Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ufundi wa Maxi, Pacome huu hapa...

Pacome X Nzengeli Staa Ufundi wa Maxi, Pacome huu hapa...

Sun, 10 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi licha ya kutoa nafasi ya kucheza kwa kila mchezaji, lakini kuna mastaa wanatikisa kulingana na kile wanachofanya uwanjani akiwamo Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI, na hilo limewaibua wakongwe kutoa neno wakifichua kinachowabeba.

Yanga imecheza mechi sita za mashindano zikiwamo mbili za Ngao ya Jamii dhidi ya Azam na Simba, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asas ya Djibouti zote ikishinda na kutinga raundi ya pili na Ligi Kuu ikiifunga KMC na JKT Tanzania kila moja mabao 5-0.

Kupitia mechi hizo Gamondi aliwatumia wachezaji tofauti ndani ya kikosi, lakini majina kadhaa yalijirudia kwa moto uleule akiwamo Maxi, Yao, Aziz KI na Pacome, japo kwa mechi hizo sita sambamba na ile ya kirafiki ya kimataifa ilipoifunga Kaizers Chiefs ya Afrika Kusini kwa bao 1-0, timu nzima inacheza vizuri na kuwapa raha mashabiki.

Baadhi ya mastaa wa zamani wa soka nchini waliokiangalia kikosi hicho kwenye mechi hizo wamefichua kinachowabeba nyota hao akiwamo Willy Mtendemema aliyesema mashabiki wamejenga imani na Max, Pacome na Ki kulingana na kile walichokifanya uwanjani, akiwataka mastaa hao kuendelea kujituma kulinda heshima wanayopewa.

“Ni wachezaji wenye maarifa makubwa uwanjani wanaweza wakakupa matokeo kwenye nyakati zote. Nimpongeze kocha Gamondi anavyojaribu kumpa nafasi kila mchezaji, hiyo inafanya kila mtu ajitume na awe na ushindani zaidi wa kutetea namba, ingawa bado ni mapena ndio kwanza ligi imeanza,” alisema beki huyo wa kati aliyewika pia na AICC Arusha kabla ya kutua Yanga miaka ya 1990.

Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa ambaye sasa ni kocha wa timu ya Taifa ya Ufukweni alisema: “Ukiona wachezaji wapo midomoni mwa mashabiki wana kitu wanachofanya cha ziada. Pacome, Max na Ki wana uwezo mkubwa wa kuamua matokeo, ingawa Yanga kwa ujumla inacheza vizuri bado wana krimu ile waliyomaliza nayo msimu uliopita.”

Rekodi za mechi sita za mashindano, Yanga imefunga mabao 19, huku Aziz KI na Maxi wakiongoza kwa kufunga manne kila mmoja wakifuatiwa na Pacome mwenye mabao mawili kama Clement Mzize, Kennedy Musonda na Hafiz Konkoni.

Wengine waliofunga moja moja ni Dickson Job, Mudathir Yahya na Yao na kuifanya Yanga iongoze msimamo wa Ligi Kuu Bara na kutinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa ikijiandaa kumenyana na El Merrikh ya Sudan.

Hata hivyo Yanga ilipoteza Ngao ya Jamii kwa mikwaju ya penalti 3-1 mbele ya Simba katika fainali iliyopigwa jijini Tanga.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: