Serikali inaendelea na taratibu mbalimbali za Ujenzi wa Viwanja vya Mazoezi na Kupumzika Wananchi (Recreational and Sports Centres) katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ambapo mikataba ya ujenzi imesainiwa kwa maeneo hayo.
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Pindi chana amesema tayari Mkandarasi amekabidhiwa maeneo na ameanza hatua za awali za ujenzi (mobilization stage), na ujenzi wa maeneo hayo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 54.6 na ujenzi utafanyika katika kipindi cha miezi 36.
Amesema. “Serikali pia inaendelea na taratibu za ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo katika Mkoa wa Dodoma katika eneo la Nzuguni ambapo zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa uwanja huo imetangazwa.”
Aidha ameongeza kuwa, “Sambamba na ujenzi wa Uwanja wa Michezo Dodoma, pia Serikali inajiandaa kujenga Uwanja kama huo katika jiji la Arusha kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya AFCON 2027 endapo nchi za Afrika Mashariki zitashinda zabuni ya kuandaa michezo hiyo.”