Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unaonaje Mgunda akirudi Msimbazi?

Mgunda Simba Gd Unaonaje Mgunda akirudi Msimbazi?

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ugonjwa wa kuhusudu makocha wa kigeni, bado unalitesa soka la Tanzania. Timu zetu hasa Simba, Yanga na Azam bila kocha wa kigeni, unaonekana ni kama unacheza tu. Kwa nini Simba wasimalize msimu na Kocha Juma Mgunda?

Simba wangekubali kukaa chini na kutengeneza timu nzuri ya baadaye bila presha kubwa kwa kuumpa timu Mgunda.

Pamoja na kuwa soka la Tanzania bado linaruhusu wachezaji wenye umri mkubwa kucheza kwa mafanikio lakini wasiwe wengi kikosini.

Kile kikosi cha kwanza cha Simba, naona kimejaa wachezaji wengi wakubwa. Kila nikifumba macho nawaona wenye miaka 30 wengi kikosini. Kila nikilala naona wenye miaka ishirini ya mwishoni wanaongezeka!

Simba hawahitaji kushindana na Yanga namna ya kucheza. Ni muda wa kutengeneza timu ya ushindi. Ni wakati wa kujenga timu mpya ya maangamizi. Ukiwa na wachezaji watano kwenye kikosi cha kwanza ambao umri wao ni zaidi ya miaka 30, kasi ya uchezaji wako itapungua tu.

Matumizi ya nguvu uwanjani yatapungua mara dufu! Sina tatizo na Simba kuleta kocha mwingine wa kigeni, lakini wangempa timu Mgunda wangepatia sana. Mgunda ni bonge moja la kocha sema kwa sababu Yanga ina kocha mgeni, na wao wanataka kushindana nao.

Septemba 7, 2022 siku chache kabla ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mserbia Zoran Maki aliyedumu kwa siku 70 ikiwa ni sawa na miezi miwili na siku 10 tu, Mgunda alikabidhiwa timu. Kuna mabadiliko makubwa sana yalitokea.

Uchezaji ulibadilika. Morali ya wachezaji ilikwenda juu. Taratibu tuliona timu inarejea kwenye ubora wake. Pengine kama Simba ingemwamini na kmtafutia wachezaji wazuri, leo tungekuwa tunaongea mengine. Mgunda ni kocha sahihi sana pale Simba, basi tu anatoka Tanga. Bado hatuna adabu na makocha wazawa. Hata afanikiwe kiasi gani, bado tunaheshimu sana wageni.

Sina tatizo na kocha wa kigeni wanayemtambulisha Simba, lakini nadhani Mgunda angetosha sana kuwavusha hadi mwisho wa msimu. Anajua sana ligi yetu. Anawajua sana wachezaji wetu. Angewavusha Simba.

Angewashangaza wengi. Julian Nagelsmann, Kocha wa Kijerumani siku moja alisema ‘Kuwa kocha bora unajitaji kutengeneza mahusiano mazuri na wachezaji kwa 70% na Mbinu 30%.”

Kwa watu ambao wamewahi kukaa pamoja na Mgunda wanajua kabisa ni mchawi wa hayo mambo yote mawili. Anajua sana kucheza na akili za wachezaji. Anajua namna bora ya kuwaandaa ili wampate Matokeo mazuri. Kwenye ufundi ndiyo usiseme, ni vile tu Bongo bahati mbaya. Najua wote tunaitazama Simba kwa macho tofauti.

Simba wanahitaji sana mtu wa kuja kutengeneza timu ya ushindani itakayodumu hata misimu mitano. Ujenzi wake hautaki presha kubwa. Mgunda anaweza sana kutengeneza timu hiyo. Naheshimu mawazo ya viongozi wa Simba kuendelea kuamini makocha wa kigeni, lakini kwa namna ninavyoiona Simba, wangebaki tu na Mgunda.

Hata hawa wachezaji waliopo kwa sasa, sio wanyonge kiivyo.

Wakipata kocha mzuri wa kuwaamsha, kinawaka. Moto Juu ya moto.

Wakati mwingine kocha wa kigeni linakuwa ni jina tu.

Ni kweli wapo makocha wengi wa kigeni wazuri na wameipatia Simba mafanikio lakini kwa nyakati hizi hata Mgunda angetosha.

Pamoja na Umri mkubwa wa wachezaji wengi kikosini lakini Simba inaweza kucheza vizuri chini ya Mgunda.

Pamoja na kupitia Matokeo magumu mechi zake za mwisho, Mnyama anaweza kuamka tena chini ya Mgunda.

Sina tatizo hata kidogo na Simba kuleta kocha mpya wa kigeni lakini kuna jembe yuko pale angewafaa.

Ifike wakati tuwajengee uwezo makocha wetu wazawa na kuwaamini. Wapo wenye uwezo. Wapo wanaoweza kuandikisha historia mpya ya soka letu. Mgunda ni moja ya makocha hao.

Simba kwa sasa wanahitaji kocha mwenye mbinu na mtu mwenye kucheza vizuri na akili za wachezaji waliojeruhiwa. Ni kama kuna pepo mchafu amepita. Ni kama wamekanyaga mti mbaya porini. Wakishapona kichwani, Simba wataamka tena.

Tuliona Mgunda kwenye mechi za kimataifa akiwa na Simba, Aliupiga mwingi sana. Mtu kama yule anahitaji mambo makubwa mawili. Mpeni wasaidizi wazuri na wachezaji wazuri. Anatoboa.

Ukishamwekea Wasaidizi wa kiwango kikubwa na kumpa wachezaji wazuri, ni kocha mzuri wa kukupa matokea mazuri. Ni vile tu Bongo bahati mbaya. Ni vile tu bado tunasumbuliwa na pepo la kupenda makocha wa kigeni.

Pamoja na kupitia wakati ngumu hivi karibuni, lakini Simba wakipata kocha mzuri, nawaona wakiamka tena. Nawaona wakianza kushinda tena mechi moja baada ya nyingine.

Najua wote tunaitazama Simba kwa macho tofauti, unaonaje kama Simba wangempa timu Mgunda? Tumie maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba ya simu hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti