NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa mikono ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula iliwazuia kupata ushindi kwenye mchezo wao wa ligi.
Juzi, Uwanja wa Mkapa, Yanga ilikuwa na kazi ya kusaka ushindi mbele ya Simba lakini ubao wa ulisoma Simba 0-0 Yanga na kufanya timu hizo kugawana pointi mojamoja.
Nabi amesema kuwa isingekuwa ni Manula basi wangeifunga Simba kwenye mchezo huo kwa kuwa walitengeneza nafasi nyingi ambazo zilikuwa zinawapa uhakika wa ushindi.
“Kipa wao yule wa Simba, (Aishi Manula) amefanya kazi kubwa kwenye kuokoa mipira yetu, kwa mfano kuna mpira ulipigwa na Said Ntibanzokiza unadhani asingekuwa imara nini kingetoa zaidi ya kuwa bao?
“Itoshe kusema kwamba ni kipa mzuri na ukitengemea kwamba ni kipa ambaye anadaka kwenye timu ya taifa, (Taifa Stars). Ni mambo ya mpira huwa yanatokea lakini ninawez akusema kwamba wachezaji wangu walicheza vizuri,” alisema Nabi.
Manula anafikisha jumla ya mechi nane kukaa langoni huku akiwa ameruhusu kufungwa mechi mbili mabao mawili na kwenye mechi sita alikuwa shujaa kwa kuwa hakufungwa.