Nimepata stori moja ya kusisimua inayomhusu kocha wa Coastal Union ya Tanga, David Ouma ambaye ameiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Wakati alipojiunga nayo kuchukua mikoba ya Mwinyi Zahera aliyekuwa ametimuliwa, uongozi wa Coastal Union ulimpa Ouma jukumu la kuhakikisha timu hiyo inasalia Ligi Kuu.
Lakini kwa mshangao kocha huyo aliwajibu kuwa yeye atafanya zaidi kwa kuhakikisha timu inamalizandani ya nafasi nne za juu na ikishindikana atawaruhusu viongozi wa Coastal Union wamuwajibishe.
Ni jambo lililoushangaza kimtindo uongozi wa Coastal Union kwa vile kipindi hicho timu haikuwa na mwenendo mzuri na haikuonyesha kama itamaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Baada ya kusaini mkataba, alichokifanya Ouma ni kukaa na wachezaji wake na kuwapa agizo la kile anachokihitaji na kuwapiga mkwara kwamba kwa yeyote ambaye ataona dalili za kutaka kumkwamisha atamuweka pembeni.
Ni ujumbe uliowaingia vyema wachezaji wa Coastal Union na wakaufanyia kazi kwa vitendo, timu ikawa na muendelezo wa kufanya vizuri ambao ulizaa matunda mwishoni mwa msimu.
Alichokifanya Ouma ni zao la kuamini katika kile alichonacho kichwani akiamini kingeweza kuibadilisha Coastal Union na kuifanya kuwa miongoni mwa timu tishio kwenye Ligi Kuu Bara.
Hakuogopa changamoto ya ugeni wa timu wala ligi na badala yake aliamini katika jitihada za wachezaji katika kufanyia kazi kile ambacho benchi la ufundi limekiandaa kwa ajili ya michezo tofauti ya ligi.
Tunahitaji kuwa na ligi yenye walimu wengi wa aina ya Ouma ambao wanaamini katika kile wanachokifanya na wanaweza kuwa na ujasiri wa kuweka malengo ya juu zaidi ya yale ambayo wamewekewa na viongozi wao.
Ni lazima tumpe kongole.