Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchafu wa Zahera si usafi wa Yanga

Zaheramwinyi Mwinyi Zahera

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita nilimsikia Ofisa Habari wa Yanga, Ally Shaban Kamwe akirudiarudia kauli kuwa; ‘Namheshimu Zahera’, wakati akijibu hoja alizoibua kocha huyo Mcongo katika mahojiano na Kituo cha Redio cha EFM.

Ni kauli inayotumiwa sana na watu kutaka kuonyesha kuwa hoja fulani aliyoisema si sahihi, hivyo hataki kumwambia si sahihi kwa kuwa anamheshimu, ila maelezo yanayofuata huwa ni kuonyesha kilichosemwa si sahihi.

Lakini maelezo ya Kamwe hayakufuatiwa na maelezo sahihi dhidi ya yale aliyozungumzia Zahera kuhusu tabia za viongozi wa Yanga, hasa Rais na mwenendo wa wachezaji ambao alituhumu kuwa baadhi wamewakalia mabegani makocha hivyo wanafanya watakavyo.

Badala yake, Kamwe aliweka mlolongo wa maswali kuhusu Zahera, akimtaka aeleze majukumu yake kama Mkuu wa Programu za Vijana aliyatekeleza vipi nia yake ya kusimamia timu ya wanawake ameyaacha vipi.

Ni kweli inawezekana hakufanya vizuri katika maeneo hayo na pengine kuna tatizo kubwa lililoifanya klabu isimuongezee mkataba. Lakini hayo hayafanyi hoja alizozitoa zisiwe na nguvu na kwa kuwa hazijajibiwa, zinaendelea kuwa na nguvu hadi hapo zitakapotolewa ufafanuzi na mamlaka. Kuna vitu vinaonekana bayana kama vile vya Rais wa Yanga, Injini Hersi Said kutaka kuonekana yuko karibu sana na timu pamoja na wachezaji. Mara kadhaa picha zimetumwa akiwa pamoja na wachezaji, wakati mwingine akishiriki mazoezi au kupiga danadana, huku picha nyingine zikimuonyesha amepozi na wachezaji nyota.

Ziko video zinazoonyesha akizungumza na wachezaji ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo. Hii ni kuweka weledi kando na kudhani kauli ya Rais ndio inayoweza kuamsha ari ya wachezaji.

Kama hizo video huchukuliwa wakati wa mapumziko, basi ni hatari kwa maendeleo ya timu na kwa kiasi fulani vitendo hivyo hupunguza ufanisi wa kocha na hatimaye timu kwa ujumla. Kila kitu kina mipaka yake.

Kwanza, siamini kama Zahera alijipeleka EFM. Ni wazi kuwa alialikwa kwenda kuzungumzia masuala mbalimbali kwa jicho la kiufundi kutokana na kazi yake.Hivyo kumchukulia kama mtu aliyeitisha mkutano na waandishi kutokana na hasira zake dhidi ya Yanga baada ya mkataba wake kusitishwa, ni makosa.

Ni wazi hakuhojiwa kuhusu Yanga pekee, bali kwa sababu masuala ya klabu hiyo hayawezi kuwa madogo ndio maana mahojiano yote yakaonekana kuwa yaliilenga Yanga.

Lakini ukiangalia aliyoyazungumzia, ni ujumbe gani unatumwa kwa wachezaji kutokana na picha hizo za Rais na baadhi wachezaji? Ni picha gani benchi la ufundi, wachezaji wengine au umma unaofuatilia soka unaipata? Ni dhahiri picha inayopokelewa ni ile inayotafsiriwa kuwa benchi la ufundi halina nguvu zozote kwa timu na kuna wachezaji wanaweza kuonyesha kiburi kwa sababu ya ukaribu wao na Rais.

Kuna wakati makocha huzuia hata viongozi kuhudhuria mazoezi, hasa wanapokuwa wanafundisha mbinu. Sijui video hizo zilichukuliwa wakati gani?

Wakati wa mapumziko ni muda ambao kocha ana muda mfupi sana kuzungumza na wachezaji na ndio maana hutumia muda huo kuhamasisha tu, hawezi kuzungumzia marekebisho ya kiufundi kwa kuwa huwa anaendelea nayo nje ya uwanja. Kwanza huwaacha wachezaji wazozane kurekebishana na baadaye humuacha msaidizi wake azungumze na baadhi ya wachezaji mmojammoja na ndipo nafasi yake huja. Hutumia nafasi hiyo kuwaonyesha kuwa wana uwezo wa kushinda na kuwahamasisha.

Mtu mwingine akiingilia muda huo, atavuruga ratiba za walimu za wakati wa mapumziko. Zahera alizungumzia kiufundi na hakuna maelezo mengine yoyote yasiyokuwa ya kiufundi yanayoweza kumfanya Zahera aonekane hana hoja. Kuna wakati Bernard Morrison aliripotiwa kukataa kwenda Kanda ya Ziwa, baadaye zikatumwa picha zinazoonyesha yuko kwenye ndege pamoja na kiongozi akienda kuungana na wachezaji wenzake waliotangulia. Ni picha gani inakwenda kwenye timu? Ni muda mrefu umepita na sasa Morrison amerudi. Haya mambo yanaendelea? Zahera anajua siri, lakini hajaziweka bayana, bali amezungumzia kwa ujumla kuonyesha kuna tatizo.

Pamoja na kwamba huo ni mfano wa muda mrefu, inawezekana chembechembe hizo bado zipo ndio maana Mcongo huyo amesema kuna baadhi ya wachezaji wako juu ya kocha au benchi la ufundi. Pengine ndio maana baadhi hawaonekani wakati wote kwenye mechi licha ya viwango vyao kuwa juu. Kocha analazimika kwenda kulingana na mazingira.

Hoja za Zahera zilitaka majibu na si kumnyooshea kidole na kumwambia ajiangalie yeye kwa kuwa ana uchafu mwingi. Wakati Zahera akiambia ajiangalie kwanza, soka haliisubiri Yanga. Linazidi kusonga mbele na wakati viongozi watakapokaa chini kutafakari, muda utakuwa umekwenda sana.

Ni Mungu tu amemtumia kuonyesha kasoro iliyopo Yanga ili zianze kushughulikiwa. Mwingine angekaa kimya kusubiri mambo yaharibike kabisa ndipo aseme; ‘Nilijua mambo yataharibika’.

Zahera, ambaye aliwahi kuifundisha Yanga wakati klabu ikiwa katika hali mbaya kiuchumi, ana heshima yake kwenye klabu hiyo, hivyo si sahihi kutayarishiwa majibu kama yale aliyosema Kamwe, tena akionyesha kana kwamba anajibiwa na mtu mmoja na si taasisi kwa kuzingatia kauli ya; ‘Mimi namheshimu Zahera’. Yaani ni kama Zahera alimkosea Kamwe na si taasisi inayoitwa Yanga.

Ni muhimu Yanga ikajirekebisha pale paliponyooshewa kidole na Zahera badala ya kufikiria kumchafua kutaifanya klabu na uongozi kuwa safi. Tunahitaji kubadilisha mienendo yetu wakati wa kujibu watu wanaoonyesha kasoro. Hawa wana mapenzi na timu na wanataka kasoro zishughulikiwe mapema kabla hazijaathiri timu. Kuwachafua hawa hakutafanya kasoro zisiwepo. Na kasoro kuendelea kuwepo ni hatari kwa maendeleo ya klabu.

Chanzo: Mwanaspoti