Timu ya Zanzibar imeanza vibaya kwenye michuano ya CECAFA kwa wanawake chini ya miaka 18 baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda inayoendelea katika Uwanja wa Azam Complex Chamanzi.
Kwa Zanzibar unakuwa mchezo wao wa kwanza na kupoteza ambapo kwa timu ya Uganda tayari wameshinda michezo yote miwili ambapo juzi dhidi ya Ethiopia kwa bao 1-0 lililofungwa na Allen Nassazi aliyetokea benchi.
Huu unakuwa mwanzo mzuri kwa Uganda baada ya kushinda michezo miwili mfululizo.
Kikosi cha Zanzibar kilichoanza leo chini ya Kocha Mkuu, Abdulmutik Haji alianza na Kipa Aisha Said mabeki Amina Ramadhani na Wigo Magoma, Rahma Nassor, Rukia Laizar, Agness Millanzi, Mwamvita Muba, Hawa Juma, Saada Said, Fatma Bakar na Anna James huku benchi akiwa Fatma Juma, Thuwaiba Mvuma, Farida Kombo, Jacqueline Solomoni, Salha Ali, Naima Nasib na Zainab Nassad.
Kwa upande wa Uganda chini ya Kocha Mkuu, Khalifa Ayub alianza na kipa Sharon Kaidu, Desire Katisi, Brenda Munyana, Agnes Nabukenya, Shamusa Najjuma, Krusum Namutebi, Sharifah Nakimera, Patricia Nanyanzi, Phionah Nabulime, Kamiyati Naigaga na Patience Nabulobi.
Wengine waliokuwa benchi ni Cecilia Kamuli, Charity Katusiime, Hadijah Namakula, Rebecca Nandhego, Immaculate Odalu, Monica Nanono, Allen Nassazi, Patricia Nayiga na Yuko Bridget.
Kipindi cha kwanza kiliisha kwa timu zote mbili kutoona lango la mwenzie huku Uganda wakionekana kulisogelea lango la Zanzibar lakini walishindwa namna ya kumalizika.
Kipindi cha pili Zanzibar walikosa utulivu na kuwapa nafasi washambuliaji wa Uganda kushambulia eneo lao ambapo dakika ya 65 Patricia Nanyanzi anawatanguliza Uganda kwa shuti kali lililoingia moja kwa moja kambani dakika ya 67 Agnes Nabukenya anaongeza bao la pili huku bao la tatu likifungwa na Phionah Nabulime dakika ya 84.