Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukata waitibulia Amani Queens

Aman Queens Ukata waitibulia Amani Queens

Tue, 2 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Amani Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya wanawake (WPL) inakabiliwa na ukata jambo ambalo linaifelisha kupata matokeo mazuri.

Matukio hayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kwani Desemba 20 mwaka huu ilikuwa na mchezo wa ligi dhidi ya Fountain Gate Princess na uliahirishwa sababu ikiwa ni suala la kifedha.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo, Morice Katembo alisema kesho wana mechi dhidi ya JKT kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi lakini mpaka sasa wako Dar es Salaam na hawajui wanaendaje.

Katembo alisema changamoto nyingine ni kuwa asilimia 40 ya wachezaji wako kambini na 60 wako majumbani mwao wakikosa nauli ya kujiunga na wenzao kambini.

Kocha huyo anawaomba wadau na mashabiki kuwaunga mkono ili kuikoa timu hiyo kwa kuwa bado haina wadhamini.

"Mfano mchezo uliopita tuliocheza na Yanga, tulifanya mazoezi wiki moja na baada ya hapo tukasafiri na kuja Dar es Salaam kwa hiyo nikasema siwezi kucheza kama wenzangu kwa sababu wana timu nzuri na uwekezaji, nikapambana na mbinu lakini bado haikuzaa matunda," alisema Katembo na kuongeza;

"Naweza kusema sababu ya hata timu kutocheza vizuri inachangiwa na tatizo la ukata kwa sababu mkikwama, wachezaji wanaweza hata kukata tamaa lakini tunapambana tuwaombe wadau watusaidie, timu bado ni changa."

Tayari Amani imecheza mchezo mmoja na Yanga Princess iliofungwa mabao 6-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi na kesho inatarajia kukutana na JKT nyumbani.

Chanzo: Mwanaspoti