WAKATI Ligi Kuu Bara ikisimama kwa muda kupisha kalenda ya michuano ya kimataifa, umeshuhudiwa ukame wa mabao kwani kati ya mechi zilizochezwa hakuna iliyomalizika kwa zaidi ya mabao mawili.
Katika michezo iliyochezwa ni Polisi Tanzania iliyoweka rekodi ya kufunga idadi ya mabao mawili kila mechi ikiizabua KMC 2-0 kisha kuichakaza Azam 2-1, huku Namungo wakishinda mechi moja kwa mabo 2-0 dhidi ya Geita Gold.
Timu nyingine ziliishia ushindi wa bao moja, ilhali mchezo wa Mbeya City na Mbeya Kwanza ukiwa ndio uliozalisha mabao mengi - manne wakati zikitoshana nguvu kwa sare ya 2-2.
Kocha wa Mbeya City, Mathias Lule alisema bado kunahitajika mbinu za ziada kuhakikisha wanapata idadi kubwa ya mabao kwani katika mechi zilizopita straika wake walikosa mabao mengi.
“Ni kweli upungufu upo kwenye ufungaji mabao na ukifuatilia mchezo wetu hasa dhidi ya Prisons tulikosa nafasi nyingi, lazima kuendelea kuisuka safu ya ushambuliaji,” alisema Lule.
Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Rashid Chama alisema ipo presha kwa washambuliaji, “tuwape muda huko mbeleni kuna mabao mengi yanakuja.”