Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unamjua au unamsikia Clatous Chama? Hili ndilo balaa lake

Clatous Chama Egypt Clatous Chama

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya kwamba jina lake haliimbwi sana msimu huu lakini Clatous Chama ni mmoja wa wachezaji wenye mchango mkubwa katika upatikanaji wa mabao katika kikosi cha Simba ndani na nje ya nchi.

Chama kufanya kwake vizuri ni kama anazaliwa upya kwani msimu uliopita mshambuliaji hakuwa kwenye kiwango kikubwa baada ya kurejea katika kikosi cha Simba akitokea RS Berkane ya Morocco.

Msimu wa 2019/20 alichukua tuzo ya mchezaji bora akiwapiku Nico Wadada na Bakari Mwamnyeto, wakati alichukua tuzo ya kiungo bora mbele ya Lucas Kikoti na Mapinduzi Balama.

Msimu huu mpaka sasa amehusika katika mabao 11 ambayo Simba imeshinda kuanzia mchezo wa Ngao ya Jamii, Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika ambako sasa amekuwa gumzo zaidi Mnyama akisaka tiketi ya kufuzu makundi.

Chama alianza kwa kutoa pasi ya bao katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao walifungwa 2-1 na Yanga, dakika 16 alitoa pasi ya bao kwa kuinua mpira juu na Pape Ousmane Sakho aliuweka wavuni.

Katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold ambao Simba ilishinda 3-0, Chama alihusika katika bao la pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Peter Banda na yeye aliingia ndani ya boksi na kupiga pasi kwa Moses Phiri na kuweka mpira wavuni.

Chama akaja kuhusika katika bao la tatu akiifungia Simba kwa mkwaju wa penalti baada ya Agustine Okrah kuangushwa ndani ya boksi.

Kwenye mchezo wa pili Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, Simba ilishinda 2-0 na aliendelea kuhusika kwenye mabao ya timu hiyo baada ya kufanyiwa faulo nje ya boksi na yeye alipiga faulo na kwenda kugonga mwamba na mpira uliporudi Moses Phiri aliunganisha kwa kichwa na mpira kwenda wavuni.

Mchezo wa tatu Ligi Kuu dhidi ya KMC ambao ulimalizika kwa sare 2-2, Chama aliichangia isawazishe dakika 89 baada ya kuchonga krosi ya juu na kugongwa kichwa na Moses Phiri na kwenda kwa Mohamed Outara aliyeunganisha kwa kuupiga na kukutana na Habib Kyombo aliyeweka wavuni.

Baada ya hapo Simba ilienda ugenini kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Nyasa Big Bullets na Chama alihusika katika bao moja katika ushindi walioupata wa 2-0.

Chama aliudokoa mpira wa faulo na kwenda kwa Kibu Denis ambaye aliucheza kwa kichwa na kudondokea kwa Moses Phiri ambaye alibinuka tiktaka na mpira kwenda wavuni.

Dakika 83 Chama alimtengenezea pasi ya bao John Bocco baada ya kuwatoka mabeki wa Big Bullets na kumpigia pasi Bocco ambaye alitupia.

Katika mchezo wa marudiano ambao Simba ilishinda tena 2-0, Chama alitengeneza bao la kwanza baada ya kupiga pasi mpenyezo kwa Moses Phiri ambaye alitulia na kuweka mpira wavuni.

Baada ya mchezo huo Simba iliichapa Dodoma Jiji 3-0 huku Chama akihusika kwenye bao moja baada ya kupiga krosi na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akiwa kwenye harakati za kuokoa aliugonga mpira na kwenda wavuni.

Chama akaja kuhitimisha ubora wake kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa tena dhidi ya C.D Primeiro de Agosto baada ya kufunga bao moja na kutoa pasi moja wakati Simba ikishinda 3-1.

Chama alifunga bao dakika ya 8 akiwa ndani ya boksi baada ya kupokea pasi kwa Agustine Okrah na yeye aliutuliza na kuweka mpira wavuni kwa shuti la chinichini.

Kiungo huyu alikuja kuhusika katika bao la pili baada ya kupigwa shambulizi la kushtukiza na Mzamiru Yassin alimpigia pasi Chama ambaye alitulia na kupiga pasi kwa Sadio Kanoute ambaye alimpigia pasi ya mwisho Israel Mwenda aliyefyatuka shuti na kwenda wavuni.

WADAU WAKIRI

Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema Chama msimu huu ameuanza vizuri na anajitambua kwani amekuwa hakubali awe chini bali aendeleze moto wake na jambo hilo linaonekana ndani ya uwanja. “Ufanisi wake upo juu, anajituma anapokuwa uwanjani na kutambua yeye ni mgeni inabidi awe wa tofauti, wachezaji wazawa wanabidi waige baadhi ya vitu kutoka kwake,” alisema Kigodeko ambaye ni mchezaji wa zamani wa Ashanti.

Kauli hiyo iliungwa mkono na nyota wa zamani wa timu ya Taifa Tanzania, Zamoyoni Mogela aliyesema; “Ni mchezaji ambaye hapendi kiwango chake kiwe chini, wachezaji wazawa inabidi wapate darasa kutoka kwake kwani kadri siku zinavyokwenda mbele anazidi kuwa kwenye kiwango cha juu.”

Chanzo: Mwanaspoti