Vijana wa Mbogo Maji wamezidi kujichimbia kwenye mashamba ya mpunga ikijiandaa kwenda kuikabili Yanga katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Mkapa, mchezo utakaopigwa Jumatatu.
Ihefu ndiyo timu ambayo ilivunja rekodi ya Yanga ya kutofungwa michezo 49 ya Ligi Kuu Bara ilipoichapa Novemba 28 mabao 2-1, Uwanja wa Highland Estates, Mbarali kwa mabao ya Never Tigere na Lenny Kissu huku bao la Yanga likifungwa na Yanick Bangala.
Afisa Habari wa timu hiyo, Peter Andrew alisema kikosi hicho kipo kwenye morali kubwa kutokana na matokeo mazuri ambayo wamekuwa wakiyapata hivi karibuni.
"Kocha amekuwa akiwapa wachezaji mazoezi mara mbili kwa siku hii yote sababu ya maandalizi ya mchezo huo na kabla ya kuondoka atapunguza na kufanya mara moja kwa siku.
"Tunatarajia kuondoka Ijumaa kwenda Dar es Salaam, ili tuweze kupata muda wa kutosha zaidi wa kujiandaa na mchezo huo ambao ni muhimu zaidi kwetu katika kupambana na kuondoka eneo tulilokuwepo," alisema Andrew.
Hata hivyo, kocha wa kikosi hicho, Zuber Katwila alisema maandalizi yao siyo kwa kuiangalia Yanga pekee bali kuwaweka sawa vijana wake kwa maandalizi ya michezo yote iliyokuwa mbele yao.
"Mchezo huo mgumu kwetu na hatuwezi kuangalia kile tulichokipata katika mchezo uliopita au tutaingia uwanjani na mbinu kama zile sababu kila wakati tunabadilika kulingana na mazingira.
"Tunapambania alama tatu kama ilivyo kwa Yanga ambao inahitaji kuendelea kuongoza ligi lakini upande wetu tunahitaji kukaa nafasi nzuri zaidi ya hapa tulipo sasa," alisema Katwila.
Ihefu tayari imeachana na wachezaji watano, Joseph Kinyozi, Taji Omary, Evarigestus Mujwahuki, Wema Sadock pamoja na Ally Ramadhan 'Oviedo' na bado wanatarajia kutembeza panga kabla ya kutangaza wachezaji wapya.