Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukame wa Mabao Ligi Kuu, Mayele atatetema leo?

Mayele Kadi Fiston Mayele

Sun, 12 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Straika wa Yanga, Fiston Mayele anatarajiwa kuiongoza Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold itakayopigwa jioni ya leo Azam Complex, huku akikabiliwa na mtihani wa kufuta ukame wa mabao ili kujisafishia njia za kuwania tuzo ya mfungaji bora kwa msimu huu.

Mayele ndiye kinara wa mabao kwa sasa wa ligi hiyo akiwa amefunga 15, lakini mara ya mwisho kufunga kwenye michezo ya Ligi Kuu ni Januari 16 wakati akiizamisha Ihefu katika pambano la marudiano lililopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Bao alilofunga kwenye mchezo huo, lilikuwa la tano kutupia kwenye duru la pili na la 15 kwa mechi zote za msimu huu katika ligi hiyo kisha kucheza mechi tatu mfululizo ambazo timu hiyo ilishinda bila kutetema, kitu ambacho mashabiki wanasubiri kuona jioni ya leo kama atahitimisha ukame huo.

Mayele aliyefunga jumla ya mabao tisa katika michuano ya CAF kwa msimu huu, yakiwamo saba ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na mawili kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, msimu uliopita alikosa tuzo ya mfungaji bora Bara akidiziwa na George Mpole aliyekuwa Geita Gold kwa tofauti na bao moja tu, Mkongomani huyo akiwa na 16 na Mpole 17.

Mchezaji anayemfukuzia kwa sasa ni Moses Phiri na Saido Ntibazonkiza wenye mabao 10 kila mmoja na jana walikuwa na nafasi ya kuongeza idadi hiyo wakati timu yao iliposhuka uwanjani kuvaana na Mtibwa Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyiopigwa Uwanja wa Manungu.

Mara ya mwisho kwa Phiri kufunga kwenye ligi ilikuwa Desemba 3 mwaka jana wakati Simba ikiiadhibu Coastal Union kwa mabao 3-0 kisha akaumia na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, hivyo kurejea kwake kwa sasa kunaweza kumpa presha zaidi Mayele kama ataendeleza moto wake.

Kutokana na hali hiyo na idadi ya mechi zilisalia kwa sasa, Mayele ana kazi kubwa ya kurejesha moto wake wa kufunga ili kuvunja rekodi ya msimu uliopita aliomaliza na mabao 16, ikiwa na maana kwa sasa amesaliwa na bao moja tu kuifikia, lakini kiu yake ya kumaliza kama mfungaji bora wa msimu.

Presha kwa straika hiyo haisababishwi na Phiri tu, lakini hata Saido, Mbrazili Bruno Gomes wa Singida Big Stars na John Bocco wa Simba nao kama wataendelea kutupia itazidi kumweka katika wakati mgumu nyota huyo wa Yanga anayeichezea timu hiyo kwa msimu wa pili mfululizo sasa.

Mayele alieleza mapema kwamba amekuja nchini kwa kazi moja ya kufunga na huwa hana presha ya kuangalia wachezaji wa timu nyingine wanafanya nini, ila anapambana kuifungia timu mabao kwa lengo la kuipa matokeo mazuri ili kutetea ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo.

Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 62 baada ya mechi 23 na leo kuanzia saa 12:15 jioni inashuka uwanjani, ikiwa pia imetinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na ikitanguliza mguu moja kwenye robo fainali kutoka Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika.

Katikati ya wiki hii mara baada ya Yanga kuichapa Real Bamako ya Mali, Kocha Nasreddine Nabi alikaririwa akieleza kutofurahishwa na hali ya uchoyo alionayo Mayele uwanjani ambao ulichangia kuinyima timu mabao zaidi kama angekuwa akiwachia wenzake waliokuwa kwenye nafasi nzuri.

Katika mechi hiyo Mayele alifunga bao la kwanza kabla ya Jesus Moloko kuongeza la pili, lakini Nabi alisema Yanga ilistahili kupata ushindi mnono zaidi kwa nafasi zilizopotezwa na nyota wake akiwamo Mayele ambaye amekuwa na kiu ya kufunga kiasi cha kuwa mbinafsi kwa wenzake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live