Salma Paralluelo, 19 aliingia akitokea benchi kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake dhidi ya Sweden na kufunga bao matata lililoivusha Hispania na kutinga fainali ya kwanza kwenye historia katika mchezo huo.
Lakini, bao hilo la Salma lilikuwa la pili akifunga mfululizo kuisaidia Hispania, baada ya kufanya hivyo kwenye robo fainali pia na kuonyesha yupo vizuri.
Hispania ilitinga nusu fainali ya Kombe la Dunia la wanawake na kuonekana kuwa na kibarua kigumu mbele kutokana na Sweden kuwa na mshindi wa Ballon d’Or mara mbili, Alexia Putellas na Aitana Bonmati ambaye anapewa nafasi ya kutwaa tuzo hiyo kwa mwaka huu 2023.
Lakini kwa mara nyingine tena, Salma aliibuka shujaa kwa Hispania na kuwa kivutio zaidi kwenye fainali hizo. Ikumbukwe kinda huyo aliivusha Hispania kwenye robo fainali kwa kufunga bao la ushindi (2-1) dhidi ya Uholanzi ndani ya dakika 30 za ziada baada ya matokeo kuwa 1-1.
Salma aliingia dakika ya 57 katika mchezo huo wa nusu fainali na kupachika bao lake la pili mfululizo dakika ya 81, Sweden ilichomoa dakika ya 88 kupitia kwa Rebecka Blomqvist kabla ya Olga Carmona kufunga bao la pili kwa Hispania inayonolewa na nyota wa zamani wa Real Madrid na FC Barcelona, Jorge Vilda.
Licha ya hayo, jina la Salma sasa liko midomoni mwa kila mtu anayefuatilia fainali hizo za wanawake huko Australia kuelekea siku za mwisho za mashindano haya ambayo ni Jumapili ambapo utachezwa mchezo wa fainali kati ya Hispania dhidi ya Australia/England.
“Tumefanikiwa. Tumepigana hadi mwisho wa mashindano. Tunaamini tunaweza kufanikiwa,” anasema Salma.
Salma alizaliwa katika Jiji la Kaskazini-Mashariki la Zaragoza, baba yake ni Mhispania na mama yake anatajwa kutokea Guinea ya Ikweta, aliwakilisha Hispania katika riadha na soka, akifanya vyema kwenye mbio za mita 400 (yadi 437) hadi katika mbio zake za ushindani mwaka 2020.
“Nilianza michezo yote miwili nikiwa na umri wa miaka saba,” anasema Salma na kuongeza kuwa anaifurahia michezo yote miwili licha ya watu kumwambia ashikamane na mchezo mmoja.
Hatimaye aliamua kujikita zaidi kwenye soka lakini alikumbana na majeraha ambayo yalimfanya kuwa mbali na michezo yote miwili kwa wakati mmoja.
“Ilinifadhaisha kwa sababu sikupona vizuri kutokana na majeraha yangu na sikuweza kutoka na kuwa mwanariadha tena. Kama ningeendelea, hata hivyo, ningepoteza zaidi,”€ anasema.
Felix Laguna, mkufunzi wa riadha wa Salma aliiambia The Athletic kwamba “Ikiwa angechagua riadha asingekumbana na majeraha, angeishia kufanya vizuri kwenye fainali ya riadha kwenye Michezo ya Olimpiki.”
Mwaka 2019, Salma aliondoka katika klabu ya mji wake na kujiunga na Villarreal, ambapo alikaa miaka mitatu, akifunga mabao 23 katika mechi 37 lakini alipata jeraha la goti lake la kushoto Aprili 2021 na kumuweka nje kwa miezi tisa.
Alijiunga na Barcelona Julai 2022. Klabu hiyo inajivunia kuwa na wachezaji wengi zaidi (tisa) kwenye kikosi cha Hispania kwenye dimba la Down Under na ilishinda Ligi ya Mabingwa pamoja nao Juni hii.
UWEZO MKUBWA
Tangu ajiunge na kikosi cha Hispania kwa Kombe la Dunia, Salma amepokea sifa nyingi kutoka kwa Vilda, ambaye anamwita mchezaji mwenye kasi, nguvu na ‘kipaji cha kuzaliwa’.
“Yeye ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anaweza kufika mbali kwenye maisha yake ya soka,” anasema Vilda.
Salma alianza kila mechi kwa Hispania kabla ya robo-fainali na alifanya makubwa katika ushindi wa mabao 5-1 Hispania dhidi ya Uswis katika hatua ya 16 kwa kusababisha mabao mawili ya Aitana Bonmati.
NI VIGUMU KUPATA WACHEZAJI KAMA YEYE
Huku Alexia Putellas akiendelea kupata utimamu kamili baada ya jeraha baya la goti, kiungo Bonmati amekuwa kiongozi katika timu ya Vilda.
“Yeye ni wa kipekee,” anasema Bonmati kuhusu Salma.
“Ni vigumu kupata wachezaji kama yeye, ambao asili yao ni riadha na mwenye ubora mwingi mguu wake wa kushoto. Tunapocheza pamoja, tunachanganya vizuri, na tunamchezesha mipira ya juu na chini.”
Salma atakuwa na jukumu kubwa kwenye mchezo wa fainali mashabiki wengi wa soka yatakuwa kwake hiyo Jumapili kwenye Uwanja wa Australia, Sydney.