Hakuna anayeamini kwamba kazi itakuwa rahisi leo Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, kwa kuwa kila timu inahitaji pointi tatu pale Yanga itakapokuwa mwenyeji wa Geita Gold.
Unaijua dhahabu? Basi watoto wa Jangwani wana majibu yake, ikishindikana ngoma itakuwa imerejea ilikotoka pale Geita.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, msako wa pointi tatu unachambuliwa hapa;.
PENALTI YA UTATA Oktoba 29, mwaka jana, walipokutana Uwanja wa Kirumba, Mwanza, ubao ulisoma Geita Gold 0-1 Yanga, ambapo bao lilipachikwa na Bernard Morrison kwa penalti.
Penalti hiyo ilizua utata kutokana na mazingira ya upatikanaji wake, hivyo utata ule utaongeza umakini kwa wachezaji kutofanya makosa karibu na boksi pamoja na waamuzi kuongeza umakini.
Florentina Zabron alikuwa mwamuzi wa kati kwenye mchezo huo ambapo George Wawa alionekana kuugusa mpira kwa mkono akiwa nje ya 18 baada ya Heritier Makambo kupiga kuelekea kwenye lango la Geita Gold.
Daniel Lyanga ambaye ni nahodha wa Geita Gold, katika tukio hilo alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 42 kutokana na kuonekana kupishana kauli na mwamuzi.
UBINGWA, TANO BORA Yanga wanapambana kuendeleza mwendo mzuri kuelekea kuteteta ubingwa, huku Geita Gold hesabu zao zikiwa ni kumaliza ndani ya tano bora.
Kwenye msimamo, Yanga ina pointi 62 baada ya kucheza mechi 23, inakutana na Geita Gold ambayo ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 34.
MBINU ZA MTUNISIA, MZAWA Mbinu za Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi raia wa Tunisia, zitakuwa zinapambana na mbinu za mzawa, Fred Felix Minziro.
Nabi kwenye mechi 23 alizoiongoza Yanga msimu huu, ni mchezo mmoja pekee kapoteza, ilikuwa dhidi ya Ihefu aliposhuhudia ubao ukisoma Ihefu 2-1 Yanga.
Wakati huo Ihefu ilikuwa chini ya Kocha Juma Mwambusi ambaye ni mzawa. Minziro amekiongoza kikosi cha Geita Gold kwenye mechi 24, huku akiambulia maumivu kwenye mechi 6 na ushindi ni mechi 8, sare zikiwa 10.
ULINZI NI SHIDA KWENYE MGODI Mgodi wa Geita Gold, unaonesha kuwa na tatizo kwenye safu yake ya ulinzi kutokana na kutunguliwa mabao mengi zaidi ya Yanga.
Ni mabao 31 wametunguliwa, huku ule ukuta wa Yanga ukiwa umetunguliwa mabao 10, ukiwa ni namba moja kwa timu ambazo zimefungwa mabao machache.
Bakari Mwamnyeto wa Yanga, ameanza kuimarika huku Dickson Job kazi yake ikiwa kubwa kwenye eneo la ulinzi na Djigui Diarra akiwa ni namba moja kwa makipa ambao wametunguliwa mabao machache.
WANAKUJA KWA KASI Fiston Mayele, huyu hatabiriki, akiliona lango anafikiria kufunga jambo linalomfanya kuwa namba moja kwa wale wenye mabao mengi ndani ya Yanga akiwa nayo 15.
Pia kuna Stephane Aziz Ki, huyu ni mtaalamu wa mapigo huru, mwingine ni Clement Mzize. Wote hawa sio watu wazuri kwa wapinzani.
Elias Maguli, moja ya washambuliaji wanaofanya vizuri ndani ya Geita Gold, alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wanawania tuzo ya mchezaji bora Februari ambayo ilikwenda kwa Yacouba Songne wa Ihefu, hivyo naye anakuja kwa kasi.
WANAOKOSEKANA Morrison na Aboutwalib Mshery, bado hawajawa fiti, wanatarajiwa kukosekana huku Juma Luizio kwa upande wa Geita Gold naye anatarajiwa kukosekana kwa kuwa bado hajawa fiti.