Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ujenzi uwanja mpya Arusha mwezi Machi

Uwanja Arusha 1.jpeg Ujenzi uwanja mpya Arusha mwezi Machi

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay amesema waandaaji wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027; Tanzania, Kenya na Uganda kila nchi itapaswa kuwa na viwanja vitatu na kwamba Tanzania tayari inavyo viwili Benjamin Mkapa na Amaan Zanzibar hivyo umebaki uwanja mmoja ambao utajengwa Arusha.

Mayay amesema mambo ya tathimini yalishakamilika na sasa wako katika hatua ya mapatano, na kwamba ujenzi wa uwanja huo mpya wenye uwezo wa kubeba watu 30,000 utaanza kujengwa mwezi ujao.

“Tuko kwenye hatua za mwisho na mkandarasi wa ujenzi wa uwanja wa Arusha, mpaka Desemba 2025 CAF watakuja kuangalia tayari utakuwa umekamilika.”

NYASI BANDIA AMAAN Mayay amesema nyasi bandia za Uwanja wa Amaan zitaondolewa na kupandwa nyasi asilia ili ukidhi vigezo vya michuano hiyo ya kimataifa.

“Uwanja wa Amaan ushakamilika kwa asilimia 100. Kilichobaki ni kubadili tu zile nyasi bandia na kupanda nyasi asilia, jambo ambalo linachukua muda mfupi tu wa kuanzia sita,” amesema na kuongeza: “Watu wengi wanazungumzia kuhusu viwanja vya mechi tu. Timu zitakuwa na viwanja vya wazi kwa ajili ya mazoezi ambavyo zinaweza kufanya mazoezi muda wowote, timu inakabidhiwa uwanja wake wa mazoezi na inaweza kufanya mazoezi muda wowote itakaotaka iwe mchana au usiku.

“Kwa Zanzibar vipo na vinaendelea kuandaliwa. Arusha maeneo ya wazi yapo. Kwa Dar es Salaam kuna Gymkhana, JK Park na hata Leaders Club patatengenezwa kukidhi viwango vinavyohitajika ikiwa ni pamoja na kuwekewa taa.”

Mayay amesema hayo leo Februari 14, 2024 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Ltd, wenye mada isemayo "Tanzania imejifunza nini kupitia AFCON 2023, ikijiandaa 2027?"

Chanzo: Mwanaspoti