Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukuta Yanga wamshitua Gamondi

Miguel Gamondi Xx Dickson Job Ukuta Yanga wamshitua Gamondi

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Yanga ikiendelea kujifua kwaajili ya mechi ijayo ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad mechi itakayopigwa Novemba 24, mwaka huu nchini Algeria, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amekitathimini kikosi chake na kugundua kuna kitu kinakosekana hususani kwenye eneo la beki wa kati.

Katika mazoezi hayo yanayoendelea uwanja wa Avic Town, Kigamboni, Yanga inawakosa nyota wake 10, Aboutwalib Msheri, Djigui Diarra, Nickson Kibabage, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Stephane Aziz Ki walio katika timu zao za Taifa.

Hali hiyo inamfanya kocha Gamondi kutengeneza timu yake bila ya mastaa hao ambao wengi wao ni wa kikosi cha kwanza ila amekomaa na waliopo huku akisema kazi kubwa anaipata inapokuja muda wa kujenga ukuta.

Katika eneo hilo kwenye beki wa kati ndipo kuna changamoto zaidi kwani mabeki Job, Mwamnyeto na Bacca ambao wamekuwa wakicheza eneo hilo kwa muda mrefu, wapo timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' huku kambini akiwepo beki mmoja tu wa timu kubwa, Mganda Gift Fred sambamba na bwana mdogo Shaibu Mtita kutoka timu ya vijana (U-20).

Eneo lingine ni lile la kipa ambapo hakuna hata mmoja wa timu kubwa kati ya wale watatu aliyepo kambini Avic Town, kwani Diarra yupo timu ya taifa ya Mali huku Msheri wakiwa na taifa Stars.

Wakati Gamondi akiwa anawaza yote hayo, wapinzani wao CR Belouizdad ni wachezaji watatu tu watakosekana ambao ni kiungo mkabaji, Mamadou Samake (Mali)

Algeria ilikuwa na mchezo wa kwanza jana dhidi ya Somalia (Nyumbani) na itakuwa na ugenini dhidi ya Msumbiji mchezo utakaochezwa Novemba 19.

"Wachezaji wengi wapo timu zao za taifa kipindi ambacho tunajiandaa na mechi ya CAF, tunaendelea kutengeneza timu yetu kupitia wachezaji waliopo kwani tuna mchezaji kwenye kila eneo lakini kwa upande wa beki wa kati na kipa kuna changamoto kidogo kutokana na uchache wa watu kwenye maeneo hayo," alisema Gamondi na kuongeza;

"Makipa wote hawapo, na mabeki wa kati watatu hawapo, hiyo ni changamoto lakini tunatarajia wataungana na sisi siku chache kabla ya mechi."

Hata hivyo ratiba za mastaa hao zinaonekana kubana kwani kwa Mali anayoichezea Diarra, itakuwa na mechi leo dhidi ya Chad lakini Novemba 20, mwaka huu, itakuwa na mechi nyingine dhidi ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati mchezo utakaopigwa nchini Mali.

Kwa upande wa Msheri, Metacha, Job, Mwamnyeto, Bacca, Mudathiri na mzize walio Taifa Stars, watacheza kesho na Niger nchini Morocco na baada ya hapo watarejea nchini ambapo watacheza na Morocco Novemba 21, kwa Mkapa.

Hivyo hivyo kwa Aucho aliye timu ya taifa ya Uganda na Aziz Ki aliye Burkina Faso, mechi zao za mwisho zitapigwa Novemba 21 mwaka huu, siku tatu kabla ya Yanga kuivaa Belouizdad ugenini.

Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alisema timu yao imewasiliana na mashirikisho walipo wachezaji wao na kuwaomba kuwahi kurudi kambini jambo ambalo linafanyiwa kazi.

"Tuna mchezo mgumu Novemba 24 ugenini lakini kwa sasa wachezaji wetu wengi wapo kwenye timu zao za taifa, tumewasiliana na mashirikisho wanayotoka tukiwaomba ili waweze kushiriki walau mazoezi ya pamoja kwa siku mbili-tatu kabla ya mechi," alisema Arafat.

Hata hivyo Mwananchi linajua, Yanga isafiri kwa makundi kwenda nchini Algeria kwaajili ya mechi hiyo, ambapo wataanza wale walioko kambini hadi sasa kisha watafuata wale walio kwenye timu zao za taifa ambapo wengi wao watapitiliza moja kwa moja Algeria.

Chanzo: Mwanaspoti