Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukiwataka hawa usiwe bahili

Wanne Wakamatwa Kwa Kutundikwa Kwa Sanamu Ya Vinicius Jr Ukiwataka hawa usiwe bahili

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Chelsea bado inahitaji saini ya straika, Victor Osimhen aende kukipiga Stamford Bridge kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa Januari.

Hata hivyo, kinachoelezwa ni kwamba kwenye usajili huo, ili matajiri hao wa London wamsajili Osimhen, Chelsea italazimika kulipa Pauni 130 milioni.

Lakini, kwa mujibu wa Transfermarkt, bei ya Osimhen sokoni ni Euro 120 milioni, hivyo ukilipa zaidi ya kiasi hicho, umepigwa.

Baada ya kutambua bei halisi ya Osimhen, Mwanaspoti linakutelea wachezaji mahiri ambao bei zao zipo juu sokoni.

Erling Haaland – Man City, Euro 180milioni

Straika wa Manchester City, Erling Haaland makali yake ya uwanjani hayana mashaka kabisa na hilo linamfanya kila kocha au shabiki wa soka duniani kutamani kuwa na mchezaji huyo kwenye kikosi chake.

Umahiri wake kwenye kufunga mabao ndicho kitu kinachompa thamani kubwa Haaland, ambapo kwa mujibu wa Transfermarkt, ukihitaji saini ya mchezaji huyo huko sokoni basi itakubidi kulipa Euro 180 milioni.

Kylian Mbappe – PSG, Euro 180milioni

Lisemwalo ni kwamba mshambuliaji matata wa Ufaransa, Kylian Mbappe atakuwa huru mwishoni mwa msimu huu na hivyo huenda akaondoka kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain bure kabisa. Hata hivyo, Transfermarkt inataja thamani ya Mbappe huko sokoni, kwamba ni Euro 180 milioni ndiyo thamani halisi ya mkali huyo wa Les Bleus.

Jude Bellingham – Real Madrid, Euro 150milioni

Real Madrid ililipa pesa nyingi sana kuinasa saini ya kiungo, Jude Bellingham kutoka Borussia Dortmund kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Tangu alipotua Bernabeu, Bellingham ameonyesha ubora mkubwa unaofanya thamani yake izidi kupanda, ambapo kwa sasa ukimhitaji staa huyo wa England, kwa mujibu wa Transfermarkt, bei yake sokoni ni Euro 150 milioni.

Vinicius Junior – Real Madrid, Euro 150milioni

Winga wa Kibrazili, Vinicius Junior kwa muda mrefu amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Real Madrid tangu alipojiunga na miamba hiyo. Panga pangua amekuwa chaguo la kwanza la Kocha Carlo Ancelotti kwenye kikosi hicho na hilo linamfanya thamani yake sokoni kupanda, ambapo kwa sasa ukihitaji saini ya mchezaji huyo kwa mujibu wa Transfermarkt, utalazimika kulipa Euro 150 milioni.

Bukayo Saka – Arsenal, Euro 120milioni

Kocha Mikel Arteta kijasho huwa kinamtoka anapokosa huduma ya mkali wake matata kabisa, Bukayo Saka kwenye kikosi chake. Winga huyo Mwingereza amekuwa na kiwango bora sana ndani ya uwanja na hivyo kujiweka kwenye mazingira bora kabisa ya kuweka bei yake juu kwenye soko la mpira wa miguu. Kwa mujibu wa Transfermarkt, Saka bei yake inayoelezwa sokoni ni Euro 120 milioni. Toa mkwanja umchukue.

Jamal Musiala – Bayern Munich, Euro 110milioni

Bayern Munich inatamba kwa kuwa na huduma ya Jamal Musiala kwenye kikosi kutokana na mchezaji huyo kucheza soka la kibabe sana huko kwenye Bundesliga na michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kiwango bora uwanjani na umri wake mdogo vinamfanya Musiala kuwa miongoni mwa wachezaji wenye thamani kubwa sokoni, ambapo kwa mujibu wa Transfermarkt, ukihitaji saini yake ni Euro 110 milioni.

Phil Foden – Man City, Euro 110milioni

Kocha Pep Guardiola amekuwa na wakati mzuri kwenye kikosi chake cha Manchester City kutokana na kuwa na mastaa wengi wenye huduma bora kabisa uwanjani akiwamo Mwingereza, Phil Foden. Mchango anaoutoa staa huyo huko Etihad hauna shaka na hilo linamfanya thamani yake sokoni kuwa vizuri pia, ambapo kwa mujibu wa Transfermarkt, Foden ukihitaji aje kwako lipa Euro 110 milioni.

Harry Kane – Bayern Munich, Euro 110milioni

Umri wake ni miaka 30, lakini kile anachokifanya kwenye kikosi cha Bayern Munich alikojiunga kdirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi akitokea Tottenham Hotspur inafanya thamani yake kuwa juu licha ya kuwa na umri mkubwa. Bayern ililipa pesa nyingi kumpata na kwa mujibu wa Transfermarkt, ukimhitaji straika huyo wa mabao kwa sasa basi itakulazimu kulipa Euro 110 milioni.

Pedri – Barcelona, Euro 100milioni

Kiungo wa Barcelona, Pedri ni miongoni mwa mastaa matata kabisa huko Nou Camp na ubora wake wa uwanjani umeifanya thamani yake kuzidi kupanda ambapo kwa mujibu wa Transfermarkt, staa huyo ukitaka saini yake itakulazimu kulipa Euro 100 milioni. Kocha Xavi amekuwa akifurahishwa na huduma ya mchezaji wake huyo ambaye mchango wake ndani ya uwanja umekuwa mkubwa.

Lautaro Martinez – Inter, Euro 100milioni

Straika wa Kiargentina, Lautaro Martinez ni mmoja kati ya wakali matata kabisa wanaocheza soka la kiwango cha juu huko Ulaya. Mkali huyo anacheza soka lake kwenye kikosi cha Inter Milan, huku ubora wake ukipandisha thamani yake sokoni kwa mujibu wa Transfermarkt. Kwa maana hiyo, ukimtaka mkali huyo itakubidi kulipa Euro 100 milioni. Wachezaji wengine wenye thamani kama hiyo ni Declan Rice wa Arsenal, Rodrygo wa Real Madrid na Federico Valverde.

Chanzo: Mwanaspoti