Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Unaambiwa Azam FC sasa wamejipata haswa

Azam Vs US Monastir Huko Azam sasa wamejipata haswa

Wed, 26 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Azam FC imeendelea kujifua katika mji wa Sousse nchini Tunisia ilipokita kambi ya wiki tatu kwa maandalizi ya msimu mpya lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Msenegal Youssouph Dabo amewamwagia sifa mastaa wake kwa kuonyesha kiwango cha juu.

Dabo amesema, kila siku amekuwa akipata picha mpya kutoka kwa mchezaji mmoja mmoja na timu nzima kwa ujumla lakini kubwa zaidi amewasifia wachezaji wake kwa kujitoa na kupambana.

"Tumekuwa na vipindi tofauti tukifanya mazoezi ya nguvu na mbinu kwa nyakati tofauti.

“Nafurahi kuona wachezaji wakijituma bila kuchoka na kuhakikisha wanafanya yale tunayowaelekeza. Nawapongeza kwa hilo," alisema Dabo.

Aidha kocha huyo alizungumzia matunda ya mechi za kirafiki tatu walizocheza Azam hadi sasa huko Tunisia wakianza kwa ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Al Hilal ya Sudan, ikafuata ile waliyopoteza kwa kufungwa 3-0 na Esperance na kushinda 2-1 mbele ya US Monastir.

"Ni mechi ambazo tunachokiangalia zaidi siyo matokeo bali ni namna gani wachezaji wetu wamepokea na kufanyia kazi kile tulichowaelekeza mazoezini.

“Kwa kiasi fulani wamefanya vizuri lakini tunaendelea kuwajenga ili kufanya vizuri zaidi. Kila hatua tunayopiga kuna kitu kinaongezeka na mwisho tutakuwa na timu imara msimu ujao," alisema Dabo.

Azam tayari imefunga usajili wake ikisajili wachezaji wanne wapya ambao ni Feisal Salum 'Fei Toto', Wasenegal beki, Cheikh Tidiane Sidibe, na mshambuliaji Alassane Diao, Sambamba na kiungo Mgambia Djibril Sillah.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live