Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ubingwa ni siku ya mwisho ya msimu

City X Gunners Ubingwa ni siku ya mwisho ya msimu

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hatima ya ubingwa wa Ligi Kuu England itafahamika kwenye siku ya mwisho ya msimu, ambayo ni kesho, Jumapili huku ikiwa ni mara ya 10 kwenye historia ya ligi hiyo, mambo kuamriwa siku ya mwisho.

Manchester City ipo kileleni kwenye msimamo wa ligi wakati ikiingia uwanjani Etihad hiyo kesho, lakini sare au kichapo mbele ya West Ham United inaweza kutoa nafasi kwa timu inayoshika nafasi ya pili, Arsenal kuchukua ubingwa, endapo itashinda dhidi ya Everton uwanjani Emirates hiyo hiyo kesho.

Historia inaibeba Man City. Kwa msimu yote, timu ambayo iliingia uwanjani kwenye siku ya mwisho ya msimu ikiwa kileleni, basi ilinyakua ubingwa.

Hata hivyo, hiyo haina maana hakujawahi kutokea mapinduzi na matukio ya kushtukiza kwa timu zilizokuwa nafasi ya pili, kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England kwa siku ya mwisho ya msimu.

Hizi hapa mara tisa, ambazo ubingwa wa Ligi Kuu England ulipambaniwa hadi siku ya mwisho ya msimu.

1994/95

Mambo yalivyokuwa. Blackburn Rovers iliingia siku ya mwisho ya msimu ikiwa na mechi ugenini Anfield kukipiga na Liverpool ikiongoza kwa tofauti ya pointi mbili, walikuwa wakipambana ubingwa dhidi ya Manchester United ilikuwa na mechi dhidi ya West Ham. Man United ilikuwa ikihitaji msaada kwa Liverpool ishinde mechi hiyo. Kama Liverpool itashinda mbele ya Blackburn, kisha Man United ikashinda dhidi ya West Ham, ubingwa utabaki Old Trafford kwa msimu wa tatu mfululizo.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Blackbur 89 Blackburn 89

2.Man Utd 87 Man Utd 88

Ilivyokuwa;

Alan Shearer aliifungia bao la kuongoza kikosi cha Kenny Dalglish, huku huko upande wa pili, Michael Hughes alifunga na kuifanya West Ham kuongoza 1-0 jambo lililoipa Blackburn matumaini ya kubeba ubingwa. Lakini, Brian McClair aliisawazishia Man United kipindi cha pili, kisha John Barnes akaisawazishia Liverpool, hapo Mashetani Wekundu wakapata matumaini ya ubingwa.

Man United ilishambulia, lakini ilishindwa kupata bao jingine la ushindi, huku kwa Blackburn, Jamie Redknapp aliifungia bao la ushindi Liverpool kwa mpira wa adhabu. Filimbi ya mwisho, Man United mechi yao ilimalizika kwa sare, huku Blackburn ilipoteza, lakini taji lilitua kwao.

1995/96

Mwaka uliofuatia ni Man United iliyoingia siku ya mwisho ya msimu ikiwa kileleni. Januari msimu huo na Newcastle ilikuwa kwenye kiwango bora kabisa, iliamini itaichapa Man United kwenye mbio za ubingwa, ambapo ilikuwa ikiongoza kwa tofauti ya pointi 12. Lakini, hadi inafika siku ya mwisho, Man United ilikuwa kileleni kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Newcastle. Man United ilikuwa na mechi ya ugenini dhidi ya Middlesbrough na Newcastle ilikuwa nyumbani kucheza na Tottenham. Newcastle ilihitaji kushinda, huku ikiomba Man United ifungwe ili wao wabebe ubingwa.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man Utd 79 Man Utd 82

2.Newcastle 77 Newcastle 78

Ilivyokuwa;

David May alishusha presha ya Man United baada ya kufunga bao la mapema kabla ya Andrew Cole kufunga la pili na hapo ikaondoa wasiwasi wa kuhusu kubebe taji. Huko kwingine, Jason Dozzell aliifungia Spurs bal la kuongoza, kabla ya Les Ferdinand kuisawazishia Newcastle. Huko kwingine, Ryan Giggs alifungia Man United bao la tatu, huku Newcastle ikibanwa na kutoka sare, hivyo taji likatua Old Trafford.

1998/99

Kipigo cha Arsenal kwenye mechi ya Leeds United, kisha sare ya Man United kwa Blackburn, ilifanya Ligi Kuu England kuingia siku ya mwisho ya msimu timu za kileleni zikiwa zimetofautiana pointi moja tu.

Man United kwenye nafasi ya kwanza na Arsenal ipo namba mbili. Katika siku ya mwisho, Arsenal ilihitaji kuichapa Aston Villa, huku ikiomba mahasimu wao Spurs waichape Man United au kutoka nao sare tu ili wao wachukue ubingwa. Arsenal ilikuwa inatetea ubingwa, lakini Man United walitibua mambo.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man Utd 76 Man Utd 79

2.Arsenal 75 Arsenal 78

Ilivyokuwa;

Kwa dakika 18, Arsenal ilikuwa na uhakika inakwenda kutetea taji lake. Na hilo lilikuja kuongezeka imani baada ya Ferdinand kuifungia Spurs bao la kuongoza dhidi ya Man United na hapo kwa kuwa Man United imesharuhusu bao na Arsenal ilikuwa bado 0-0, pointi zilikuwa sawa 76 na timu zote zilikuwa na tofauti sawa na mabao. Lakini, bao la kusawazisha la Andrew Cole na lile la David Beckham lilifanya Man United kuichapa Spurs 2-1 na kufikisha pointi 79, ambazo hazikufikiwa na Arsenal, ambao ilifunga bao lake kupitia Nwankwo Kanu na kufikisha pointi 78.

2007/08

Timu mbili zilizokuwa zikishindania ubingwa, ziliingia siku ya mwisho ya msimu zikiwa zimelingana pointi. Vita hiyo ya ubingwa ilikuwa ya Chelsea na Man United. Lakini, Mashetani Wekundu walikuwa vizuri kwenye tofauti ya mabao, ambayo iliwafanya kuwa na faida kubwa wakati wanakwenda kukipiga na Wigan na Chelsea wao walikuwa na mechi dhidi ya Bolton Wanderers. Man United ilichokuwa inataka ni kushinda tu kwenye mechi hiyo, wakiamini tofauti ya mabao itawapa taji hata kama Chelsea itashinda.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man Utd 84 Man Utd 87

2.Chelsea 84 Chelsea 85

Ilivyokuwa;

Man United ilianza vyema baada ya kufunga bao kwa mkwaju wa penalti kwenye dakika 20 kupitia kwa Cristiano Ronaldo. Huko kwingine, Andriy Shevchenko aliifungia Chelsea bao la kuongoza na hapo kufanya pointi zao ziwe sawa na Man United. Lakini, Man United ilifunga tena kupitia kwa But Giggs, wakati upande mwingine, Bolton ilisawazisha kupitia kwa Matthew Taylor na kuzima matumaini ya The Blues na msimu ulimalizika kwa bingwa Man United akibeba kwa tofauti ya pointi mbili.

2009/10

Timu zilezile ziliendelea kupambana kwenye mbio za ubingwa, Chelsea na Man United, ambazo ziliingia siku ya mwisho ya msimu zikipambana kuwania ubingwa. Chelsea ilikuwa kileleni kwa tofauti ya pointi moja na mechi yao ya mwisho ilikuwa inakwenda kukipiga na Wigan, wakati Man United yenyewe ilikuwa na kibarua cha kuikabili Stoke City uwanjani.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Chelsea 83 Chelsea 86

2.Man Utd 82 Man Utd 85

Ilivyokuwa;

Chelsea iligoma kabisa kuipa matumaini Man United kwenye mbio hizo na hadi mapumziko, timu hizo mbili, kila moja ilikuwa mbele kwa mabao 2-0. Hadi ilikuwa mbaya kwa Wigan baada ya mchezo wao mmoja kuonyeshwa kadi nyekundu na hapo iliipa nafasi Chelsea kuangusha kipigo cha mabao 8-0 katika mechi hiyo, huku Man United ikiishia kushinda 4-0. Didier Drogba alifunga hat-trick kwa upande wa Chelsea.

2011/12

Mahasimu wawili wa jiji la Manchester, Man City na Man United zikiingia siku ya mwisho ya msimu zikichuana kwenye ubingwa, zikiwa na pointi sawa na kutofautiana kwa mabao tu, ambapo Man City ilikuwa na mabao +12 zaidi ya wapinzani wao kwenye tofauti ya kufunga na kufungwa.

Siku ya mwisho, Man City ilikuwa nyumbani kucheza na QPR, hivyo ilihitaji ushindi ili kushinda taji lao la kwanza la Ligi Kuu England, huku Man United wao walikuwa na kazi ya kuikabili Sunderland.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man City 86 Man City 89

2.Man Utd 86 Man Utd 89

Ilivyokuwa;

Mambo yalionekana yangekuwa tofauti siku ya mwisho ya msimu, wakati Wayne Rooney alipoifungia Man United bao la kuongoza kwenye dakika ya 20 tu ya mchezo. Filimbi ya mwisho inapulizwa huko Sunderland, Man United ilishinda 1-0 na hapo walikuwa na uhakika wa kuwa mabingwa, kwa sababu Man City ilikuwa imebanwa na QPR iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani kufungana 2-2. Mechi ya Man City ilikuwa kwenye dakika za majeruhi, ndipo Sergio Aguero alipofunga bao la ushindi na hivyo kuwafanya Man City kunyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya mabao baada ya pointi kulingana, 89 kila upande.

2013/14

Vita ya ubingwa iliingia siku ya mwisho kwenye msimu huu na miamba iliyokuwa ikichuana ni Liverpool na Man City. Timu hizo zilitofautiana pointi mbili, wakati ligi inaingia siku ya mwisho, ambapo katika siku hiyo ya mwisho, Man City ilikuwa na mechi dhidi ya West Ham United na Liverpool ilikuwa inakipiga na Newcastle. Uzuri timu hizo zilizokuwa zikichuana kwenye ubingwa, kila moja ilikuwa nyumbani.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man City 83 Man City 86

2.Liverpool 81 Liverpool 84

Ilivyokuwa;

Man City haikutaka kuvuruga mambo siku ya mwisho baada ya kushinda 2-0, shukrani kwa mabao ya Samir Nasri na Vincent Kompany. Liverpool yenyewe pia ilipambana na kupata ushindi wa mabao 2-1, ikifunga mabao yake kupitia kwa Daniel Agger na Daniel Sturridge. Ushindi wa Liverpool haikuwa na kitu cha kubadilisha, hivyo ligi ilimalizika kwa timu hizo kutofautiana pointi mbili.

2018/19

Kulikuwa na pengo la pointi moja baina ya timu mbili za juu, Man City na Liverpool. Hivyo, timu hizo zilionyesha ubabe mwingine kwenye siku ya mwisho ya msimu kwenye Ligi Kuu England. Kwenye siku hiyo ya mwisho ya msimu, Man City ilikuwa na mechi dhidi ya Brighton ugenini na Liverpool yenyewe ilikuwa nyumbani kukipiga na Wolves.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man City 95 Man City 98

2.Liverpool 94 Liverpool 97

Ilivyokuwa;

Kwenye mechi hizo, kila timu kwenye mchakamchaka huo wa kuwania ubingwa ilishinda mechi yake, hivyo kuifanya Man City kufanikiwa kutetea ubingwa wake. Liverpool ilitangulia kufunga kupitia kwa Sadio Mane na Brighton waliiduwaza Man United kwa kutangulia kufunga kupitia kwa Glenn Murray.

Lakini, Man City ilicharuka na kushinda mabao 4-1 mechi hiyo, huku Liverpool yenyewe ikiishia kushinda 2-0 na kufanya pengo la pointi kubaki kuwa lilelile, pointi moja.

2021/22

Vita iliendelea kubaki kuwa ileile baina ya Liverpool na Man City kufukaza kwenye mbio za ubingwa hadi mwisho wa msimu. Kila timu ilihitaji matokeo chanya ya mchezo wa mwisho ili kunyakua taji.

Hivyo, kuteleza kwa Man City kwenye mechi ya mwisho, kungeweza kuwapa ubingwa Liverpool endapo kama watakuwa imeshinda dhidi ya Wolves. Man City yenyewe ilikuwa inakipiga na Aston Villa.

Msimamo ulivyokuwa kabla na baada mechi

1.Man City 90 Man City 93

2.Liverpool 89 Liverpool 92

Ilivyokuwa;

Man City ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi moja na ilifanikiwa kushinda mechi ya mwisho mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa, huku Liverpool nao waliichapa Wolves mabao 3-1. Kila timu ilishinda, lakini ubingwa ulirudi Etihad kwa tofauti ya pointi moja, 93 kwa 92.

ITAKUWAJE KESHO?

Man City inaingia siku ya mwisho ya msimu ikiwa kileleni na mbele yao imesimama West Ham United, ambapo kwa miamba hiyo inayonolewa na Pep Guardiola kubeba taji la nne mfululizo, itahitaji kushinda.

Arsenal wao wanaonolewa na Mikel Arteta itakuwa nyumbani kukipiga na Everton. Hivyo, kila upande utaomba mabaya kwa mpinzani wake, huku zenyewe zikisaka ushindi. Timu hizo zimetofuatiana pointi mbili.

Msimamo ulivyo kabla ya mechi

1.Man City 37 +60 88

2.Arsenal 37 +61 86

Man City ibebe vipi ubingwa?

Kama Man City itashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya West Ham United nyumbani, haitajali matokeo ya Arsenal yatakavyokuwa, yenyewe itakuwa imeweka rekodi ya kunyakua taji hilo kwa mara ya nne mfululizo.

Arsenal itabebaje?

Kwa Arsenal wao kumaliza ukame wa miaka 20 ya kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England, itahitaji kuichapa Everton, huku yenyewe ikiomba sare tu kwa Man City na West Ham kama itashindiakana kupoteza kabisa mechi. Sare itawabeba Arsenal kutokana kuwa na wastani mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

-Nini kitatokea pointi zikilingana?

Kama timu zitalingana pointi, mambo yafuatayo yatatazamwa kupata bingwa;

1.Tofauti ya mabao

2.Mabao ya kufunga

3.Timu iliyoshinda pointi nyingine timu hizo zilipokuatana zenyewe

4.Timu iliyofunga mabao mengi ugenini timu hizo zilipokutana zenyewe

5.Mechi ya mchujo kwenye uwanja huru, mfumo ambao utaamriwa na Bodi ya Ligi kwa sababu zao

Chanzo: Mwanaspoti