Timu ya Mkwawa Queens ya mkoani hapa imekwama kusafiri kwenda mkoani Lindi kwa ajili ya michezo wake dhidi ya amani Queen ambayo ulitarajiwa kuchezwa leo katika uwanja wa Ilulu.
Hii ni mara ya pili kwa timu hiyo kukwama kwenye safari zake, ambapo awali ikiwa Dar es Salaam ilishindwa kusafiri kurudi nyumbani kwa kukosa nauli hadi kujikuta ikishikiliwa katika nyumba ya wageni walipofikia kwa deni la Sh810, 000 kabla ya wadau akiwamo Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego kuisaidia.
Akizungumza leo April 5, Ofisa habari wa Timu hiyo Francis Godwine amesema kuwa hadi sasa timu yao bado haijaondoka kuelekea mkoani Lindi kwa ajili ya michezo huo kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wao hali ambayo imelazimika kusubiri hadi mambo yatakapo kaa sawa ili kucheza michezo huo.
"Maandalizi ya kwenda kucheza mchezo ambao tulitakiwa kucheza leo sio mazuri kwa sababu tulitakiwa kuondoka jumapili April 2, kwenda Lindi kucheza na Amani Queens ila hatujasafiri" amesema Godwine
Godwine ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo hadi sasa wameiandika barua shirikisho la soka nchini (TFF) kwa ajili ya kuwajulisha juu ya Timu ya kukwama kusafiri na kuomba upangiwe tarehe nyingine wakati uongozi uliendelea kusaka nauli.
" Tunachokifanya kwa sasa ni kuangalia kitu gani tunaweza kufanya ili kutatua changamoto hii na tukikamilisha tutawajulisha TFF kwa ajili ya kutupangia mchezo huo ili tuweze kuendelea na ratiba ya mchezo huo." amesema
Ofisa huyo ameeleza kuwa sababu ya kukwama kwa timu yao ni ukata wa kifedha na kwamba ili timu iweze kusafiri bila tatizo wanahitaji Sh10 milioni.
Hata hivyo amesema kuwa kwasasa wanaendelea na jitihada mbalimbali za kuangalia namna nzuri ya kuweza kuwapata wadau ili waweze kuwasaidia kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.