Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unamjua anayefungwa leo kwa Mkapa?

Mashabiki Wa Simba V Yanga Unamjua anayefungwa leo kwa Mkapa?

Sun, 23 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ukitazama usajili wa Stephane Aziz KI, Bernard Morrison na uwepo wa Fiston Mayele, bila shaka yeyote hakuna ambaye aliamini kama Yanga inaweza kutolewa kabla ya hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ukitazama usajili wa Augustine Okrah, Victor Akpan, Habib Kyombo na kocha Mzawa, Juma Mgunda kila mtu alikuwa anadhani Simba hamna kitu msimu huu. Kumbe mambo yanabadilika?

Kumbe soka sivyo lilivyo. Sina hamu nao. Ni vigumu sana kutabiri Dabi ya Kariakoo kwa sababu mara nyingi matokeo ya mchezo huu, hayaakisi moja kwa moja ubora wa timu kabla ya mechi. Hii ni mechi flani hivi kigeugeu. Hii ni mechi flavi hivi ambayo kila mmoja anaona anakwenda kushinda kwa Mkapa.

Unamjua anayefungwa leo kwa Mkapa? Naomba jibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi kuipitia namba yangu ya simu hapo juu.

Mechi hii mwenzio imenishinda kutabiri. Ni mechi ambayo haijalishi nani anaanza kwenye kikosi cha kwanza. Ni mechi ambayo haijalishi nani amekuwa na rekodi nzuri kabla ya kukutana.

Hii kwa Tanzania ni mechi mpya yenye kuleta matokea mapya kila siku. Kwa mtazamo wa karibu unadhani ni kama mechi ya Mayele na Phiri, lakini kumbe inaweza kuamuliwa na Kibwana Shomary.

Unaweza kudhani ni mechi ya Augustine Okrah na Aziz KI, kumbe mabao yapo kwa John Bocco. Ni mechi muhimu sana kwa kocha Mgunda. Tayari kuna kitu ameanza kuwaaminisha mashabiki na wapenzi wa Simba kuwa inawezekana timu ikawa salama kwa kutumia kocha mzawa.

Tayari ameanza kuwaaminisha wana Simba anaweza kutimiza malengo ya klabu msimu huu. Hata kama wamefika hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, furaha kubwa ya wana Simba ni kumfunga mtani jioni ya leo kwa Mkapa.

Simba amesumbuka sana mbele ya Yanga kwenye ligi ndani ya misimu hii miwili na nusu. Ni muda wa Mgunda kuwapa furaha Simba. Ni mechi ngumu sana kwa kocha Nasreddine Nabi Kwa sababu wana Yanga wanataka ushindi tu leo.

Mashabiki wa Yanga wamechanganyikiwa baada ya kutolewa mapema na Al Hilal kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Hawaamini macho yao.

Njia pekee ya kujipoza ni kumpasua mtani jioni ya leo. Kibarua pia cha Nabi kinakuwa salama zaidi kama atashinda mechi hii.

Mechi ya Simba na Yanga ni kama kombe lingine nchini. Ndiko iliko furaha ya juu kwa mashabiki na viongozi wa soka. Ndiyo mahali ambapo unaweza kusamehewa ‘dhambi’ zako zote.

Kama ndugu yangu una ujuzi wa kutabiri mechi hii, nitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Pamoja na kuwapeleka Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, mashabiki wanataka Mgunda ashinde leo. Asiposhinda watu wanaweza kugeuza mtazamo juu yake na kutaka kocha Mzungu aje. Pamoja na presha kuwa kubwa sana kwa Nabi, kama atashinda leo anaweza kujikuta yuko mikono salama hata kama atakuja kufungwa na Club Africain kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii ndiyo nguvu ya mechi hii. Huu ndiyo umuhimu wa mchezo wa leo. Nabi kama anafanya masihara, mechi ya Club Africain anaweza asifike.

Kama Mgunda anafanya masihara, anaweza asiwe na Simba tena kwenye mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ni mechi ambayo hata asiyefuatilia matokeo ya ligi nzima huwa anataka kujua kilichojiri.

Hii ni mechi ambayo hata ugomvi wa wana Ndoa kuna muda huwa unamalizwa kwa matokeo ya mechi hii. Ni mechi yenye nguvu za ajabu. Bao linaweza kufungwa na Feisal Salum kwa Mkapa, ukasikia kuna shabiki amepoteza maisha Kigoma kwa mshituko!

Bao linaweza kufungwa na Mohammed Hussein kwa Mkapa, ukasikia kuna mtu ameachana na mkewe kule Mtwara. Kifupi hii ni zaidi ya mechi. Imenishinda kabisa kutabiri kabisa.

Unadhani nani anapoteza leo kwa Mkapa? Niandikie maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Natamani kuona ukubwa wa Moses Phiri kwenye mechi kama hii. Ufalme wa Soka la Tanzania unapatikana kwenye mechi kama hizi.

Watu kama kina Emmanuel Okwi, Amissi Tambwe, Meddie Kagere, Donald Ngoma walijiweka kwenye moyo wa mashabiki wa soka kwenye mechi kama hizi.

Ni muda wa Phiri kutengeneza ufalme wake. Cloatus Chama amepata Ufalme sio tu kuwafunga Al Ahly, amewanyanyasa pia Yanga vya kutosha.

Fiston Mayele pamoja na mambo mengine, hizi ni mechi ambazo zimempatia heshima kubwa sana pale kwa Wananchi.

Hakuna raha kwenye mpira wa Tanzania kama kumfunga mtani. Kuna kila dalili ya kupata mechi bora jioni ya leo kama waamuzi pia watakuwa bora. Vikosi vimejaa mafundi sana kwa pande zote mbili. Unadhani nani anakufa jioni ya leo?

Nitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Itakuwa ni heshima kubwa sana kwa Mgunda kuwafunga Yanga.

Itakuwa ni salama zaidi kwa kocha Nabi kushinda mchezo huu. Kama Yanga wanapoteza mashabiki hawatokumbuka tena kuwa wamecheza mechi 42 za Ligi Kuu bila kufungwa.

Yatakuwa ni machungu juu ya machungu. Sare kidogo inaweza kutuliza moto kwa pande zote mbili huku Simba wakitaka kumuona kocha atawapa nini hatua ya makundi, wakati Yanga wakitaka kuona kama Nabi atawavusha dhidi ya Watunisia kwenye mechi ya mtoano kuelekea hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti