Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ubingwa waipa mzuka Alliance, yapokelewa kishujaa Mwanza

Alliance U15 Ubingwa waipa mzuka Alliance, yapokelewa kishujaa Mwanza

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya Wasichana ya kituo cha Alliance chini ya umri wa miaka 15 (U-15) imepokelewa leo jijini Mwanza baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya shule za msingi na sekondari ya Afrika (African School Championship) kwa upande wa Tanzania yaliyomalizika hivi karibuni jijini Tanga.

Alliance Girls U-15 ilitwaa ubingwa huo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 8-0 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Sahare Sekondari ya Tanga katika Uwanja wa Mnyanjani jijini Tanga.

Timu hiyo itaiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya African School Championship ngazi ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Nairobi, Kenya Desemba mwaka huu,a ambapo bingwa ataiwakilisha Afrika Mashariki kwenye fainali za Afrika zitakazofanyika nchini Misri, mwaka 2024.

Kikosi cha timu hicho chenye wachezaji 20 na benchi la ufundi kimepokelewa leo Alhamisi Novemba 9, 2023 katika Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa na Naibu Meya wa halmashauri ya jiji hilo, Bhiku Kotecha pamoja na viongozi na wadau mbalimbali wa soka mkoani hapa.

Katika mashindano hayo ambayo yamefanyika jijini Dar es Salaam na Tanga kuanzia Novemba 4, mwaka huu, Alliance Girls imecheza mechi tano ikifunga mabao 26 na kuruhusu moja pekee, ambapo imezichapa shule za Tungi (10-0), High View (2-0), Kawe (4-0), Makurumula (2-1) na Sahare (8-0).

Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo baada ya kuwapokea, Naibu Meya wa jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha, amesema ubingwa huo ni heshima kwa jiji hilo huku akiahidi kuwa Serikali itakuwa nao bega kwa bega katika maaandalizi ya kwenda Nairobi na kuwashika mkono.

“Mtakapokwenda Nairobi mtapeperusha bendera ya nchi na mkifanya vizuri lazima Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) atawakumbuka, hivyo mkafanye vizuri muonekane na muendeleze vipaji vyenu. Menejimenti na uongozi mfanye maandalizi mazuri muwe na nidhamu na hawa watoto muwape ushirikiano ili kufanya vizuri,” amesema Kotecha

Mwenyekiti wa kituo cha Alliance, Stephano Nyaitati, amesema uongozi una imani kubwa timu yao itafanya vizuri kwenye hatua zinazofuata za mashindano hayo ili kuiheshimisha Tanzania na kuvitangaza vipaji vinavyozalishwa kituoni hapo.

Nahodha wa timu hiyo, Elizabeth Chenge, amesema mashindano yalikuwa magumu ukiwemo ushindi wa tabu wa mabao 2-1 kwenye nusu fainali dhidi ya Makurumula lakini walicheza vizuri kwa kujituma na kufuata maelekezo ya walimu wao, huku akiomba sapoti ya wadau kuhakikisha wanafanya vizuri kimataifa.

Chanzo: Mwanaspoti