Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchawi wa Aziz Ki, Pacome huu hapa

Aziz KI X Pacome Pacome na Aziz Ki

Sun, 10 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga kimesharejea jijini Dar es Salaam kutoka Lindi ilipoenda kupata ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Namungo na sasa inajindaa na mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa kesho dhidi ya Ihefu, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi akifichua siri zinazowabeba Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua na Mudathir Yahya.

Yanga itaikaribisha Ihefu kwenye Uwanja wa Azam Complex kesho ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa duru la kwanza ugenini kwa mabao 2-1. kikiwa ndicho kipigo pekee ilichopata timu hiyo hadi sasa katika mechi 17 ilizocheza, lakini ikitoka kucheza mechi saba mfululizo baada ya mapumziko mafupi ya ligi hiyo na kufanya vyema.

Tangu ligi iliporejea tena baada yab kusimama Desemba 23 mwaka jana kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, Yanga imeshinda mechi sita na kutoka sare moja na Gamondi amefichua uchawi unawaobeba nyota wa kikosi hicho akisema ni utimamu wa wachezaji hao akimpongeza kocha wa viungo, Taibi Lagrouni kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kina Muda, Aziz Ki na wenzake kutochoka uwanjani.

Rekodi zinaonyesha tangu Desemba 23, mwaka jana Yanga imeshinda mechi sita na sare moja katika Ligi Kuu dhidi ya Tabora United (1-0), Kagera Sugar (0-0), Dodoma Jiji (1-0), Mashujaa (2-1), Tanzania Prisons (2-1), KMC (3-0) na juzi ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Namungo, huku timu ikionekana kuupiga mwingi hasa kwenye kipindi cha pili.

Kocha Gamondi, aliliambia Mwanaspoti siri ya timu hiyo kufanya vizuri kwenye mechi hizo, huku alifafanua licha ya ushindi mara sita na suluhu moja katika michezo saba iliyopita, bado wana safari ndefu kutetea taji lao huku akikiri mechi 10 ni nyingi kujihakikishia ubingwa sasa, lakini akimwagia sifa msaidizi wake, Taibi Lagrouni.

"Sifa zimwendee kocha wa viungo kutokutofautisha utimamu kwa wachezaji wanaocheza mara kwa mara na wasio cheza jana (juzi) ni ubora wake (Lagrouni), tuliwakosa wachezaji sita lakini waliopo wamefanya kazi nzuri na bora kwa kutupa pointi tatu muhimu}" alisema Gamondi na kuongeza;

"Pia wachezaji wamekuwa katika nafasi nzuri kila mmoja kuhitaji namba ya kucheza na wakipewa nafasi wanafanya vizuri hilo linanipa nguvu na kuniaminisha lolote linawezezekana kabla ya msimu kuisha."

Gamondi alisema wana mechi nyingine tatu mfululizo kabla ya ligi kusimama kupisha ratiba za mechi ya kirafiki kwa timnu za taifa, huku akikiri umuhimu wa mechi hizo ambazo amesema anatamani kuona wanapata pointi zote tatu ili kujihakikishia nafasi ya kutetea taji.

"Tumecheza juzi tuna siku mbili za kupumzika kabla ya mchezo mwingine naupongeza uongozi kwa kufanikisha suala la ndege kuja Lindi na naamini kurudi pia tutarudi kwa haraka kuiwahi Ihefu. Utimamu wa wachezaji wangu utasaidia kuendeleza ushindani najivunia kikosi nilichonacho naamini kila mchezaji anauhitaji wa mafanikio hili litasaidia kupata mafanikio," alisema.

MUDA, PACOME, AZIZ Katika mechi hizo saba ilizocheza Yanga, ikishinda sita na suluhu moja timu hiyo imefunga jumla ya mabao 12 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara moja tu na Mudathir Yahya, Aziz KI na Pacome wakioonyesha ndio vinara wa kutupia kambani.

Muda ndiye baba lao kwa kukwamisha mabao matano wavuni katika mechi hizo, huku Pacomne, Stephane Aziz Ki na Clement Mzize kila mmoja akifunga mabao mawili. Mbali na nyota hao waliozalishamabao 11, kati ya 12 ambalo hilo moja liliwekwa kimiani na Maxi Nzengeli aliyefunga dhidi ya Mashujaa wakati Yanga ikiibuka na Mashujaa wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kurejea kileleni ikiing'oa Azam iliyokalia kiti cha uongozi kwa muda mrefu ikifikisha pointi 46 kupitia mechi 17, tatu pungufu na ilizonazo Wanalambalamba yenye alama 44, japo inaongoza kwa mabao ya kufunga ikiwa na 45, wakati Yanga ina 42 hadi sasa na Simba ikifuatia nyuma yao na jana jioni ilikuwa uwanjani.

Chanzo: Mwanaspoti