyika mjini Lyon Jumapili, Julai 7, 2019.
Mwanzoni mwa mwaka 2019 Salima alikwenda Doha, Qatar pamoja na waamuzi wengine 26 na waamuzi wasaidizi 48 kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake.
Kozi ya maandalizi ya kombe hilo kwa waamuzi wa kike ilianza Februari 2019 mjini Doha na kudumu hadi Februari 15. Kulingana na Kari Seitz, Meneja Mwandamizi wa Waamuzi wa FIFA, hiyo ilikuwa “Ni semina ya kina sana, na bora sana.”
Kozi ya Doha haikujumuisha vipindi vya mazoezi tu uwanjani na VAR bali pia masomo ya nadharia pamoja na ukaguzi wa afya na utimamu wa mwili.
Nini kiliendelea baada ya Salima kutoka Doha?
Tutaendelea kukupa