Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ulinzi ndiyo tatizo Mtibwa Sugar

Mtibwa Ligi Kuu Ulinzi ndiyo tatizo Mtibwa Sugar

Fri, 17 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Mtibwa Sugar ikiwa mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo 27 na kukusanya jumla ya pointi 20, ila inashika nafasi ya nne kwenye timu 16 ambazo zimefunga idadi kubwa ya mabao msimu huu, huku ikionekana kuwa na tatizo kubwa kwenye eneo la ulinzi.

Timu hiyo inayopambana na janga la kushuka daraja, imefunga jumla ya mabao 27 ikizidiwa na mabingwa Yanga ambao waliofunga (60), Azam FC inayoshika ya pili (54) na Simba ya tatu iliyofunga 51.

Nyota wa timu hiyo anayeongoza kwa mabao ni Seif Karihe mwenye matano akifuatiwa na Matheo Anthony aliyefunga manne huku, Omary Marungu na Charles Ilanfya wakifunga matatu kila mmoja.

Licha ya kuonekana tishio kwenye kufunga, ila imekuwa na changamoto kwenye eneo la kujilinda ikiwa ndiyo inaongoza kwa timu iliyofungwa mabao mengi msimu huu, baada ya kuruhusu mara 46, ikifuatiwa na KMC (38), Singida Fountain Gate na Tabora United zilizoruhusu 34 kila moja.

Mtibwa imeonekana kuwa na wastani wa kuruhusu mabao mawili kwenye kila mchezo ambao imecheza msimu huu, lakini ikiwa na wastani mzuri wa kufunga bao moja kwenye mchezo, jambo ambalo linaonyesha kuwa kama safu ya ulinzi ingekuwa imara timu hiyo ilitakiwa kuwa nafasi salama kwa sasa.

Sababu kubwa ya kuruhusu idadi kubwa ya mabao inatokana na kufanyika mabadiliko ya mara kwa mara kuanzia eneo la kipa ambapo licha ya uwepo wa Mrundi, Justin Ndikumana aliyejiunga na timu hiyo Januari mwaka huu akitokea Coastal Union ila amekuwa akifanya makosa mengi, lakini pia ugomvi wa safu ya ulinzi wa mara kwa mara.

Mfano mzuri kwake ni katika mchezo wa Aprili 29, ambao Mtibwa ilipoteza kwa mabao 2-1, dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo ambapo alifanya kosa lililosababisha bao la pili la Sixtus Sabilo dakika ya 90.

Baada ya mchezo huo, aligombana na wachezaji wenzake hali iliyomfanya kocha wake, Zubery Katwila kumweka pembeni katika michezo yao iliyofuata na kumpa nafasi Mohamed Makaka.

Mbali na hilo, ila ni miongoni wa timu zilizoshinda michezo michache zaidi msimu huu (5), kama ilivyokuwa kwa Geita Gold na Tabora United.

Pia inaongoza kwa kudaiwa mabao mengi (19) ikifuatiwa na Tabora United (17) na Geita Gold (14) ambazo zote zinapambana kubaki.

Mtibwa Sugar inayoburuza mkia na pointi 20, ikiwa itashinda mechi tatu zilizobakia itafikisha pointi 29 ambazo zinaweza kuitoa mkiani kutegemea na matokeo ya timu nyingine zilizopo juu yake, lakini kama ikipoteza mchezo ujao itajiweka kwenye asilimia kubwa ya kushuka.

Michezo ya Mtibwa iliyobaki itaanza na Namungo FC kwenye Uwanja wa Manungu Complex Mei 20, kisha kumalizia mechi zote mbili ugenini ikianza na Mashujaa ambayo haipo salama kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma Mei 25, na kuifuata Ihefu CCM Liti Singida, Mei 28.

Mchezo wa kwanza Mtibwa ilichapwa bao 1-0 na Namungo, Desemba 7, mwaka jana na ilipokutana na Mashujaa ilishinda mabao 2-1, Desemba 19, mwaka jana kisha kuchapwa 3-2 na Ihefu Februari 12, mwaka huu jambo ambalo haitokuwa rahisi zaidi kwao kwenye mechi zilizobaki.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Zubery Katwila alisema ushindani umekuwa mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu jambo ambalo limekuwa likitoa presha zaidi kuanzia kwenye benchi la ufundi hadi wachezaji wenyewe katika kila mchezo husika.

"Timu hazijapishana pointi nyingi ndio maana unaweza ukashinda mchezo mmoja tu ukatoka nafasi ya chini na kusogea juu zaidi, tunaendelea kupambana kwa sababu ukiangalia tulipo sio sehemu salama na sitaki kuona tunarudi tulikotoka tena."

Kwa upande wa kipa wa timu hiyo, Mohamed Makaka alisema bado hawajakata tamaa na wanachokifanya kwa sasa ni kuhakikisha wanavuna pointi tisa katika michezo yao mitatu iliyobaki kisha baada ya hapo ndipo watajua hatma ya kikosi hicho msimu huu.

Kanuni ziko hivi:

Timu mbili zitakazomaliza chini kwenye msimamo, yaani nafasi ya 16 na 15 zitashuka moja kwa moja, lakini timu zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitacheza play off zenyewe kutafuta timu moja itakayocheza na mshindi wa play off wa Championship itakayoshinda itacheza Ligi Kuu, itakayopoteza itacheza Championship msimu ujao.

Chanzo: Mwanaspoti